Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpina achukua fomu urais INEC, aanza kusaka wadhamini

Mtiania wa Urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina na mgombea mwenza, Fatma Abdulhabib Ferej wakati wa uchukuaji fomu katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuchukua fomu ya uteuzi kuwania nafasi hiyo.

Dodoma. Mtiania wa urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amechukua fomu ya uteuzi katika Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku akisisitiza kuzingatia matakwa ya kisheria kuelekea michakato inayofuata.

Sambamba naye, wengine waliochukua fomu leo Agosti 15, 2025 ni mtiania wa nafasi hiyo wa Chama cha UDP, Saumu Rashid na Haji Khamisi wa Chama cha NCCR Mageuzi, huku kila mmoja akitoa ahadi yake pale atakapopewa ridhaa.

Kati ya watiania wote, ni Mpina pekee hakueleza vipaumbele vyake pale atakapoteuliwa, kwa kile alichoeleza kwamba atayasema hayo wakati wa kisheria utakapofika, lakini sasa amejikita kuomba udhamini kutoka kwa wananchi.


Ilivyokuwa kwa Mpina

Mpina aliyepitishwa kuwa mgombea wa urais wa ACT Wazalendo, Agosti 6, 2025, alifika katika ofisi za INEC saa 9:18 akiambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa chama hicho wakiwa ndani ya vazi la suti.

Amefika katika ofisi hizo akisindikizwa na viongozi wa chama hicho, akiwemo Kiongozi, Dorothy Semu, Katibu Mkuu, Ado Shaibu na wengine wa kitaifa na mikoa.

Upande wa sare haikuwa zambarau kama ilivyo kawaida ya chama hicho, makada na viongozi wote walivalia suti nyeusi na wapo walivalia tai.


Alichosema Mpina

Katika mahojiano yake na wanahabari, Mpina amesema wamepata ushirikiano na mgombea wenza wake, Fatma Ferej wa kukabidhiwa fomu na kwa sababu ni masuala ya kisheria wamezihakiki na kwamba orodha ya vitu muhimu vyote vipo kama inavyopaswa.

"Kazi ni moja kuzunguka katika mikoa kwa ajili ya kupata wadhamini na tunawaomba Watanzania tutakapofika kwenye mikoa wajitokeze kwa wingi kuhakikisha takwa la kisheria tunalikamilisha ili kupata uteuzi wa kuwania urais," amesema.

Amesema anaamini Watanzania watajitokeza kwa wingi bila kujali itikadi za kisiasa.

"Kwa sababu kazi iliyopo ni kutafuta wadhamini. Mambo ya vipaumbele yataelezwa kwa kina baada ya kumaliza jukumu la kuomba wadhamini," amesema.

Amesema kwa sasa anakwenda Kisesa kuomba udhamini na baada ya hapo wanakwenda kwenye mikoa yote kwa ajili ya kuomba udhamini ili kupata uhalali wa kisheria.


UDP

Mtiania wa kiti cha Rais wa chama cha UDP Saum Rashid ameibuka upya sera ya kuwajaza mapesa Watanzania akisema ndiyo wakati wake.

Msafara wa mtiania huyo uliingi saa 3.30 asubuhi akiwa na watu wachache waliokuwa wakiimba nyimbo zenye mahadhi ya moja ya makabila yanayotoka Kanda ya Ziwa.

Hata hivyo, amejitofautisha na watiania wengine kwa namna alivyoingia na wapambe wake kwani ukiacha CCM huyu ni mgombea mwingine aliyekuwa na wasindikizaji watu wazima waume ka wake

"Watanzania watupe nchi ili tukawajaze mapesa, tunavyo vipaumbele vingi lakini hili la mapema muhimu sana," amesema Saumu.

Ametaja njia zitakazopelekea watu kujazwa na manoti ni kuboresha miundombili ikiwemo ya kilimo, viwanda na masuala ya biashara ili kuvusha Nchi katika matatizo ya kiuchumi.


NCCR Mageuzi

Mtiania wa NCCR-Mageuzi, Haji Khamis na mtiania mwenza wake Dk Evaline Munisi waliingia Ofisi za INEC wakiwa na wasindikizani 11.

Miongoni mwa waliowasindikiza alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara Joseph Selasini ambaye walimtangaza kuwa ndiye mgombea mwenza.

Akizungumza na wanahabari, mtiania huyo amesema kuwa ajenda yake kuu itakuwa ni maadili.

"Maadili yameporomika sana, nchi imekosa maadili na kila mmoja anajiona kuwa na ndevu lazima tukakomeshe hilo," amesema Khamis.

Amewataja baadhi ya wasanii akisema wanatunga nyimbo za ajabu akitolea mfano wa wimbo wa 'sisi ni walevi' kwamba zinaharibu kizazi cha leo.

Kwa mujibu wa Khamis, NCCR-Mageuzi wakikabidhiwa nchi, ndani ya siku 100 watakamilisha mchakato wa Katiba kwa haraka na kuanza kufanyia kazi.