Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya hapa matokeo waliopenya ubunge viti maalumu

Dar /Mikoani. Baadhi ya watiania ubunge viti maalumu wanaomaliza muda wao, katika mikoa minne wamefanikiwa kutetea nafasi hizo kwa kupenya kwenye mchakato wa kura za maoni uliofanyika leo Jumatano Julai 30,2025.

Kura za maoni hizo zimefanyika katika mikoa mbalimbali kupitia mikutano mikuu ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT). Baadhi ya mikoa iliyopata wagombea ubunge viti maalumu ni pamoja na Dar es Salaam, Njombe, Shinyanga na Kilimanjaro.

Mchakato wa kura za maoni ni miongoni mwa hatua za awali, ambapo baada ya hapo watiania walioibuka kidedea watakwenda hatua nyingine kujadiliwa kisha kupitishwa na Kamati Kuu tena.

Katika Mkoa wa Shinyanga, waliokuwa wabunge wa viti maalumu mkoani humo waliomaliza muda wao, wamefanikiwa kutetea viti vyao kwa kuongoza kwa kura za maoni kati ya wagombea wote walioshinda nao.

Akitangaza matokeo hayo  msimamizi mkuu  wa uchaguzi huo, Halima Dendego ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, amesema  uchaguzi huo umefanyika kwa uhuru na  haki.

Dendego amesema aliyeongoza kwenye kura za maoni ni Santiel Kirumba (730) akifuatiwa na Christina Mnzava na Salome Makamba ambaye kipindi kilichopita alikuwa mbunge wa viti maalumu.

Mkoani Dar es Salaam, walioshinda ni Janeth Mahawanga ambaye ni mbunge anayemaliza muda wake huku anayemfuatia Amina Said akiingia kwa mara kwanza.

Msimamizi mkuu wa uchaguzi  huo,  Idrisa Ramadhani amesema katika wagombea tisa waliokuwa wakipigiwa kura Mahangwa ameongoza kwa kupata kura 448 huku Amina kura 421 na Jane Jerry kura akiwa wa tatu kwa kupata kura 300.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, ameibuka mshindi matokeo ya awali ya viti maalumu mkoani Njombe kwa kupata kura 700, akifuatiwa na Rebecca Nsemwa kura 588.

Msimamizi wa Uchaguzi, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa (MNEC) wa Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwanselela amesema wajumbe katika uchaguzi huo waliopaswa kuwepo ni 861, lakini waliohudhuria na kupiga kura ni 841 na kura moja pekee ndiyo imeharibika.

Mwanselela amewataja wagombea wengine kuwa ni Neema Mgaya (263), Anna Mwalongo (53), Dk Scholastika Kevela (47) Tegemea Mbogela (22), Magreth Kyando (5) Tulalumba Mloge (3).

Katika Mkoa wa Kilimanjaro aliyekuwa mbunge wa viti maalumu mkoani humo, Esther Malleko ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 1,149 akifuatiwa na Zuena Bushiri kura 964.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Mjini Moshi, umehusisha wagombea wanane huku wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa UWT wakiwa 1,329.

Matokeo hayo yalitangazwa na msimamizi wa uchaguzi huo, Dk Batilda Burian, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, akiwataja wengine ni  Regina Chonjo (145), Caroline Lyimo (109), Never Zekeya (108), Pamela Mallya(69), Marry Nashanda(19) na Aika Ngowi aliyepata kura(12).

Msimamizi huyo wa uchaguzi, amesema hayo ni matokeo ya awali na kwamba mchakato bado unaendelea.


Sura mpya Arusha

Sura mpya za wabunge wa viti maalumu Mkoa wa Arusha zimeibuka baada ya wajumbe wa mkutano mkuu maalumu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) kufanya uamuzi wa kutowarudisha wabunge waliomaliza muda wao.

Katika uchaguzi uliofanyika jana Jumanne Julai 30, 2025 na matokeo yake kutangazwa usiku, kulikuwa na ushindani mkubwa kati ya wabunge waliomaliza muda wao, Catherine Magige na Zaytun Swai na majina mapya.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi alisema akidi ilikuwa ni wapigakura 1,261 huku waliopiga kura ni 1,252, kura zilizoharibika zilikuwa saba na kura halali 1,245.

