Prime
Vigogo UWT walivyobwagwa sura mpya zikichomoza
Muktasari:
- Wajumbe wa UWT wamemaliza kazi yao ya kuwachagua wagombea wa viti maalumu kwa CCM, baadhi wakishinda tena, wengine wakianguka; uamuzi wa mwisho unasubiri Halmashauri Kuu ya Taifa.
Dar/mikoani: Mbivu na mbichi sasa zimejulikana. Wajumbe wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ngazi ya mikoa wamehitimisha kura ya maoni ya watiania wa ubunge wa viti maalumu wakiwaacha nje baadhi ya vigogo, wakiwemo wabunge wanaomaliza muda wao.
Hata hivyo, uamuzi huo wa wajumbe si wa mwisho, kwani orodha ya washindi itarudishwa mbele ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo itafanya uteuzi wa mwisho kisha kuwasilisha majina hayo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa ajili ya uteuzi, baada ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Jana, mikoa yote nchini ilifanya uchaguzi kwa ajili ya kuwapata wabunge wa viti maalumu kupitia UWT, ambapo kila mkoa utawakilishwa na wabunge wawili.
Katika matokeo yaliyotangazwa jana usiku, zimekuwepo na sura mpya zilizong’ara kwa kuongoza kwa idadi kubwa ya kura dhidi ya waliokuwa wabunge kwenye maeneo hayo.
Aidha, baadhi ya waliokuwa wabunge wamefanikiwa kutetea nafasi zao kwa kupata kura nyingi.
Baadhi ya waliokuwa wabunge wa viti maalumu ambao kura zao hazikuwawezesha kuingia katika nafasi mbili za juu, ni pamoja na Minza Mjika (Simiyu), Catherine Magige na Zaytun Swai (Arusha) pamoja na Riziki Lulida (Lindi).
Hata hivyo, wapo waliobahatika kutetea nafasi zao kwa ushindi wa kura nyingi, akiwemo Suma Fyandomo na Maryprisca Mahundi (Mbeya), Jacqueline Msongozi na Mariam Nyoka (Ruvuma), Zainab Katimba (Kigoma), Juliana Shonza (Songwe) na Aziza Ally (Kagera).
Sura mpya zilizong’ara
Katika uchaguzi huo Mkoa wa Morogoro, Lucy Kombani pamoja na Sheila Lukuba, ni miongoni mwa sura mpya zilizopenya.
Lucy ambaye ni mtoto wa marehemu Celina Kombani, aliyekuwa mbunge wa Ulanga na Sheila, wamepata kura nyingi zilizopigwa na wajumbe, Lucy akiongoza kwa kura 1,269 akifuatiwa na Sheila aliyepata kura 592.
Katika kinyang’anyiro hicho mkoani Simiyu, Tina Chenge ameibuka kinara katika kura za maoni kuwakilisha mkoa huo, akipata kura 631, akifuatiwa na Esther Midimu aliyepata kura 500.
Akitangaza matokeo hayo, Kamisaa wa CCM Mkoa wa Simiyu ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Anamringi Macha amesema jumla ya wajumbe 1,034 walipiga kura ambapo kura tano ziliharibika.
Tina ambaye ni sura mpya katika kinyang’anyiro hicho, amefanikiwa kuongoza huku aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Esther akifanikiwa kurejea huku mbunge mwingine wa viti maalumu, Minza Mjika akipata kura 292.
Wagombea wengine na kura walizopata ni pamoja na Caritas Machupa (312), Rosemary Ng’hwani (186), Limi Kilalo (60), Jane Masanja (50) na Grace Balele (34).
Mkoani Lindi, mwandishi wa habari Kijakazi Yunus ameongoza katika kura hizo akiwabwaga wakongwe.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Patric Sawalla amesema Kijakazi amepata kura 942 akifuatiwa na Zainab Kawawa aliyepata kura 492.
"Washindi wetu wa ubunge Viti Maalumu kwa Mkoa wa Lindi ni Kijakazi Yunusi pamoja na Zainabu Kawawa," amesema Kanal Sawalla.
Katika kinyang’anyiro hicho wagombea walikuwa sita, wakiwemo Zena Katambo aliyepata kura 362, Teckla Ungele (324), Riziki Lulida (218) na Maimuna Pathan amepata kura 29.
