Safari ya demokrasia Tanzania kutoka mwaka 1958 mpaka sasa
Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, utakuwa wa 16 tangu Tanzania ilipoanza kutumia mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Hii ni hatua nyingine muhimu katika historia ya demokrasia ya Taifa, ambayo mizizi yake ilianza kuwekwa zaidi ya miongo sita iliyopita.
Uchaguzi wa kwanza nchini ulifanyika kwa awamu mbili, Septemba 1958 na Februari 1959, kwa ajili ya kuchagua wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (Legco).
Katika uchaguzi huo, viti 30 viligombewa na Chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) kilishinda viti 28, huku vingine 34 vikitolewa kwa njia ya uteuzi.
Uchaguzi uliofuata ulifanyika Agosti 30, 1960, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 885,000, lakini kura halali zilizopigwa zilikuwa 121,445.
Tanu ilizoa kura 100,581 (asilimia 82.82) na kupata viti 70. Vyama vingine vilivyoshiriki ni African National Congress (ANC) iliyopata kura 337 (asilimia 0.28) na mgombea huru, Herman Sarwatt, aliyepata kura 20,527 (asilimia 16.90).
Tanzania ilifanya uchaguzi wake wa kwanza wa Rais Novemba 1, 1962. Waliogombea walikuwa Mwalimu Julius Nyerere wa Tanu, aliyeshinda kwa kura 1,127,978 (asilimia 98.15), dhidi ya Zuberi Mtemvu wa ANC aliyepata kura 21,276 (asilimia 1.85), kati ya kura halali 1,149,254 zilizopigwa.
Baada ya mabadiliko ya Katiba, Tanzania iliingia rasmi katika mfumo wa chama kimoja, Tanu kwa upande wa bara na Afro-Shirazi Party (ASP) Zanzibar, viliungana mwaka 1977 na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hivyo, kuanzia mwaka 1965 hadi 1990, chaguzi zote ziliendeshwa chini ya mfumo wa chama kimoja.
Mwaka 1965, Mwalimu Nyerere alichaguliwa bila kupingwa, huku asilimia 77.1 ya waliojiandikisha (3,373,089) wakijitokeza kupiga kura.
Kura halali zilikuwa 2,499,503, na kati ya hizo, kura za ndiyo zilikuwa 2,410,903 sawa na asilimia 96.46. Katika chaguzi za 1970, 1975 na 1980, Mwalimu Nyerere aliendelea kupita bila kupingwa huku idadi ya wapiga kura na ushiriki ukiendelea kuongezeka na kila uchaguzi kura za ndiyo zilikuwa zaidi ya asilimia 93.
Lakini mwaka 1985 baada ya Nyerere kung’atuka madarakani, Ali Hassan Mwinyi alichaguliwa Rais kupitia uchaguzi uliofanyika Oktoba 27.
Katika uchaguzi mkuu huo, Mwinyi alipata kura za ndiyo 4,778,114 sawa na asilimia 95.68 kati ya kura halali 4,993,740. Uchaguzi wake wa pili ulifanyika Oktoba 28, 1990 na alipita tena bila kupingwa huku akijizolea kura 5,198,120 sawa na asilimia 97.79.
Mchakato huu wa kihistoria umeonesha mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini, kutoka mfumo wa kikoloni hadi uhuru, kisha chama kimoja na baadaye kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Lakini uchaguzi mkuu wa mwaka huu, utakuwa sehemu ya safari hiyo ya kihistoria, ikiwa ni wa tano kufanyika tangu kuanza kwa karne ya 21 na wa 16 kwa jumla, ukiashiria hatua nyingine ya kuimarisha misingi ya demokrasia Tanzania.
Historia inaonesha kuwa uchaguzi uliofanyika mwaka 1990, ulikuwa wa mwisho chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, kabla ya mabadiliko ya Katiba na sheria yaliyofanyika Julai 1992 yaliyoruhusu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya mfumo huo mpya ulifanyika Oktoba 29, 1995. Wakati huo, wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 8,929,969 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 6,846,681 sawa na asilimia 76.7 huku kura halali zilikuwa 6,512,745 na zilizoharibika zilikuwa 333,936.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa alishinda kwa kupata kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82, akifuatiwa na Augustine Mrema wa NCCR-Mageuzi aliyepata kura 1,808,616 (asilimia 27.77), Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) kura 418,973 (asilimia 6.43) na John Cheyo wa UDP kura 258,734 sawa na asilimia 3.97.
Matokeo hayo yalithibitishwa baada ya uchaguzi wa marudio kufanyika Novemba 19, 1995 katika majimbo saba ya Mkoa wa Dar es Salaam, kutokana na kasoro za awali.
Vyama vilivyoshiriki ni CCM, NCCR-Mageuzi, CUF, Chadema, UDP, Ada- Tadea, NRA, UMD, TLP, NLD, UPDP, PONA, na PPT-Maendeleo.