Akitangaza matokeo, Kihongosi amesema Marta Kivunge ameongoza kwa kupata kura 1,004 akifuatiwa na Chiku Issa aliyepata kura 775, Catherine Magige (213), Dk Asanterabi Lowasa (196) na Zaytun Seif Swai (141).

Wagombea wengine ni Navoi Mollel (95), Martha Amo (50) na Dk Lillian Badi (9).

“Niwapongeze wagombea wote na wajumbe wa UWT kwa ujumla kwa kuonyesha ushirikiano muda wote wa uchaguzi na hayo ndio matokeo yetu,” amesema Kihongosi.

Baada ya kutangazwa matokeo hayo wagombea hao walishukuru mchakato wa uchaguzi kufanyika katika mazingira huru na uwazi.


Matokeo Iringa

‎Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James ametangaza rasmi matokeo ya kura za maoni kwa nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Iringa huku Rose Tweve akiongoza na kufuatiwa na Nancy Nyalusi.‎

‎Jumla ya wagombea wanane waliwania nafasi hiyo huku kura halali 851 zikipigwa kati ya 852 zilizohesabiwa, na kura moja ikiharibika.‎

‎Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo katika ukumbi wa Masiti uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, ‎amesema katika matokeo hayo, Rose Tweve ameibuka kinara kwa kupata kura 594, akifuatiwa na Nancy Nyalusi aliyepata kura 507. Fatma Rembo alipata kura 326, Seki Kasuga 152, Maria Makombe 59, Tumaini Msowoya 31, huku Lydia Nzema akipata kura 25.‎


Matokeo Simiyu

 Mjumbe wa Baraza la Taifa la Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Tina Chenge, ameibuka kinara katika kura za maoni za kuwania nafasi ya ubunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, baada ya kupata kura 631 kati ya kura halali 1,029 zilizopigwa.

Kura hizo zilipigwa katika Mkutano Maalumu wa UWT Mkoa wa Simiyu uliowakutanisha wajumbe 1,053, kati yao waliopiga kura ni 1,034, kura tano ziliharibika.

Akizungumza baada ya kutangaza matokeo hayo, Kamisaa wa CCM Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni  Mkuu wa Mkoa, Annamringi Macha, amesema kura hizo ni za maoni na si za ushindi wa moja kwa moja, bali zitatumika kama sehemu ya mchakato wa ndani ya chama kuelekea uteuzi wa mwisho.

"Zoezi hili ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa chama kinapata wawakilishi bora kwa ajili ya ubunge Viti Maalumu. Tunasisitiza kuwa hakuna mshindi, hizi ni kura za maoni zitakazowasilishwa ngazi husika kwa hatua zaidi," amesema.

Katika matokeo hayo, wagombea wengine ni Ester Midimu (500), Caritas Machupa kura (312), Minza Mjika kura (292), Rosemary Ng’hwani kura (186).

Wengine ni pamoja na Limi Kilalo kura (60), Jane Masanja kura (50 )na Grace Balele kura (34).

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Alliance mjini Bariadi huku ukihudhuriwa na wajumbe kutoka wilaya zote sita za mkoa huo.


Lindi

Mchakato wa kuwapata wabunge viti maalumu kwa Mkoa wa Lindi umetamatika baada ya mwandishi wa habari Kijakazi Yunus kushinda kwa kura nyingi huku akiwabwaga wakongwe.

Akitangaza matokeo leo Jumatano Julai 30,2025 msimamizi wa uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,  Kanal Patric Sawalla amesema kuwa Kijakazi Yunus amepata kura 942 akifuatiwa na Zainab Kawawa aliyepata kura 492.

"Washindi wetu wa ubunge Viti mMaalum kwa Mkoa wa Lindi ni Kijakazi Yunusi pamoja na Zainabu Kawawa."amesema Kanal Sawalla

Naye Kijakazi Yunus amewashukuru wanawake wa Mkoa wa Lindi kwa kumchagua kwa  kura nyingi huku akiwaahidi ushirikiano uliotukuka.