Kwingineko mkoani Arusha, Msimamizi wa uchaguzi huo, Kenan Kihongosi alimtangaza Martha Kivunge kuwa ameongoza kwa kupata kura 1,004 akifuatiwa na Chiku Issa aliyepata kura 775.
Washindi hao walifuatiwa na aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Catherine Magige (213), Dk Asanterabi Lowassa (196) na alikuwa mbunge wa viti maalumu, Zaytun Swai (141). Wagombea wengine ni Navoi Mollel (95), Martha Amo (50) na Dk Lillian Badi aliyeambulia kura tisa.
“Niwapongeze wagombea wote na wajumbe wa UWT kwa ujumla kwa kuonyesha ushirikiano muda wote wa uchaguzi na hayo ndio matokeo yetu,” amesema Kihongosi, mkuu wa mkoa wa Arusha.
Waliotetea nafasi zao
Huko Mwanza, aliyekuwa mbunge wa viti maalumu akiwakilisha mkoa huo, Mary Massanja ameibuka mshindi wa kwanza katika kura za maoni kwa kupata kura 1,040, akifuatiwa na Kabula Shitobelo aliyepata kura 815.
Matokeo hayo yalitangazwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Kagera, Karim Amri akisema jumla ya kura zilizopigwa ni 1,488.
Massanja, ambaye alihudumu kama mbunge wa viti maalumu kuanzia mwaka 2020 hadi 2025, amepata ushindi huo dhidi ya wagombea wengine saba.
Nafasi ya tatu imechukuliwa na Furaha Matondo aliyepata kura 556, wote hao pia walikuwa wabunge wa viti maalumu mwaka 2020 hadi 2025.
Wagombea wengine na kura zao kwenye mabano ni Jesca Nicholas (350), Adellah Mayengela (138), Suzana Kabula (38), Khadija Liganga (22) na Lidia Miyaye (kura 14).
Mkoani Kigoma, Naibu Waziri Tamisemi, Zainab Katimba ameongoza kwa kura 973 akifuatiwa na Amina Mwaipopo (686).
Hata hivyo, Sabreena Sungura ambaye naye alikuwa mbunge wa viti maalumu katika mkoa huo, ameshindwa kutamba akiibuka na kura 71.
Akitangaza matokeo hayo jana usiku, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi amewataja wagombea wengine na kura zao kuwa ni Selina Makebe (176), Ashura Kahoye (89), Amina Kaumo (80), Jackline Rugo (22) na Prisca Mapunda (20).
Matokeo katika Mkoa wa Kagera yanaonyesha aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Aziza Ally ameongoza katika uchaguzi huo kwa kupata kura 1,133 akifuatiwa na Christine Mndeme aliyepata kura 1,011.
Akitangaza matokeo ya wagombea wengine, msimamizi wa uchaguzi huo, Fatuma Mwaasa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, amewataka Rebeka Kashindye (17), Zahara Michuzi (30), Mkuwe Isaya ‘Mamy Baby’ (84), Zuwena Mohamed ‘Shilole’ (104), Dk Bayoum Kigwangala (269) na Jacqueline Kainja (508).
Katika Mkoa wa Ruvuma, Jacqueline Msongozi ameongoza baada ya kupata kura 946 kati ya 1,330 zilizopigwa, akifuatiwa na Mariam Nyoka aliyepata kura (755).
Msongozi na Nyoka walikuwa wabunge wa viti maalumu wakiwakilisha mkoa huo katika Bunge lililopita.
Wengine walioshiriki uchaguzi huo ni Happiness Ngwando (444), Getrude Haule (329) na Laura Hyera (58), Sabrina Lipukila (96), Sophia Kihalile (12) pamoja na Otilia Hyera (17).
Huko Mbeya, waliokuwa wabunge wa viti maalumu, Suma Fyandomo na Maryprisca Mahundi wametetea nafasi zao baada ya kuongoza katika kura zilizopigwa na wajumbe mkoani humo.
Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa uchaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro amewatangaza Suma aliyeongoza kwa kura 1,152 na Maryprisca aliyepata kura 1,150, kuwa washindi.
“Nafasi ya tatu ilishikiliwa na Ikupa Mwaifwami amepata kura 200, Sarah Mwangasa (189), Hobokela Mwankina (72), Tumain Mwakasege (45), Upendo Kalasa (18) na Anna Mwangolombe (7),” amesema Sirro.