Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT - Wazalendo yaja na ilani ya mageuzi 2025 – 2030

Mtiania wa Urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina na mgombea mwenza, Fatma Abdulhabib Ferej wamechukua fomu katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuchukua fomu ya uteuzi kuwania nafasi hiyo.

Muktasari:

  • ACT -Wazalendo imezindua ilani yake ya uchaguzi kwa kipindi cha 2025 hadi 2030, ikiahidi mageuzi katika nyanja za kiuchumi, kijamii, na kisiasa. Ilani hii inazingatia mambo makuu saba yenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa yenye haki, usawa, na kujitegemea zaidi.

Dar es Salaam. Kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, Chama cha ACT - Wazalendo kimezindua ilani yake ya 2025-2030 iliyoahidi mageuzi katika sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa, zaidi ikiazimia kuifanya Tanzania kuwa yenye haki, usawa na kujitegemea.

Katika suala la ajira, chama hicho kimeazimia kutengeneza ajira milioni 12 ndani ya miaka mitano. Ajira hizo zitalenga sekta zenye uwezo mkubwa wa kukua kama vile viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, teknolojia, ubunifu na huduma za kijamii.

Chama hicho kinapendekeza Serikali kuwekeza moja kwa moja kwenye sekta za uzalishaji “na kupunguza utawala wa wachache juu ya rasilimali za taifa.”

Upande wa huduma za kijamii, chama hicho kimedhamiria kutoa bima ya afya kwa wote ili kufikia usawa, bila kujali kipato au eneo wanaloishi mtu.

Chama hicho kimesema kitahakikisha elimu itakuwa bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.

Aidha, kimeahidi kutoa huduma za maji safi na umeme wa uhakika, gesi ya kupikia kwa bei nafuu, na mfumo wa ulinzi wa kijamii unaojumuisha wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi na wakazi wa vijijini.

Upande wa miundombinu, ilani inazungumzia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ya Kusini, ukarabati wa njia za reli za mikoa, na ujenzi wa barabara muhimu kama vile Barabara ya Korosho ili kukuza biashara ya pwani.

Pia, chama kimeahidi kitafanya maboresho ya bandari ikiwemo upandishaji daraja wa bandari muhimu kama vile Mtwara, Tanga, Bagamoyo na Kigoma pamoja na upanuzi wa huduma za umeme, maji na mawasiliano vijijini.

ACT Wazalendo katika ilani hiyo, imesema kutakuwa na utawala bora na haki za binadamu. Kwanza kwa kuanza na mageuzi ya Jeshi la Polisi. Kubadilisha jeshi hilo kuwa jeshi linalohudumia umma.

Vilevile, kufanya mageuzi ya mahakama na sheria. Chama hicho kimeahidi kufanya mageuzi katika mfumo wa Mahakama, kupitia upya sheria kandamizi na kuanzisha mfumo wa haki ya jinai wenye ubinadamu.


Mchakato wa Katiba

Ndani ya miezi sita ya kwanza madarakani, chama kinaahidi kufufua mchakato wa Katiba mpya itakayopunguza mamlaka ya Rais, kuweka wazi utengano wa madaraka na kuunda Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).


Usimamizi wa rasilimali

ACT-Wazalendo inatoa ahadi ya kurejesha ardhi iliyonyakuliwa, kuongeza uwazi katika sekta za uchimbaji madini na kuhakikisha Watanzania wananufaika kwa usawa kutokana na rasilimali za madini, gesi, ardhi na misitu.

Katika suala la uwazi chama hicho kimesema mkataba wowote utakaosainiwa katika sekta ya uchimbaji utawekwa wazi kwa umma.


Nishati na mazingira

Chama kinajizatiti kuongeza uzalishaji wa umeme mbadala, kwa lengo la kuzalisha megawati 9,365 ifikapo mwaka 2030, kutoka vyanzo kama vile umeme wa maji, gesi, na jua.

Aidha, punguzo la umeme ikiwa ni moja ya ahadi ni kupunguza bei ya umeme kwa nusu. Pia, kuimarisha ulinzi wa mazingira na kukuza uchumi wa kijani.


