Wagombea ubunge waanza kumwaga ahadi majimboni
Muktasari:
- Profesa Kitila Mkumbo na Abdallah Ulega wazindua kampeni wakitoa ahadi kwa wananchi.
Mkuranga/Dar. Wakati mgombea ubunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega akiahidi kuendelea kufanya mapinduzi ya huduma za kijamii, anayewania nafasi hiyo Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara.
Ahadi hizo wamezitoa leo Septemba 6, 2025 kwa nyakati na maeneo tofauti, kwenye mikutano ya hadhara ya kampeni.
Akihutubia wananchi wilayani Mkuranga, Ulega anayewania ubunge kwa mara ya tatu, amesema katika kipindi cha uongozi wake ameleta mabadiliko makubwa, ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, shule za msingi na sekondari na kuifanya Mkuranga kuwa moja ya maeneo ya kimkakati kitaifa kwenye uzalishaji viwandani.
Akimnadi mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, amesema iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kutafanyika upanuzi wa barabara ya Kilwa, hivyo kupunguza foleni ya kuingia na kutoka Mkuranga kutokea jijini Dar es Salaam.
“Wana-Mkuranga, ninyi ni mashahidi kwamba Mkuranga ya leo si ya jana. Leo umeme umefika kila mahali na sasa tumeanza kujenga shule za ghorofa. Tukimchagua Samia, nitashirikiana naye kuhakikisha kesho ya Mkuranga inakuwa nzuri kuliko leo,” ameahidi.
Amewaomba Watanzania kumchagua mgombea urais wa CCM, akieleza ndiye kiongozi mwenye nia, historia, maono na uwezo wa kuwaletea Katiba mpya.
Amesema ilani ya CCM ya mwaka 2025 -2030 imeahidi kufufua mchakato wa Katiba ya Tanzania na Samia ndiye mgombea urais wake ana sifa za kutimiza ahadi hiyo.
“Watanzania wenzangu, uchaguzi huu unatupa fursa ya kihistoria ya kuchagua mgombea urais anayeweza kutuachia zawadi ambayo itabaki katika kumbukumbu zetu kwa muda mrefu. Zawadi hiyo si nyingine bali ni Katiba mpya ya Tanzania,” amesema.
Jimbo la Ubungo
Profesa Kitila katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Makurumla, amewaomba wananchi jimboni humo kumchagua tena ili atekekeleze vipaumbele mbalimbali, ikiwamo miundombinu ya barabara hasa za mitaani.
“Katika awamu hii ya pili, tutakwenda kuongeza kilomita 25 za mradi wa DMDP, kilomita nane za Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na kilomita 10 za Tarura (Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini),” ameahidi na kuongeza:
“Jumla tutapata kilomita 43 za lami kutoka kilomita 27 za sasa, hadi kufikia kilomita 63 za jimbo la Ubungo. Tunataka kuona asilimia 60 ya barabara za mitaani ziwe za lami ili zipitike muda wote.”
Kuhusu huduma za afya, amesema atahakikisha kinajengwa kituo kipya cha afya cha Mwembeni na zahanati ya Makoka.
“Tutajenga vivuko katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Sahara Mabibo. Tutashughulikia pia changamoto za Mto Gide kati ya Makuburi na Ubungo,” amesema Profesa Kitila, akiahidi pia kushughulikia changamoto za maji.
Profesa Kitila ameahidi ujenzi wa masoko makubwa katika kata za Kimara na Makuburi kutokana na wingi wa wananchi ili kurahisisha huduma.
Akimnadi Ulega, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), Mary Chatanda amesema chama hicho kimewasimamisha wagombea bora, hivyo kina uhakika wa kushinda kwa kishindo uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.