Mamilioni yanayomwagwa kwenye sherehe yazua mjadala, wataalamu waonya
Muktasari:
- Wasema mbali na kuhamasisha matumizi yanayozidi uwezo wa wengi, mazingira hayo yanaweza pia kutumiwa na baadhi ya watu kuhalalisha fedha zilizopatikana kwa njia zisizo halali, jambo linalohitaji macho ya karibu kutoka kwa mamlaka.
Dar es Salaam. Wakati video za watu wakikabidhiwa mafungu ya mamilioni ya fedha kwenye sherehe zikiendelea kusambaa mitandaoni, wachumi na wanasaikolojia wameonya kuwa mwenendo huo unastahili kuangaliwa zaidi ya taswira ya ukarimu.
Wameeleza kwa kina jambo hilo linaweza kuwa na athari kwa uchumi, ustawi wa jamii na hata kuibua maswali kuhusu uwazi wa vyanzo vya fedha. Wanasema tatizo siyo mtu kutoa kiasi kikubwa cha fedha kama zawadi, bali ni pale kunapokosekana mfumo wa kuthibitisha chanzo cha fedha hizo na mazingira hayo yanaweza pia kutumiwa vibaya kuhalalisha fedha zilizopatikana kwa njia zisizo halali.
Katika miaka ya karibuni, imekuwa kawaida kwenye baadhi ya sherehe kushuhudia wageni wakijitokeza mbele ya hadhira na kukabidhi fedha taslimu kwa mwenye shughuli, huku kiasi hicho kikitangazwa hadharani na kurekodiwa kwa ajili ya kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kulingana na wataalamu wa uchumi, tatizo si wingi wa fedha zinazotolewa, bali kutokuwepo kwa mifumo inayoweza kuthibitisha chanzo cha fedha pale inapobidi.
Mbali na kuhamasisha matumizi yanayozidi uwezo wa wengi, mazingira hayo yanaweza pia kutumiwa na baadhi ya watu kuhalalalisha fedha zilizopatikana kwa njia zisizo halali, jambo linalohitaji macho ya karibu kutoka kwa mamlaka zinazosimamia miamala ya kifedha.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Jehovaness Aikael, amesema sheria haimzuii mtu kutoa zawadi ya fedha nyingi ikiwa zimepatikana kwa njia halali na masharti ya kodi yametekelezwa pale inapobidi.
“Huwezi kumpangia mtu kiasi cha kutoa kama zawadi, ilimradi fedha hizo ni halali. Changamoto inakuja pale ambapo hakuna mfumo wa kufuatilia chanzo cha fedha hizo au kama kodi zinazostahili zimelipwa,” amesema.
Amesema kwa mtazamo wa uchumi, fedha nyingi zinapotolewa kama zawadi badala ya kuelekezwa kwenye shughuli za uzalishaji zinaweza kupunguza mchango wake katika uwekezaji, ajira na mapato ya Serikali.
Akizungumzia uwezekano wa sherehe kutumika kama njia ya kutakatisha fedha, Profesa Aikael amesema hilo linaweza kutokea endapo fedha hizo hazijapitia mfumo rasmi wa kifedha.
“Kama fedha haijapita kwenye mfumo rasmi halafu inaletwa kwenye sherehe kama zawadi, inaweza kuwa na viashiria hivyo, hasa ikithibitika ilipatikana kwa namna fulani. Ndiyo sababu haijaingia kwenye mfumo, ila ikiwa fedha inatoka kwenye akaunti ya mtu na iliingia kwa halali kisha akaitoa kumpa mwingine, hapo suala la utakatishaji litahitaji uchunguzi zaidi.
“Ninachoweza kusisitiza ni Watanzania tujitahidi kujifunza elimu ya matumizi ya fedha. Ukweli ni kwamba fedha inayotumika vizuri ni ile inayowekwa kwenye uwekezaji. Hii haina maana wanaotoa zawadi hawana matumizi mazuri,” amesema.
Kwa upande wake, Profesa Abel Kinyondo amesema pamoja na uhalali wa mtu kutumia fedha zake, jamii imeanza kujenga utamaduni wa kupima mafanikio kwa maonesho ya ukwasi badala ya matumizi yenye tija.
