Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM Moshi Vijijini yataka nguvu zielekezwe kutafuta kura uchaguzi ukuu

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Siril Mushi akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Sirili Mushi, ametoa rai hiyo leo, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya, kilichofanyika katika ofisi za chama hicho, ambapo amewataka wagombea udiwani kujikita kutafuta kura na kuacha vita ya kusaka uenyekiti wa Halmashauri kwani wakati bado.

Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, kimewaonya wagombea udiwani kuacha vita ya kutafuta nafasi za uongozi ndani ya Halmashauri na badala yake kwa sasa waelekeze nguvu katika kutafuta kura za chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Sirili Mushi, ametoa rai hiyo leo, wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya, kilichofanyika katika ofisi za chama hicho, ambapo amewataka wagombea udiwani kujikita kutafuta kura na kuacha vita ya kusaka uenyekiti wa Halmashauri kwani wakati bado.

Ameonya wagombea kuacha kutumia mbinu za kurubuni au kuhonga wakiamini zinaweza kuwapa nafasi za uenyekiti wa Halmashauri, akisisitiza kuwa chama hakitavumilia vitendo hivyo na kwamba vigezo na taratibu za chama ndizo zitakazoamua nani atakuwa mwenyekiti au makamu mwenyekiti wa Halmashauri.

"Sasa unapoanza kupitapita kurubuni watu na kudanganya watu kwamba watakuwezesha kuwa mwenyekiti wa Halmashauri unajidanganya. Halafu bado hata udiwani hujaupata, unaomba uenyekiti wa Halmashauri, sasa si unajimaliza mwenyewe," amesema Mushi.

Ameongeza kuwa; “nitoe rai hasa kwa madiwani watarajiwa, msijihusishe na kampeni za kuwania nafasi za mwenyekiti au makamu wa mwenyekiti wa halmashauri. Mamlaka hayo hayako kwetu;  wakati ukifika sisi tutapendekeza majina mkoani na baadaye yatapelekwa kamati Kuu kwa uamuzi wa mwisho.”

Pia, amewataka wagombea wote kutambua dhamana waliyoomba kwa wananchi na kuwa na hofu ya Mungu, moyo wa kujitolea na upendo kwa wananchi.

Amesisitiza pia umuhimu wa wagombea kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuepuka kutoa ahadi ambazo hazimo kwenye ilani hiyo.

“Usitoe ahadi nje ya ilani ya CCM. Kama ni ahadi binafsi, hakikisha una uwezo wa kuitekeleza wewe mwenyewe au kwa msaada wa marafiki zako. Kiongozi akiahidi jambo ambalo halitekelezeki, inaleta fedheha kwa chama chetu,” alisema.

Mushi ameongeza kuwa chama hakitaruhusu kugawanyika kwa makundi, kwa kuwa kwa sasa kinapaswa kuwa na mshikamano mmoja wa CCM pekee, huku akiwataka wagombea kuwapenda wananchi na kufanya kazi kwa dhamira ya dhati ya kuwatumikia.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu amesema katika uchaguzi wa mwaka huu, wagombea udiwani 20 kati ya 32 ni wapya  na kwamba wagombea 12 wanatarajiwa kupigiwa kura ya “ndiyo” au “hapana”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava ametoa wito kwa wanachama na viongozi wa CCM kuendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kupiga kura, akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha usalama na amani katika kipindi chote cha kampeni na siku ya uchaguzi.