Sakata la urais wa Mpina ACT-Wazalendo latua kwa Msajili
Dar es Salaam. Sakata la kupingwa kwa mtiania wa urais wa ACT Wazalendo, Luhaga Mpina limefika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, huku chama hicho kikitakiwa kutoa maelezo kwa ofisi hiyo kesho Jumatano Agosti 20, 2025.
Mzizi wa hilo, ni barua iliyoandikwa na Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala akipinga kupitishwa kwa Mpina kuwa mgombea urais, kwa kile alichosema ni kinyume na kifungu cha 16(1)4)I cha kanuni za kudumu za uendeshaji chama toleo la mwaka 2015.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mwanachama anayewania nafasi ya urais kupitia chama hicho, anapaswa kuwa mwanachama wa zaidi ya siku saba.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Naibu Katibu wa Mawasiliano, Uenezi na Mahusiano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema hayuko tayari kulizungumzia hilo.
“Kwa hili nipo kimya siko tayari kulizungumzia,” amesema Shangwe alipotafutwa kwa njia ya simu.
Awali, alitafutwa katibu mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, simu yake iliita bila majimbu. Vivyo hivyo kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Issihaka Mchinjita.
Mpina alijiunga na chama hicho Agosti 5 na Agosti 6, 2025 akapitishwa na mkutano mkuu uliofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam kuwa mtiania wa urais wa chama hicho.
Tayari Mpina amekabidhiwa fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na anaendelea kutafuta wadhamini wasiopungua 200 kila mkoa katika mikoa 10 ikiwemo miwili ya Zanzibar.
Ndala amemwandikia barua msajili wa vyama baada ya Agosti 15, 2025 kumwandikia Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo kulalamika juu ya ukiukwaji wa kanuni hizo na kumshauri kuzingatiwa kwa kanuni hizo ili kukiepusha chama kukosa mgombea.
Leo Jumanne, Agosti 19, 2025, Ndala amesema ameandikia barua kwa msajili wa vyama, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo kuhusu uvunjifu wa kanuni hizo kumwomba Msajili kufuatilia suala hilo ili chama chake kisikose mwakilishi kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Mwananchi limemtafuta Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza kujua kama barua hiyo ya Ndala imefika na hatua zinazofuta ambapo amesema tayari wamepokea barua hiyo na kukielekeza chama husika kitoe maelezo kuhusu yanayolalamikiwa.
“Tumepokea hiyo barua leo (Agosti 19) na tayari tumeshaiandikia ACT-Wazalendo barua ili hadi kesho iwe imetoa maelezo kuhusu malalamiko husika,” amesema Nyahoza.