Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasioona kupiga kura kwa staili hii

Muktasari:

  • Mkutano huo ni sehemu ya mfululizo wa vikao vya tume na wadau wa uchaguzi vinavyoendelea nchini hadi Agosti 3, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani mwaka huu, wenye kauli mbiu ya “Kura yako haki yako, jitokeze kupiga kura.”

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema inaandaa mchakato ili watu wenye ulemavu wa macho (wasioona) watumie karatasi za kura zenye maandishi ya nukta nundu katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo imesema karatasi hizo zitaliwezesha kundi la wasioona kupiga kura wenyewe kwenye uchaguzi huo wa Rais, wabunge na madiwani nchini.

Hata hivyo, kwa wale ambao hawataweza kutumia karatasi hizo, tume imebainisha kuwa wataruhusiwa kwenda vituoni na watu wa kuwasaidia.

Mbali na wasioona, INEC imesema kwa wale wenye ulemavu wa viungo, umewekwa mkakati wa kuwawezesha kupiga kura kwa faragha.

“Wenzetu wenye ulemavu wa viungo ambao hawawezi kusimama na kushindwa kutumia vituturi kama vilivyo, tume imeandaa vituturi ambavyo vikigeuzwa chini juu vitawawezesha watu wenye ulemavu wa viungo kupiga kura kwa faragha,” amesema Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele.

Akizungumza leo, Alhamisi Julai 31, 2025, katika mkutano wa tume hiyo na wawakilishi wa watu wenye ulemavu nchini, uliofanyika jijini Dar es Salaam, Jaji Mwambegele amesema katika kuhakikisha ushirikishwaji kwa watu wenye ulemavu, tume imechukua hatua mbalimbali za kuwawezesha kushiriki kwa ufanisi kwenye uchaguzi mkuu.

Miongoni mwa hatua hizo, Jaji Mwambegele amesema ni maandalizi ya karatasi za kura zenye maandishi ya nukta nundu kwa kundi la watu wasioona, pamoja na vituturi maalumu vinavyowezesha watu wenye ulemavu wa viungo kupiga kura kwa faragha.

“Tume inatambua mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu na itaendelea kushirikiana nanyi ili kuhakikisha mnawekewa mazingira rafiki ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi,” Jaji Mwambegele amewambia wawakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka taasisi mbalimbali.

Katika mkutano huo, Jaji Mwambegele amewahimiza pia watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi na kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani na kuepuka kushiriki katika vurugu au vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa taifa kipindi cha kampeni.

Amesema uzoefu wa chaguzi zilizopita unaonesha kipindi cha kampeni huwa na joto la kisiasa, ambapo baadhi ya watu hujihusisha na vitendo vya uchochezi kutokana na kukosa uvumilivu wa kisiasa, hivyo ni muhimu kwa watu wenye ulemavu kuwa mabalozi wa amani ndani ya jamii.

“Mnapaswa kuwahimiza wenzenu kupitia majukwaa yenu kuwa makini na kuhakikisha hawawi chanzo cha vurugu au uvunjifu wa amani wakati wa kampeni. Kila Mtanzania ana haki ya kushiriki siasa, lakini ndani ya mipaka ya sheria,” amesisitiza Jaji Mwambegele.

Kampeni zimepangwa kuanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025 kwa Tanzania Bara, na Oktoba 27 kwa upande wa Zanzibar.

Katika mkutano huo, uliokwenda sanjari na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani, kuwasilisha mada iliyohusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025 iliyokuwa na vipengele 10, Jaji Mwambegele amesema hoja na changamoto za kundi la wenye ulemavu zitajadiliwa, na tume itapokea ushauri na maoni ya kundi hilo kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Mkutano huo ni sehemu ya mfululizo wa vikao vya tume na wadau wa uchaguzi vinavyoendelea nchi nzima hadi Agosti 3, 2025, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi huo wenye kauli mbiu ya “Kura yako haki yako, jitokeze kupiga kura.”

Akizungumzia mchakato huo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago, amesema hatua ya tume kuweka mikakati ya mazingira rafiki kwa kundi hilo kwenye uchaguzi ni hatua jumuishi kwao.

“Hii inatupa faraja na kuona uchaguzi utakuwa huru na haki, kwani changamoto yetu kubwa huwa ni miundombinu, jambo ambalo Tume imetuhakikishia kulizingatia,” amesema.

Amesema ubora wa vifaa utafanikisha watu wenye ulemavu, hususan wale wasioona na wenye ulemavu wa viungo, kupiga kura kwa siri na kuondoka.

“Matarajio yetu ni kwamba vifaa vitakuwa bora na rafiki,” amesema.

Akigusia kundi hilo wakati wa kampeni, amesema kama shirikisho wamepokea tahadhari ya kutojihusisha na vurugu na wao kuomba wawekewe utaratibu rafiki, mfano kukaa mbele au kivulini kwa wale wenye ualbino, na hata wakati wa kupiga kura wapewe kipaumbele na kutokaa kwenye foleni.