"Nimegombea hii ni mara ya tatu niwaombe wanawake wenzangu na vijana hatupaswi kukata tamaa ushindi huu ni wetu sote niwahidi ushirikiano ili tuweze kuleta maendeleo katika mkoa wetu wa Lindi."amesema Yunus


Songea

Jacquelin Msongozi ameongoza kura za Maoni  kwenye uchaguzi wa Ubunge Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma baada ya kupata kura za maoni 946 kati ya 1,330 zilizopigwa.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo leo Julai 30, 2025 katika Uwanja wa Majimaji Manispaa ya Songea ambako uchaguzi huo umefanyika , Msimamizi wa Uchaguzi huo, Jabiri Makame amesema kura 1 333 zilipigwa, kura tatu zimeharibika na kura halali ni 1,330.

Amesema, Mariam Nyoka amepata kura (755), Happiness Ngwando (444), Getrude Haule (329) na Laura Hyera ameambulia kura 58.

Wengine ni Sabrina Mbene Lipukila (96), Sophia Gladness Kihalile (12) na Otilia Hyera kapata kura 17.


Morogoro

Mchakato wa kura za maoni kuwapata wagombea ubunge viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani Morogoro umekamilika, huku Lucy Kombani akiongoza kwa kupata kura 1,314 kati ya kura halali 1,646 zilizopigwa, akifuatiwa na Sheila Lukuba aliyepata kura 597.

Katika mkutano huo maalumu wa kura za maoni, jumla ya wajumbe 1,653 kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo, kura 6 zimeharibika na kufanya kura halali kuwa 1,646.

Akitangaza matokeo jana Jumatano Julai 30, 2025 saa tano usiku, Msimamizi wa uchaguzi huo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema shughuli hiyo imehusisha wagombea tisa akiwemo Josephine Kupuna aliyepata kura 454, Jane Claude Mihanji 339, Aliyah Awadh Omar 236, Amina Ally Karuma 153, Hajira Said Mwikoko 90, Kulwa Nuhu Kangeta 75 na Rahel Mashishanga 37.

“Niwapongeze wajumbe kwa hatua hii nzuri tuliyofikia baada ya hapa majina yanaenda ngazi za juu kwaajili ya taratibu za mwisho kwa mujibu wa taratibu za chama chetu cha Mapinduzi,” amesema Malima.

Naye Lucy Kombani amewashukuru wasimamizi kwa kusimamia upigaji kura  wajumbe wote kupiga kura kwa uhuru na haki, huku akiahidi kuunga mkono mipango ya Serikali kwa maslahi mapana ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Mkutano huo maalumu wa UWT Mkoa wa Morogoro umefanyika katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.


Tanga

Wagombea wawili kati ya wanane ambao majina yao yalirejeshwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kuwania nafasi mbili za ubunge wa viti maalumu wanawake Mkoa wa Tanga wameibuka na  ushindi katika kura za maoni viti maalumu, ambapo Husna Sekiboko ameongoza kwa kupata kura 1,637 huku nafasi ya pili ikienda kwa Mhandisi Mwanaisha Ulenge aliyepata kura 921.

Husna na Mwanaisha wameweza kutetea nafasi zao za ubunge wa viti maalumu wanawake Mkoa wa Tanga walizokuwa wakishikilia kipindi hiki kinachomalizika.

Mwantumu Zodo ambaye pia alikuwa miongoni mwa wabunge watatu wa viti maalumu Mkoa wa Tanga kipindi kilichopita, ameshika nafasi ya tatu baada ya kupata kura 772.

Akitangaza matokeo hayo msimamizi wa uchaguzi Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuwa jumla ya wajumbe 1,904 walipiga kura ambapo amewatangaza walioshinda ubunge huo kuwa ni Husna Sekiboko na Mwanaisha Ulenge.

Wakizungumza baada ya kupata ushindi huo, Husna na Mwanaisha wameahidi kusimamia changamoto zinazowakabili wanawake na wakazi wa Mkoa wa Tanga wa ujumla.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa matokeo zaidi.