“Hata watu wenye kipato cha chini wameingia kwenye mashindano ya kuonyesha uwezo wa kifedha kwenye sherehe, wakati fedha hizo zingeweza kuelekezwa kwenye elimu, afya, makazi, uwekezaji au maeneo mengine yenye uzalishaji.
“Kama tunaweza kuchangia mamilioni kwenye sherehe, kwa nini tusifanye hivyo kwenye elimu kuwasaidia wale wasiokuwa na uwezo, kugharamia matibabu ya wahitaji au hata kuwapatia makazi wasiokuwa na makazi?” amesema.
Naye mchumi Marietha Ngowi amesema kutokuwepo kwa kumbukumbu za nani alitoa fedha, kiasi gani na chanzo chake kunaweza kuvutia watu wenye nia ya kuhalalisha fedha chafu.
“Hatusemi kila anayetoa fedha nyingi anatakatisha fedha. Tunachosema ni kwamba mazingira yasiyo na uwazi yanaweza kutumiwa vibaya,” amesema Marietha.
Kwa upande wake, mchumi Amede Amedius amesema wakati uchumi wa Tanzania ukiendelea kuelekea kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali, kuendelea kutegemea fedha nyingi taslimu kwenye shughuli za kijamii kunapaswa kuwa sehemu ya mjadala wa uwajibikaji wa kifedha.
“Duniani kote shughuli zinazohusisha fedha nyingi taslimu huwekewa uangalizi kwa sababu zinaweza kuficha mwenendo wa fedha,” amesema Amedius.
Profesa Kinyondo amesema wakati umefika kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia namna ya kufuatilia miamala mikubwa ya fedha inayotolewa kwenye sherehe ili kubaini kama kuna wajibu wa kodi unaotekelezwa.
“Katika kipindi hiki ambacho wahisani wamerudi nyuma na tunaambiwa tufunge mkanda, kuna haja ya kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi. Eneo mojawapo ni hili la sherehe, maana kama tuna jamii yenye ukwasi wa watu kutoa mamilioni kwenye zawadi, basi TRA iende ikachukue kodi kwa hao wanaopewa,” amesema.
TRA yafafanua
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, amesema mamlaka hiyo inakusanya kodi na tozo kwenye shughuli za kiuchumi, si za kijamii.
“Sisi tunakusanya kwenye maeneo ya uwekezaji, mfano viwanda, migodi, biashara au hata yakifanyika manunuzi na mauzo ya mali. Kama kinachofanyika si shughuli ya kiuchumi, hatuingii, na ukiangalia harusi au sherehe si shughuli ya kiuchumi,” amesema Kayombo.
Imekaaje kisaikolojia?
Mbali na athari za kiuchumi, wanasaikolojia wanasema maonesho hayo ya fedha yanaacha athari kubwa kwa jamii, hasa kwa vijana na watu wenye kipato cha chini.
Mwanasaikolojia wa kijamii, John Shija, amesema maonesho ya fedha hadharani yanajenga shinikizo la kijamii linalowafanya baadhi ya watu kupima thamani yao kwa kiwango cha fedha wanachoweza kutoa.
“Vijana wanaweza kujiona hawajafanikiwa kama hawawezi kutoa fedha kama wanazoona mitandaoni. Hali hiyo inaweza kusababisha madeni yasiyo ya lazima, msongo wa mawazo na hata kutafuta fedha kwa njia zisizo halali ili kulinda hadhi,” amesema Shija.
Naye mwanasaikolojia Dorothy Banzi amesema baadhi ya watu hulazimika kukopa au hata kuuza mali ili wasionekane wameaibika wanapohudhuria sherehe za ndugu au marafiki.
“Baada ya sherehe kuisha, wanaobeba mzigo wa madeni ni watu wale wale wenye kipato cha chini. Hili linaweza kuongeza migogoro ya kifamilia na kuathiri afya ya akili,” amesema Dorothy.
Amesema mitandao ya kijamii imeongeza kasi ya mwenendo huo kwa kuwafanya wengi kutafuta kuonyesha taswira ya mafanikio mbele ya umma kuliko kuishi kulingana na uwezo wao halisi.