Umoja wa kitaifa na sera za nje

Chama kimejizatiti kuja na muundo wa Muungano utakaohakikisha usawa na kuheshimiana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa upende wa sera ya nje itazingatia mshikamano wa Afrika, ushirikiano wa kimataifa, na haki duniani. Pia ahadi ya kupinga ukandamizaji na ukoloni mamboleo, huku wakionyesha mshikamano na mapambano ya kimataifa kama yale ya Palestina na Sahara Magharibi.


Muungano wa haki

ACT Wazalendo kimeahidi kuimarisha Muungano kwa misingi ya usawa na heshima ya pande zote mbili, kupitia mfumo wa serikali tatu.

Aidha, ilani ya ACT Wazalendo imeahidi kujenga diplomasia ya kimshikamano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa watu wa Afrika; itasimama na kushikamana kupinga uonevu na ukandamizaji wa watu na mataifa ya Palestina, Sahara Magharibi na duniani kote; itaanzisha na kuendeleza uhusiano ya kimataifa yenye maslahi kwa pande zote.


Mazingira, nishati mbadala

ACT Wazalendo inakusudia kujenga uchumi utakaokuza matumizi ya nishati jadidifu, kuboresha mifumo ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuchochea ustawi wa maisha ya Watanzania.

“Tutaongeza uzalishaji wa umeme hadi megawati 9,365 kufikia mwaka 2030 kwa vyanzo vya maji, gesi na jua, huku tukipunguza bei ya umeme kwa asilimia 50,” inaeleza sehemu ya muhtasari wa ilani hiyo.


Huduma za staha

Ilani inatoa mkakati madhubuti wa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji, nishati na hifadhi ya jamii. Inahakikisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wote kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii; elimu bure hadi chuo kikuu, isiyokuwa na michango ya aina yeyote;

“Ilani itahakikisha usambazaji na upatikanaji wa maji na umeme kwenye kila kaya; upatikanaji na unafuu wa gesi ya kupikia; na hifadhi ya jamii kwa wote Taifa,” inasomeka sehemu katika muhtasari huo wa ilani ya ACT Wazalendo.


Waimulika ilani ya ACT

Mjumbe wa kamati ya ilani ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema ilani ya chama hicho imeangazia maeneo mengi muhimu ikiwa na lengo la kuboresha maisha ya Watanzania kupitia sera zinazowajumuisha wote kunufaika na rasilimali zao.

“Chama chetu kinakuja na ilani bora ambayo italiwezesha Taifa hili kuwa la wote, hata walio pembezoni. Tuna rasilimali nyingi ambazo tunazihitaji katika kuchochea uchumi wetu na vizazi vyetu vijavyo,” amesema Nondo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama hicho.

Ameongeza kwamba kwamba masuala ya miundombinu ya kisasa, huduma za jamii kama elimu, maji na afya, usimamizi wa rasilimali za Taifa na mengine mengi, yamepewa nafasi katika ilani hiyo inayotarajiwa kupeperushwa na mgombea urais atakayeteuliwa na INEC.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Zacharia Kanoni amesema ilani ya chama inatakiwa kujikita katika changamoto zinazoikabili jamii na masuala mengine mtambuka ili kutoa mwelekeo wa maisha yao ya baadaye.

“Kama ilani yao imegusa mambo hayo, nadhani chama hicho kitakuwa na nafasi kubwa ya kushindana na vyama vingine katika kunadi sera zao kwa wananchi. Lazima maisha ya mwananchi wa kawaida yaakisiwe katika ilani za vyama,” amesema.

Ameongeza kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa na mambo mengi kutokana na mambo yanayoendelea katika jamii, hata hivyo wananchi wanapenda kusikia wagombea wakieleza namna watakavyokabiliana na changamoto zao.

“Kumekuwa na matukio ya mauaji katika jamii, sasa itakuwa ni jambo la ajabu kama vyama vya siasa havijalibeba jambo hili kama ajenda kwenye uchaguzi. Hii ni muhimu ili kuwahakikishia wananchi ulinzi na usalama,” amesema.