Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Balozi Sefue: Miaka 17 ndani ya kuta za Ikulu, marais wanne

Muktasari:

  • Balozi Ombeni Sefue, mwanadiplomasia aliyefanya kazi kama Msaidizi wa Rais na mwandishi wa hotuba za Rais kuanzia wakati wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi na miaka 10 na Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa.



Miaka 17 nyuma ya marais wanne. Unaposikia mtu yuko karibu na Rais, fikra zinazokuja kichwani ni kwamba anapata raha na kila anachohitaji. Lakini kwake ilikuwa ni tofauti, ni heshima iliyoambatana na wajibu mkubwa.

Balozi Ombeni Sefue, mwanadiplomasia aliyefanya kazi kama Msaidizi wa Rais na mwandishi wa hotuba za Rais kuanzia wakati wa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi na miaka 10 na Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa.

Vilevile, alipanda ngazi na kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, kwa miaka minne, na miezi minne ya Serikali ya awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli, kabla ya kustaafu rasmi mwaka 2016.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Balozi Sefue, akisimulia namna alivyoweza kufanya kazi na viongozi hao, changamoto alizokutana nazo katika kipindi chote cha miaka 17 alichokuwa Ikulu na marais hao.

Balozi Sefue anaeleza kwamba kazi ya kumsaidia Rais ni heshima kwani inaonyesha namna alivyokuamini kumsaidia katika kazi zake. Hata hivyo, anasema kazi hiyo ni ngumu na inatisha tofauti na wengi wanavyodhani.

“Kuwa Msaidizi wa Rais ni kazi ya heshima, lakini ni kazi ambayo inatisha. Unajua ukisikia fulani ni msaidizi wa Rais, ni Katibu Mkuu Kiongozi, wewe unaona zile mbwembwe za kuwa karibu na Rais, lakini…ni kazi ngumu sana,” anasema.

Anasema alipokuwa kijana, akiwa ofisa mdogo katika Ubalozi wa Tanzania huko Stockholm, Sweden, alipigiwa simu na Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akimweleza kwamba anatakiwa Ikulu, taarifa ambayo ilimshtua.

Wakati huo, anaeleza kuwa maofisa walikuwa wanakaa ubalozini miaka minne, ikiisha walitakiwa kurudi nyumbani. Anasema kutokana na maisha kuwa magumu nchini mwanzoni mwa miaka ya 1990, walilazimika kuvuta muda ili wasirudi nyumbani.

Baada ya simu hiyo, anasema alirudi nchini na kwenda moja kwa moja Ikulu kuitikia wito alioitiwa kutoka Stockholm.

“Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, akaniambia unakuwa Msaidizi wa Rais, unachukua nafasi ya Balozi Daraja ambaye alikuwa Msaidizi wa Rais Mwinyi na alikuwa anatakiwa kurudi Wizara ya Mambo ya Nje aende ubalozini.

“Siku ya kwanza unakwenda kutambulishwa kwa Rais sasa, unaweza kufikiria hofu uliyonayo. Kwa sababu ukiwa chini ya mtu mwingine yeyote, ukivuruga watakuhamisha, utakwenda huku, Rais akikukataa unakwenda wapi?” anahoji Balozi Sefue.

Anasema kuwa Msaidizi wa Rais, kila siku lazima iwe kichwani mwako, kwamba “nikiharibu itakuwaje?” Anasema Rais akikukataa hakuna mtu wa kukupokea, labda aamue mwenyewe kukupeleka sehemu fulani.

Balozi Sefue anasema Rais Mwinyi alikuwa kama baba yake, alijua kwamba alikuwa na wasiwasi katika jukumu hilo alilopewa, lakini alimtuliza. Anasema alikuwa akimfanya amuone kama baba yake na siyo kama Rais.

Anasema changamoto yake ya kwanza kwa Rais Mwinyi ilikuwa Kiswahili kwani wakati huo Kiingereza ndiyo ilikuwa lugha rasmi serikalini.

“Sasa unakuja kuwa Msaidizi na mwandishi wa hotuba wa mbobezi wa Kiswahili kama Rais Mwinyi. Unapeleka rasimu ya kwanza inarudi imesahihishwa na wino mwekundu…kwanza inakutisha. Unajaribu tena inaenda, inarudi imesahihishwa.

