Matumaini mapya kwa wakulima wa chai, parachichi
Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan
Muktasari:
Mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan ameeleza mikakati itakayotekelezwa kuboresha kilimo cha chai na parachachi, pia kuyapatia masoko mazao hayo.
Rungwe. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kumaliza changamoto ya soko la parachichi nchini, huku akieleza hatua zilizochukuliwa kuwakwamua wakulima wa chai wilayani Rungwe wanaomdai mwekezaji wa kiwanda kilichofungwa.
Samia amebainisha mikakati watakayoitekeleza kuhakikisha wakulima wa parachichi na mazao mengine nchini wanajengewa mazingira wezeshi ya kuyafikia masoko kwa uhakika na ubora unaotakiwa.
Akiwa katika mkutano wa kampeni leo Septemba 5, 2025 wilayani Rungwe mkoani Mbeya, amepokea changamoto kutoka kwa wagombea ubunge wa CCM wa majimbo ya Rungwe na Busokelo, wakiwasilisha kilio cha wananchi kuhusu madai yao kwa mwekezaji wa kiwanda cha chai ambaye licha ya kukifunga, anadaiwa na wakulima na waliokuwa wafanya kazi kiwandani.
Mgombea ubunge Jimbo la Rungwe, Antony Mwantona amesema kiwanda cha chai kilichokuwa kikinunua mazao ya wakulima kimefungwa kikiwa kinadaiwa na wakulima, hivyo amemuomba Samia, ambaye ni Rais anayemaliza muda wake awasaidie walipwe stahiki zao.
"Hapa Rungwe, kiwanda cha chai kimefungwa. Wakulima wapatao 15,000 wanakidai kiwanda hiki Sh1.18 bilioni. Tunaomba uingilie kati suala hili ili wananchi wapate fedha zao," ameomba.
Pia, ameomba wasaidiwe kupata soko la parachichi kwa sababu msimu uliopita walikabiliwa na changamoto ya kukosa masoko.
Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Busokelo, Lutengano Mwalwiba amemwomba Samia asaidie kujeresha kiwanda cha chai ili wakulima na wafanyakazi waendelee na shughuli za kujiletea maendeleo.
"Ndugu mgombea, nina maombi maalumu, ombi langu la kwanza ni chai, la pili ni chai na la tatu ni chai. Tuna kiwanda cha chai hapa Rungwe lakini kimefungwa, tunaomba utusaidie ili wananchi wetu wapate maisha," amesema.
Ahadi ya Samia
Akijibu maombi hayo, Samia amesema Serikali ilitoa mashamba kwa wawekezaji, Wetco na Mohamed Enterprises ikiamini inafanya kazi na sekta binafsi.
Amesema Serikali iliweka mazingira mazuri ya uwekezaji, biashara na kufanya kazi, wakakubaliana wakipewa mashamba waweke viwanda vya kuchakata zao hilo. Hata hivyo, amesema kazi hiyo imewashinda.
"Tumeunda timu inayofanya kazi ya kutathmini viwanda na mashamba ili kubaini ambayo hayafanyi kazi, lengo letu kuvimilikisha kwenye vyama vya ushirika chini ya usimamizi wa Serikali ili vizalishe,” amesema na kuongeza:
"Viwanda vingi vya namna hii vinadaiwa na wakulima. Tumewaelekeza waanze kulipa madeni ya watu. Tunakwenda kusimamia, madeni lazima yalipwe."
Kuhusu parachichi amesema zinazolimwa Tanzania zimepata soko kubwa duniani, nchi ikishika nafasi ya tatu Afrika baada ya Afrika Kusini na Kenya.
Hata hivyo, amesema mbali na mataifa hayo kuzalisha zao hilo, mengine pia yanazalisha jambo linalotatiza soko lake.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, amesema Serikali itajenga vituo vya kuhifadhi zao hilo kwa muda ili kusubiri parachichi zipungue sokoni, kwani wazalishaji ni wengi na wote wanazalisha kwa wakati mmoja.
"Tunakuja kujenga vituo 50 vya kuhifadhi parachichi, viwili vitakuwa hapa Rungwe. Vituo hivi vitakuwa na baridi ya kuhifadhi parachichi na mbogamboga kwa miezi mitatu ili kusubiri kabla ya kupeleka sokoni," amesema.
Samia amesema wanakwenda kujenga kongani za viwanda kwenye kila wilaya ili kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na kuwawezesha vijana kuongeza vipato vyao.
Mpango mwingine, amesema: "Tumeamua kuajiri maofisa ugani maalumu kwenye zao la parachichi, tumewapatia vifaa vya kupimia udongo na kutoa huduma za ugani kwa wakulima."
Amesema ruzuku itaendelea kutolewa kwenye zao la parachichi kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya soko.
"Dawa ya kupulizia parachichi itatolewa kwa wakulima bure ili parachichi itoke vizuri, tupate soko la uhakika," amesema.
Mkulima wa parachichi kutoka Kijiji cha Iluti, wilayani Rungwe, Joseph Bukuku amesema kauli ya Samia imekata kiu yake na kurejesha matumaini yaliyopotea.
"Kimsingi ujenzi wa vituo vya kuhifadhia parachichi na utoaji wa miche milioni moja inakwenda kuleta utajiri mkubwa kwa wakulima wa parachichi," amesema.
Kwa nini kura kwa Samia?
Mgombea ubunge Jimbo la Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza ni kwa nini wananchi wamchague Samia, akitaja sababu kadhaa ikiwamo kuwa ni mgombea wa CCM, chama kinachopambana na kero za wananchi.
Sababu nyingine, amesema ni rekodi yake ya uongozi ndani ya miaka minne iliyopita kwani wananchi wameona kazi aliyoifanya katika huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji.
"Amefanya makubwa kwenye sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour. Rungwe ina utalii wa mandhari, ndiyo maana Wajerumani waliipenda," amesema.
Mgombea ubunge Jimbo la Uyole, Dk Tulia Ackson amesema kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM: "Samia pekee ndiye anaweza kutufanya wana-Rungwe tuwe na utulivu... nendeni mkamchague ili muendelee kupata neema. Twendeni tukmpatie ushindi wa heshima."