Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa sababu Katambi kuburutwa mahakamani

Muktasari:

  • Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Tabora, chini ya hati ya dharura dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).



Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Dk Willibrod Slaa wamefungua kesi ya kikatiba kupinga zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Walalamikaji katika kesi hiyo wanapinga tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi la Juni 26, mwaka huu, kuhusu kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, wakidai linakiuka haki za msingi zinazolindwa na Katiba.

Mbali na kesi hiyo, utekelezaji wa zuio hilo umeendelea kuibua maswali kutoka kwa baadhi ya wadau wa siasa, wanaodai kuwapo viashiria vya upendeleo, baada ya baadhi ya viongozi wengine kuendelea kufanya mikutano hadharani.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Tabora, chini ya hati ya dharura dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Pia, wadaiwa wamewaunganisha Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na Wadhamini wa Chama cha ACT-Wazalendo kutokana na masilahi yao katika shauri hilo.

Chanzo cha mgogoro huo ni kauli iliyotolewa Juni 26, 2026 bungeni na Waziri Katambi, alipotangaza kusitishwa kwa utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara nchini.

Katambi alisema hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na sababu za kiusalama na akamwelekeza Mkuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa katika maeneo yote ya nchi.

Walalamikaji wanadai kauli hiyo imeanza kutekelezwa na Jeshi la Polisi na maofisa wake, jambo walilosema limeathiri haki za wananchi kushiriki shughuli za kisiasa na mijadala ya umma.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji wanadai zuio hilo linakiuka ibara mbalimbali za Katiba zinazolinda usawa mbele ya sheria, uhuru wa kujieleza, mawasiliano na ushiriki wa wananchi katika shughuli za umma.

Wanadai pia kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani hana mamlaka ya kikatiba wala ya kisheria kusimamisha au kuzuia haki za msingi zilizotolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kutokana na hoja hizo, wanaiomba mahakama itamke kuwa kauli iliyotolewa kuhusu kusitishwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni batili kwa kuwa inakiuka masharti ya Katiba.

Pia, wanataka mahakama itamke kuwa haki za kikatiba haziwezi kuzuiwa kwa uamuzi wa kiutawala bila kuwepo msingi wa kisheria unaoruhusu hatua hiyo kufanyika.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wanaoundwa na Jaji Isaya Arufani ambaye ni kiongozi wa jopo, pamoja na Majaji Ilvin Mugeta na Martha Mpaze.


Jitihada zashindwa

Hatua ya kufungua shauri hilo, zimeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, kuwa imechukuliwa baada ya jitihada za kutaka tamko hilo liondolewe kushindikana.

"Tulimtaka waziri afute kauli yake, awaombe radhi wananchi na aruhusu mikutano ya kisiasa iendelee. Baada ya kutofanya hivyo, tumeamua kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uhalali wa tamko hilo," amesema.

Henga, amesema haki ya kukusanyika na kutoa maoni ni miongoni mwa haki za msingi zinazolindwa na Katiba pamoja na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini.

Amesema kesi hiyo imefunguliwa chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu pamoja na kanuni zake, ikilenga kupima uhalali wa tamko lililotolewa.

Kwa mujibu wa Henga, shauri hilo halimlengi mtu binafsi bali ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, hivyo mabadiliko yoyote ya viongozi hayatabadilisha mwenendo wa kesi hiyo.


Taifa kurudi nyuma

Kwa upande wake, Dk Slaa amesema ameamua kujiunga katika shauri hilo kama mwananchi anayehofia kutetereka kwa mwenendo wa demokrasia na uhifadhi wa haki za msingi na taifa kurudi nyuma.

"Naumia kuona Taifa letu linaendelea kurudi nyuma katika misingi ya demokrasia. Haki ya kukusanyika na kutoa maoni si zawadi ya mtu yeyote, bali ni haki ya kikatiba," amesema.

Dk Slaa, amesema maendeleo ya taifa yanategemea kuheshimiwa kwa Katiba, sheria na misingi ya utawala bora, akisisitiza kuwa mamlaka yoyote yanapaswa kutenda ndani ya mipaka ya sheria.

Naye, wakili kutoka TLS, Jebra Kambole amesema haki za binadamu haziwezi kusimamishwa kwa uamuzi wa mtu au taasisi, isipokuwa katika mazingira yanayotambuliwa kisheria.

Kambole amesema Katiba imeweka utaratibu maalumu wa kushughulikia hali za hatari za kitaifa na kwamba haki za msingi haziwezi kuondolewa nje ya utaratibu huo.


Viashiria vya upendeleo

Wakati kesi hiyo ikiendelea kusubiri kusikilizwa, baadhi ya matukio ya utekelezaji wa zuio hilo yameendelea kuibua maswali kutoka kwa wadau wa siasa nchini.

Miongoni mwa matukio yaliyoibua mjadala ni lile la Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu wa ACT-Wazalendo, aliyedai kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara jimboni kwake ilhali wabunge wengine wa chama tawala wanaruhusiwa.

Julai 13, mwaka huu, Ado alimwandikia Spika wa Bunge, Mussa Zungu, akilalamikia hatua ya kuzuiwa kufanya mkutano ambao alisema ulikuwa sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

Katika barua hiyo, Ado alisema hatua hiyo inakiuka kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296.

Alisema sheria hiyo inampa mbunge uhuru wa kufanya mikutano katika jimbo lake na inazitaka mamlaka husika kuwezesha shughuli hizo kwa mujibu wa sheria.

Madai hayo yalikuja siku chache baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ayoub Mohamed Mahmoud, kueleza kuwa zuio la mikutano haliwahusu wabunge wanapotekeleza majukumu yao ya uwakilishi.

Ingawa Spika Zungu hajapatikana kuzungumzia barua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alisema polisi walikuwa wanatekeleza tangazo lililotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani.

"Kitu pekee anachoweza kufanya (mbunge) ni mkutano wa ndani, hilo limeruhusiwa, lakini sio mkutano wa hadhara. Maana tangazo lilitangazwa hadharani," amesema Chilya.

Kamanda huyo alisema iwapo kuna mashaka kuhusu utekelezaji wa agizo hilo, viongozi husika wanapaswa kufuata njia rasmi za kupata ufafanuzi kutoka mamlaka zilizolitoa.

Licha ya tukio hilo, baadhi ya wabunge wa CCM wameonekana kuendelea kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao bila kuzuiwa.

Julai 10 mwaka huu, Mbunge wa Makambako, Festo Sanga, alifanya mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Maleutsi akiwa katika ziara ya kawaida ya jimbo.

Pia, Mbunge wa Ikungi Magharibi, Elibariki Kingu alikutana hadharani na waendesha bodaboda na kuwachangia Sh5 milioni kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.

Mbunge wa Nachingwea, Fadhili Liwaka naye ameendelea kufanya ziara na mikutano ya hadhara katika kata mbalimbali za jimbo lake katika kipindi cha zuio hilo.

Mwananchi imempigia simu mara kadhaa Waziri Katambi kwa lengo la kupata maelezo kuhusu madai ya ukiukwaji wa Katiba na tuhuma za upendeleo katika utekelezaji wa zuio hilo, simu yake imekuwa ikiita tu bila kupokewa.

Hata hivyo, waziri huyo aliwahi kunukuliwa akitetea uamuzi wake kuwa hakuvunja sheria, bali alilenga kuhakikisha Tanzania inakuwa salama.