Prime
ACT-Wazalendo mtegoni urais wa Mpina, Msajili atia mguu
Dar/Zanzibar. Wakati Chama cha ACT Wazalendo kikiweka msimamo kuhusu kura ya mapema visiwani Zanzibar, kwa upande wa bara kimepewa saa zisizozidi 30, kujibu malalamiko kuhusu taratibu za kumpitisha Luhaga Mpina kuwa mgombea wake wa urais.
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imekitaka chama hicho kutoa maelezo, kutokana na malalamiko ya Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala, anayepinga kupitishwa kwa Mpina kwa kile anachodai kimekiuka kifungu cha 16(4)i, iii na iv, cha Kanuni za Kudumu za Uendeshaji chama toleo la mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kifungu hicho: “Wagombea wa urais/viongozi wa chama katika ngazi ya Taifa anatakiwa awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya wagombea wa chama.”
Aidha, kifungu cha 16 (4) (i), kinasema wagombea urais/viongozi wa chama ngazi ya Taifa, “awe mwanachama wa ACT-Wazalendo kwa muda usiopungua mwezi mmoja kabla ya tarehe ya mwisho ya uteuzi ya mgombea wa chama.”
16(4)(iii) kinasema: “Awe tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kabla ya kuteuliwa kugombea kwa kufuata utaratatibu ulioainishwa katika sehemu ya VI ya nyongeza ya Katiba ya ACT-Wazalendo.
16(4) (iv) “Awe ni mtu aliyethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aonyeshe utayari wa kuisimamia na kuiishi.”
Monalisa anadai Mpina alijiunga na chama hicho Agosti 5 na Agosti 6, 2025 mkutano mkuu ukampitisha kuwa mgombea wa urais, jambo ambalo ni kinyume na kanuni husika.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu ameiambia Mwananchi kuwa wamepokea barua ya msajili na wanaifanyia kazi na wataijibu ndani ya muda waliopewa.
“Tutamjibu Msajili kwa sababu kila kitu kwenye chama chetu kinafanywa kwa kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa na taratibu zetu za ndani,” amesema Ado.
Akijibu swali aliloulizwa wao wanalichukuliaje suala hilo, Ado amesema: “Tunaona ni suala la kawaida kwa sababu kila jambo tulizingatia taratibu na kanuni zote za chama.”
Alipoulizwa ikitokea mgombea akakosa sifa nini wanakipanga, Ado amejibu: “Hatuamini kama hiyo itatokea.”
Mezani kwa msajili
Hatua ya Msajili imekuja siku tano baada ya Monalisa kumwandikia barua Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo juu ya suala hilo, na Jumanne, Agosti 19, 2025 kada huyo amekwenda amewasilisha malalamiko hayo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ofisi ambazo awali alizitumia nakala na kwa katibu mkuu wa Act-Wazalendo.
Katika taarifa yake mpya, Monalisa ameandika akirejea vifungu 6A (2) na 4(5)(b) vya Sheria ya vyama vya siasa.
Kifungu cha 6A(2) kinasema: “Chama cha siasa kitaendeshwa kwa kuzingatia Katiba ya nchi, sheria ya vyama vya siasa, katiba ya chama na kanuni zake.” Kifungu cha 4(5)(b) kinasema, “ofisi ya msajili itakuwa na jukumu la kufuatilia chaguzi na uteuzi wa ndani ya vyama.”
Ameandika anatarajia msajili huyo atazingatia maombi yake na kuyapa umuhimu wa dharura ili kukinusuru chama chake kisikose mgombea halali kulingana na kanuni stahiki.
Hatua hiyo imekuja wakati Mpina akiwa tayari amechukua fomu INEC kuomba kuteuliwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. INEC itafanya uteuzi wa wagombea waliokidhi vigezo Agosti 27.
Ilichosema Ofisi ya Masajili
Akizungumza na Mwananchi leo, Agosti 19, 2025, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema wamepokea barua ya Monalisa na kukielekeza chama husika kitoe maelezo kuhusu yanayolalamikiwa.
“Tumepokea hiyo barua leo (Agosti 19) na tayari tumeshaiandikia ACT Wazalendo barua ili hadi kesho iwe imetoa maelezo kuhusu malalamiko husika,” amesema.
Ukiacha alichoandika Monalisa kupitia barua hiyo, pia alifanya mahojiano na moja ya vyombo vya habari, akieleza kiu yake ya kutaka mtu mwingine apewe nafasi ya kugombea nafasi hiyo.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza, chama hicho kimekuwa kikipokea wanachama kutoka CCM na kuwapa nafasi kisha wanarudi walikotoka, hivyo kutoka suala hilo liachwe.
Julai 2020, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Mje, Bernard Membe alijiunga na ACT-Wazalendo baada ya kufukuzwa ndani ya CCM, Februari 28, 2020. Membe alipitishwa kuwania urais katika uchaguzi mkuu 2020.
Mei 2022, Membe alitangaza kurejea CCM. Mwaka mmoja baadaye mwanadiplomasia huyo mbobevu alifariki dunia Mei 12, 2023.
Wapinga kura ya mapema
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema chama hicho hakiko tayari kuruhusu kupigwa kwa kura ya mapema.
Kauli ya Jussa inakuja siku moja baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutaja kura ya mapema itakayopiogwa Oktoba 28, 2025.
Akifungua kikao cha kamati kuu maalumu ya chama hicho kilichofanyika katika ofisi zake zilizopo Vuga kisiwani Unguja, Jussa amesema wananchi kwa sasa hawatakiwi kuchukua hatua yoyote kuhusu uamuzi huo, hadi chama kitakapotoa mwongozo.
"Suala la kura ya mapema tumeshalipigia kelele sana, hivyo tunachohitaji kwa Wazanzibari ni kuwa watulivu kwa sababu viongozi wao bado tunalifanyia kazi na ikifika wakati tutaelewana kwa kutoa mwongozo," amesema Jussa.
Amesema suala la kura ya mapema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 limesababisha maafa, hivyo chama hicho hakiwezi kuliafiki kwani hawataki yajirudie yaliyotokea awali.
Ameeleza bado wananchi wa Zanzibar wanahitaji mabadiliko ya kweli na hawataacha hadi lengo hilo litimie.
Jussa amesema kati ya mambo matatu waliyohitaji yarekebishwe, ni mfumo wa uchaguzi ikiwemo kura ya mapema.
Mengine, amesema ni fursa ya vitambulisho vya Uzanzibari kwa ambao wamenyimwa na marekebisho ya sektretarieti ya ZEC na kuwa hayo yote hayajatekelezwa.
Hata hivyo, ametoa pongezi kwa wananchi kuwa wavumilivu na kuwa na misimamo thabiti wa kuhitaji mabadiliko na chama hicho ndicho chenye dhima ya kuleta mabadiliko hayo.
Wakati juzi akitangaza ratiba ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, Mwenyekiti wa ZEC, George Joseph Kazi amesema kura ya mapema itapigwa Oktoba 28.
Kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria upigaji kura wa mapema utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi.