Kimbisa: Dodoma lazima iongoze kura za Rais, Chinyele ataja migogoro ya ardhi
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma Adam Kimbisa akizpungumza katika ufunguzi wa kampeni Jimbo la Dodoma Mjini kata ya Chang’ombe. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam amesema Dodoma inategemea kuwa ya kwanza katika wiki wa kura za Rais lakini haitafikia hapo bila wananchi kujitokeza siku ya kupiga kura.
Dodoma. Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, amesema chama hicho kimejipanga kuhakikisha kinaongoza kwa kura za urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, akibainisha kuwa mkoa huo ni ngome imara ya CCM.
Akizungumza na wanachama na viongozi wa chama hicho Ijumaa, Septemba 5, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Dodoma Mjini, Kimbisa alisema mafanikio hayo hayawezi kufikiwa pasipo ushiriki wa wananchi kwa wingi siku ya uchaguzi.
“Dodoma tunatarajia kuwa wa kwanza kwa kura za urais, lakini hilo haliwezi kufanikiwa kama wananchi hawatajitoa kwa wingi kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025,” alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wote walioteuliwa kugombea kupitia CCM, wabunge na madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali kuhakikisha wanazisaka kura kwa ajili ya mgombea urais wa CCM, Dk Samia Suluhu Hassan, ili chama hicho kiendelee kuongoza.
Katika hatua nyingine, Kimbisa aliwaonya wanachama wa CCM kutosikiliza watu wanaopotosha na kuhamasisha kutoshiriki uchaguzi, akisema tabia hiyo ni sawa na kuidhoofisha CCM kutoka ndani.
“Kupuuza wito wa kupiga kura ni sawa na kuisaliti CCM. Kura yako ni silaha ya ushindi wetu.
“Ili uende peponi lazima ufe. Katika maisha ya siasa, kama kuna kosa la jinai basi ni kosa la kuzila kura. Wanachama wa CCM vunjeni makundi, tusubiri chaguzi zingine ili tugombee,” alisisitiza Kimbisa.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kwa chama hicho, Pascal Chinyele, ameahidi kushughulikia changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo endapo atapewa ridhaa ya kuongoza.
Chinyele alisema moja ya kipaumbele chake ni kuhakikisha tatizo la maji linamalizika ili wananchi wapate huduma hiyo bila usumbufu.
“Kila mmoja wetu anatambua changamoto ya upatikanaji wa maji hapa Dodoma, hivyo tunakwenda kuhakikisha tatizo hili linabaki historia,” alisema.
Mgombea huyo alisisitiza kuwa Serikali kupitia wabunge wake imeweka mkazo katika sekta ya miundombinu ya barabara, na yeye akipewa nafasi atahakikisha barabara za ndani katika jimbo hilo zinawekwa lami ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupunguza adha kipindi cha mvua.
Kingine, amezungumzia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akiahidi kwamba zitatolewa na zinatumika ipasavyo, ili kusaidia wananchi kiuchumi na kuondoa urasimu wa upatikanaji wake.
Kwenye migogoro ya ardhi ambayo ni kilio cha wengi ameahidi kuanza na suala la malipo ya fidia stahiki kwa wanaodai, kwani anatambua namna ilivyo na ukubwa ndani ya jimbo hilo.