Mangi Marealle atoa gari kusaidia kampeni za CCM Kilimanjaro
Muktasari:
- Mangi Marealle pamoja na mke wake wamekabidhi gari hilo Julai 30, mwaka huu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kupokelewa na Katibu wa chama hicho Mkoa, Mercy Mollel.
Moshi. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kutambulisha wagombea wake wa ubunge na udiwani mkoani Kilimanjaro, Mangi wa Marangu, Frank Marealle amekabidhi gari jipya aina ya Toyota Alphard kwa chama hicho mkoani humo, ili kusaidia shughuli za kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Mangi Mareale pamoja na mke wake wamekabidhi gari hilo Julai 30, mwaka huu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na kupokelewa na Katibu wa chama hicho Mkoa, Mercy Mollel pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, Patrick Boisafi.
Frank Marealle ambaye ni Mfanyabiashara mashuhuri na Mangi (Chifu) wa wachanga wa Marangu, aliwahi pia kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania.
Akizungumzia sababu za kukabidhi gari hilo, Mangi Marealle amesema chama hicho kinahitaji gari kwa ajili ya kusaidia shughuli za kampeni za kuomba kura ya Rais mkoani humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro (CCM), Patrick Boisafi, akiwasha gari ambalo limetolewa na Mangi wa Marangu, Frank Mareale kwa ajili ya kusaidia shughuli za kampeni uchaguzi mkuu. Pembeni ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu. Picha na Janeth Joseph
"Mimi binafsi na mke wangu, tulikaa na kuzungumza na kusema tukisaidie Chama cha Mapinduzi na kwamba kinahitaji gari la kwenda kuomba kura maana Rais anachaguliwa na wananchi, hivyo nikaona jukumu hilo ni la wana Kilimanjaro na sio mkuu wa mkoa pekee, ni letu sote, na tukaona tutoe mchango kidogo tusaidiane,"amesema Mangi Marealle
Aidha, amewaomba viongozi hao wa chama kuhakikisha gari hilo linatunzwa ili liweze kukisaidia kwa muda mrefu.
"Naomba mtunze gari hili kama mtoto kwa sababu gari bila matunzo halitaweza kudumu, naomba sana mkishindwa kwenye matengenezo niiteni tu,"amesema Mangi Marealle
Naye mke wa Mariale, Rose Marealle amesema gari hilo litasaidia mambo mengi ikiwemo shughuli za chama za mkoa huo.
Kwa upande wa Boisafi amesema gari hilo limetolewa kwa wakati mwafaka na litasaidia katika shughuli za kampeni.
"Nashukuru sana kwa kuona hitajio la kukisaidia chama chetu katika kipindi hiki cha kampeni, tunajua ni kipindi kigumu lakini tunapoungwa mkono na watu wengi ukiwemo wewe, kwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan umeonyesha kwa vitendo,"amesema Boisafi
Amesema: "CCM Mkoa wa Kilimanjaro tunakushukuru wewe na familia yako, tunajua tumejipanga vizuri lakini tunahitaji msaada kwa watu wengi, maisha au uchaguzi ni namba tunataka mwaka huu wa 2025 tuweke historia kwa kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Katika hatua nyingine Boisafi amesema kwa kipindi cha miaka minne, Rais Samia ametoa fedha za maendeleo zaidi ya Sh1.4 trilioni mkoani humo.
Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu amemshukuru Mangi Mareale kwa moyo wa kujitoa kwa upendo kwa kukisaidia chama hicho na kumuahidi kuwa gari hilo litatumika kama alivyokusudia.
"Nakushukuru sana na mama kwa moyo huu, sio wengi wenye moyo kama wa kwako, kwa ajili ya kufanya kazi za kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu,"amesema Babu.