“Siku moja akaniita, akasema unajua wewe tabu yako ni nini? Mimi naenda kuhutubia kwa Kiswahili, lakini wewe unaanza kufikiri kwa Kiingereza, halafu unatafsiri Kiingereza chako kwa Kiswahili. Akaniambia ni kosa kubwa.

“Akasema kama mimi nakwenda kuzungumza Kiswahili, fikiri Kiswahili, andika Kiswahili. Naenda kuzungumza Kiingereza, fikiri Kiingereza, andika Kiiingereza. Naweza kusema hilo lilikuwa ni somo kubwa ambalo siwezi kulisahau,” anasema.

Anasema baada ya mazungumzo hayo alibadilika na alikuwa akiandika rasimu inarudi safi. Anasema uzoefu huo unawafaa pia watu wa kada nyingine kama waandishi wa habari wanapotafsiri kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na kupoteza muktadha.

Balozi Sefue anasema kazi ya Msaidizi wa Rais ni ya kuaminiwa kwani inabidi kuvaa uhusika kwenye hotuba unazoziandika. Anasema baada ya Rais kusoma hotuba yake, alikuwa akifuatilia vyombo vya habari siku inayofuata ili kupata mrejesho.

Anasema wakati fulani alikuwa akizungumza na aliyekuwa Msaidizi wa Mwalimu Julius Nyerere, Joan Wicken, akamwambia utamu wa kazi hiyo ni ile heshima unayopata kutoka kwa Rais, ya kupangilia anachotaka kuzungumza kwenye hadhara.

Anasema Wicken alimweleza kisa kimoja kilichotokea kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika (OAU) ambapo kuna jambo Mwalimu Nyerere alilizungumza, marais wenzake wakamkosoa. Anasema waliporejea nchini, alikwenda kuandika barua ya kujiuzulu lakini Mwalimu hakukubali.

“Ukitamani kazi hiyo (Msaidizi wa Rais), ni kazi ngumu mno. Wakati mwingine unaweza kukaa saa 24 hujalala. Kwa mfano mko kwenye ziara, kila siku Rais anatakiwa kuzungumza, wenzio wakilala wewe ndiyo unamwandaa kwa ajili ya kesho.

“Kwa hiyo naweza kusema ni kazi ambayo inatia hofu. Inahitaji kweli uwe umejitolea kumhudumia Rais na kwamba siyo wewe ni yeye, lakini ujiweke kwenye nafasi yake na umwandae aweze kufikisha ule ujumbe anaotaka kuufikisha,” anasema Balozi Sefue.


Miaka 10 na Mkapa

Wakati wa Rais Mkapa, Sefue alitarajia kuondoka Ikulu, lakini aliambiwa abaki "kidogo," ahadi ambayo ilidumu kwa miaka 10.

Changamoto kubwa ilikuwa weledi wa Mkapa katika uandishi na usomaji. Ili uwe na tija kwa Mkapa, Sefue anasema ilibidi usome zaidi ya Rais.

“Kila mkisafiri, wenzio wanaenda kununua manukato (perfume), mimi niko kwenye duka la vitabu (bookshop) namtafutia vitabu rais na mimi mwenyewe".

Anasimulia tukio la kipekee Rais Mkapa akiwa anaumwa hospitalini nje ya nchi, lakini akasisitiza kurekodi hotuba ya mwisho wa mwezi ili kuwatoa hofu Watanzania, akisema: “Wananchi wangu watakuwa na wasiwasi.”

Sefue anasema walirekodi hotuba ile huku kiongozi huyo akiwa na maumivu makali, kielelezo cha uongozi usiojijali binafsi.

Balozi Sefue anataja tukio hilo kama moja ya mambo yaliyomjenga na kumwonyesha maana halisi ya uongozi, kwamba kiongozi wa kweli hajijali yeye mwenyewe, bali anajali watu wake kwanza hata anapokuwa katika ugonjwa.


Changamoto alizopitia

Alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi chini ya Rais Kikwete, alikabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Philemon Luhanjo kwa angalizo kuwa “kiti hicho ni moto”.

Akiwa katika kiti hicho, anasema alikumbana na changamoto kubwa kipindi cha ugunduzi wa gesi mkoani Mtwara, ambapo wanasiasa walichochea hofu kwa wananchi kuwa rasilimali hiyo itachukuliwa bila wao kunufaika, jambo lililosababisha mgomo na kauli ya “gesi haitoki”.