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2000
Watanzania 10,088,484 walijiandikisha kwa ajili ya kupiga kura na waliojitokeza walikuwa 8,517,598 sawa na asilimia 84.4. Kura halali zilikuwa 8,172,284 na zilizoharibika zilikuwa 345,314.
Benjamin Mkapa (CCM) alishinda tena kwa kupata kura 5,863,201 sawa na asilimia 71.74, akifuatiwa na Profesa Lipumba wa CUF aliyepata kura 1,329,077 (asilimia 16.26), Augustine Mrema (TLP) kura 637,115 (asilimia 7.80), na John Cheyo (UDP) kura 342,891 sawa na asilimia 4.20.
Vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo vilikuwa ni CCM, CUF, TLP, UDP, Chadema, NCCR-Mageuzi, UPDP, PONA, Ada- Tadea, UMD, NLD, TPP na NRA.
Uchaguzi wa Desemba 14, 2005
Kwenye uchaguzi mkuu huu, jumla ya wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 16,401,694, waliopiga kura 11,875,927 (asilimia 72.4) na kura halali zilikuwa 11,365,477 na zilizoharibika 510,450.
Katika uchaguzi huo, mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete alipata ushindi mkubwa wa kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28, akifuatiwa na mgombea wa CUF, Profefa Lipumba aliyepata kura 1,327,125 sawa na asilimia 11.68 huku mgombea wa Chadema, Freeman Mbowe akipata kura 668,756 sawa na asilimia 5.88.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo waliopata kura chini ya asilimia moja ni Augustine Mrema wa TLP, Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi), Christopher Mtikila (DP), Emmanuel Makaidi (NLD), Anna Senkoro (PPT), Leonard Shayo (Makini) na Paul Kyara wa SAU.
Uchaguzi wa Oktoba 31, 2010
Waliojiandikisha walikuwa 20,137,303, waliopiga kura 8,626,283 (asilimia 42.8). Kura halali zilikuwa 8,398,394 na zilizoharibika 227,889.
Kikwete (CCM) alishinda tena kwa kura 5,276,827 (asilimia 62.83), akifuatiwa na Willibrod Slaa (Chadema) kura 2,271,941 (asilimia 27.05), Lipumba (CUF) kura 695,667 (asilimia 8.28). Wagombea wengine walipata chini ya asilimia mbili kila mmoja.
Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015
Katika uchaguzi huo, mgombea wa CCM, John Magufuli alipata kura 8,882,935, akifuatiwa na Edward Lowassa aliyegombea kupitia Chadema aliyepata kura 6,072,848.
Wagombea wengine walikuwa Anna Mgwhira (ACT-Wazalendo), Chifu Yemba (ADC), Hashim Spunda (Chaumma), Elifatio Lyimo (TLP), Kasambala Malik (NRA) na Nassoro Dovutwa (UPDP), wote walipata kura chini ya laki moja.
Uchaguzi wa Oktoba 28, 2020
Katika uchaguzi huo, walioajiandikisha kupiga kura walikuwa 29,754,699 kati ya hao, waliojitokeza kupiga kura walikuwa 15,091,950 sawa na asilimia 50.72.
Katika uchaguzi huo, kura zilizoharibika zilikuwa 261,755, hivyo kufanya kura halali kubakia 14,830,195.
Baada ya matokeo kutoka, mgombea wa CCM, John Magufuli alipata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.40, Tundu Lissu aliyegombea kwa tiketi ya Chadema, alipata kura 1,933,271 sawa na asilimia 13.04 na wagombea wengine waligawana kura 380,672 (asilimia 2.57).
Katika uchaguzi huu, wagombea wa urais walitoka vyama 15, wakiwamo
Queen Sendinga (ADC), Bernard Membe (ACT-Wazalendo), John Magufuli (CCM), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Tundu Lissu (Chadema), Cecilia Mwanga (Demokrasia Makini), Hashim Spunda (Chaumma), Seif Maalim Seif (AAFP), John Shibuda (Ada-Tadea), Yeremea Maganja (NCCR-Mageuzi), Philipo Fumbo (DP), Leopard Mahona (NRA), Muttamwega Mgaywa (SAU), Twalib Kadege (UPDP), na Maisha Muchunguzi (NLD).
Uchaguzi huo uliashiria mwitikio mdogo zaidi ikilinganishwa na idadi ya waliojiandikisha, lakini ukabeba ushindani wa kihistoria, hasa kati ya vyama vya CCM na Chadema.
Kwa jumla, historia ya uchaguzi wa vyama vingi nchini imekuwa na ushindani unaoimarika kwa sababu idadi ya wapigakura inaongezeka ikiakisi mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea kuakisi ukuaji wa demokrasia.