Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia aahidi kupanga maeneo ya kiutawala baada ya tathmini

Muktasari:

  • Tangu ameanza kampeni zake katika majimbo mbalimbali nchini, Samia amepokea maombi kadhaa kutoka kwa wagombea ubunge wakitaka kupandishwa hadhi kwa halmashauri au wilaya.

Makambako. Kutokana na maombi mengi ya kuanzishwa kwa maeneo mapya ya kiutawala na kupandishwa hadhi, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kwenda kuyapitia upya maombi hayo ili kuona yanayokidhi vigezo.

Samia ametoa ahadi hiyo leo Jumamosi Septemba 6, 2025 aliposimama Makambako kuwasalimia wananchi, baada ya kupokea ombi kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga maarufu kama Jah People, aliyetaka Makambako iwe wilaya.

Tangu ameanza kampeni zake katika majimbo mbalimbali nchini, Samia amepokea maombi kadhaa kutoka kwa wagombea ubunge wakitaka kupandishwa hadhi kwa halmashauri au wilaya.

Akiwa Mbalizi, Septemba 4, 2025, Samia alipokea ombi kutoka kwa mgombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Patali aliyeomba Mbalizi, ambayo ni mji mdogo, ipandishwe hadhi na kuwa mji kamili.

Vilevile, akiwa Njombe, Septemba 5, 2025, mgombea huyo wa urais alipokea ombi kutoka kwa mgombea ubunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika aliyeomba halmashauri ya mji wa Njombe ipandishwe hadhi kuwa manispaa.

Ombi kama hilo limetolewa pia na mgombea ubunge wa Mafinga Mjini, Dickson Lutevele ambaye amemwomba Samia kuipandisha hadhi halmashauri ya mji wa Mafinga kuwa halmashauri ya manispaa kwa kile alichoeleza kuwa mji huo umekua.

Leo, akiwa Makambako, Samia amepokea ombi kutoka kwa Jah People ambaye amemweleza kwamba mji huo umekua na taasisi nyingine za kiserikali zilizopo katika mji huo ni za kiwilaya, imebaki kuwa na utawala pekee.

"Ndugu mwenyekiti, tunakuomba sana, ikikupendeza Makambako tupate wilaya. Taasisi zako zote zilizopo hapa ni za wilaya; polisi ni wilaya, Tanesco ni wilaya, imebaki tu kuwa na utawala kwa maana ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya," amesema Jah People.

Akijibu ombi la Jah People, Samia amesema kutokana na maombi mengi aliyopokea huko alikopita, watakwenda kufanya tathmini na kuangalia maeneo yanayostahili kupandishwa hadhi au kupatiwa mamlaka ya kiutawala.

"Kama mnavyojua, kwa muda mrefu tulizuia kufungua maeneo ya utawala ili kupunguza gharama za kiutawala ndani ya Serikali, lakini maombi yamekuwa makubwa.

"Tutaangalia katika awamu ijayo, wapi haswa panatakiwa kuwa wilaya kwa hadhi zake zilivyo. Amejenga hoja vizuri hapa mwenyekiti (Jah People), kwamba taasisi zote ni za kiwilaya. Ni hoja tutakayoizingatia wakati tunapanga maeneo ya kiutawala," amesema mgombea huyo wa urais.


Maombi ya Chongolo kwa Samia

Akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea ubunge wa Jimbo la Makambako, Daniel Chongolo amesema Makambako ndiyo kitovu cha biashara katika ukanda wa nyanda za juu kusini na nchi jirani kwani huwezi kwenda mikoa ya Mbeya, Ruvuma au Iringa bila kupita Makambako.

Amemshukuru Samia kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa katika Jimbo la Makambako na tayari mkandarasi amepatikana kuanza kazi hiyo. Pia, amemshukuru kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere katika mji huo.

Chongolo amemwomba mgombea huyo wa urais aseme neno kwenye eneo la barabara licha ya kwamba baadhi ya barabara katika mji huo zimejengwa na nyingine ziko kwenye mchakato wa ujenzi.

"Nikuombe mama, useme neno ili Makambako nasi tupate barabara za lami," amesema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza mgombea urais wa CCM.

Kwenye sekta ya kilimo, amesema wakulima wa Makambako wamelima kwa wingi msimu huu, lakini hawana vituo maalumu vya kununulia mahindi, jambo linalowafanya baadhi ya walanguzi kuwalaghai wakulima, hivyo amemuomba Samia aseme neno ili wakulima wafurahi.

"Mgombea wetu wa urais, nikuombe useme neno ili watu wa NFRA (Wakaka wa Taifa wa Chakula) waje kujenga vituo vya kunumulia mazao hapa Makambako," amesema Chongolo.

Pia, mgombea huyo ameomba kujengwa kwa bandari kavu katika jimbo lake na tayari wametenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo katika eneo hilo linalopitiwa na reli ya Tazara.


Samia awaahidi neema

Akijibu maombi ya Chongolo, hususani la vituo vya kununulia mazao, Samia amesema mwezi ujao (Oktoba), watafungua vituo vya kununulia mahindi katika mji wa Makambako ili wakulima wanufaike na jasho lao.

Kuhusu kujengwa kwa bandari kavu Makambako, Samia amesema watalifanyia kazi kwani wamepokea maombi mengi ya kujengwa kwa bandari kavu, hivyo wataangalia wapi panafaa kujengwa kwa bandari kavu.

"Hili la bandari kavu tutalizingatia ni la kulikalia na kuona wapi tujenge bandari kavu. Songwe wameomba bandari kavu na tayari tunajenga, kwa hiyo tutaona ni wapi panastahili kujengwa bandari kavu," amesema Samia.

Mgombea huyo ameahidi kutekeleza yote yaliyoahidiwa katika Mkoa wa Njombe ikiwamo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.