Ili kutatua hilo, alilazimika kwenda kusoma kozi maalumu katika Chuo Kikuu cha Cambridge ili kujifunza namna ya kuandaa sheria na sera za mafuta na gesi kwa mataifa machanga katika sekta hiyo.

Anasema uamuzi huo ulizaa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 inayotumiwa kama mfano na nchi nyingine zilizogundua rasilimali hiyo.

Vilevile, anataja mchakato wa kuunda Bunge la Katiba kama wakati uliomnyima usingizi kutokana na ushindani wa makundi yenye maslahi kutaka uwakilishi kwenye chombo hicho ili mwishowe Katiba mpya ipatikane.

Aidha, katika uandishi wa hotuba za Rais, anasema alikuwa na jukumu zito la kuhakiki takwimu na taarifa zinazotoka wizarani kabla hazijamfikia Rais, akijua kuwa ikiwa Rais atasoma taarifa isiyo sahihi, lawama zitamrudia yeye kama msaidizi.


Mambo anayojivunia

Balozi Sefue anasema anajivunia kuwa sehemu ya historia kwa kusaidia kuandika vitabu vya maisha (autobiographies) vya Rais Mwinyi na Rais Mkapa, vikiwa ni kumbukumbu muhimu za maisha ya viongozi hao.

Alishiriki katika kutafsiri kitabu cha Rais Mkapa kwenda Kiswahili baada ya kiongozi huyo kufariki, kazi ambayo Rais Samia aliizindua. Pia, alifanikiwa kukusanya na kuchapa hotuba za viongozi hao katika majuzuu (volumes) mbalimbali, jambo linalohifadhi fikra na uongozi wao kwa vizazi vijavyo.

Kwa mujibu wa Sefue, kuitwa “Ruksa” kwa Rais Mwinyi ilikuwa ni wazo lake la utambulisho (branding) ili kuonyesha kiini cha mageuzi ya kiongozi huyo, licha ya baadhi ya watu kuona kama ni utani. Alama nyingine ni maandalizi ya Sheria ya Mafuta (Petroleum Act).

Balozi Sefue anajivunia kuwa sheria hiyo iliyoandaliwa kwa umakini mkubwa ili isiwatishie wawekezaji huku ikilinda maslahi ya taifa, sasa imekuwa mfano unaoigwa na nchi nyingine nyingi zinazoendelea.

Vilevile, Balozi Sefue alikuwa mhimili mkuu katika kuanzisha na kuendeleza taasisi za kimkakati kama Taasisi ya Uongozi na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC). Taasisi hizi zimelenga kuandaa viongozi wenye fikra za kimkakati kwa ajili ya dunia ya kesho.

Anajivunia kuona viongozi wakibadilika na kuwa na mbinu za kisasa za uongozi baada ya kupitia programu zinazotolewa na taasisi hizo.

Akiwa mwenyekiti wa tume mbalimbali, Balozi Sefue ameacha alama katika mfumo wa kodi nchini kwa Tume ya Rais ya Kutathmini Maboresho ya Mfumo wa Kodi Nchini kutoa mapendekezo 284, ikiwamo lile la kuwapa wajasiriamali wadogo mwaka mmoja wa kutolipa kodi wanapojirasimisha.

Katika mfumo wa haki jinai, anajivunia kubadilisha fikra za magereza kutoka kuwa sehemu ya adhabu pekee na kuwa sehemu ya kurekebisha tabia na kutoa ujuzi kwa wafungwa kupitia vyuo za VETA ili waweze kurudi kwenye jamii wakiwa na manufaa.

Kimataifa, Balozi Sefue anajivunia kuteuliwa na marais wa Afrika kuhudumu katika Jopo la Watu Mashuhuri (Panel of Eminent Persons) la APRM kwa miaka mitano, akitathmini utawala bora barani kote.

“Faraja yangu kubwa ni kuona kuwa mawazo ya marais niliofanya nao kazi yaliwekwa katika lugha na mifumo iliyoleta tija kwa taifa,” anasema.

Siri yake ya kudumu katika majukumu ya Ikulu ni msimamo wake wa “I must deliver” (lazima nitekeleze) aliojiwekea kwa kila jukumu analopewa, bila kukubali kushindwa.