Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma yaahidi bandari kavu kuhifadhia mazao

Muktasari:

Kwa mujibu wa Chaumma, bandari kavu itajengwa Chekereni, mkoani Kilimanjaro kama eneo la kimkakati la kuvuna fursa za kiuchumi za nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Moshi. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu, ameahidi kujenga bandari kavu ya kuhifadhi mazao ya kilimo eneo la Chekereni, mkoani Kilimanjaro, iwapo atachaguliwa Oktoba 29, 2025 kushika wadhifa huo.

Amesema atajenga eneo hilo kwa kuwa ni la kimkakati katika kuvuna fursa za kiuchumi za nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwalimu amesema bandari hiyo itakuwa na miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi nyanya, vitunguu, mbogamboga, ndizi na parachichi.

Akizungumza leo, Septemba 5, 2025 katika mikutano ya kampeni iliyofanyika Chekereni na Kaaya Mashariki, amesema lengo la kujenga mradi huo ni kuongeza thamani ya mazao, kupunguza upotevu wa chakula na kufungua fursa za biashara na uwekezaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

"Kupitia bandari hiyo, tutaondoa dhana ya kwenda kusafirisha bidhaa zetu nchi jirani. Tutajenga miundombinu yote ya kisasa ya usindikaji na uhifadhi kuanzia hapa Chekereni," amesema.

Mwalimu alieleza hayo baada ya kuelezwa kwamba eneo hilo lina changamoto ya kuhifadhi mazao ili kulifikia soko.

Amesema wananchi watakaopisha ujenzi wa bandari hiyo watalipwa fidia kulingana na thamani ya wakati huo, huku akiahidi kujenga pia barabara ya kisasa itakayounganisha eneo hilo na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Tutapunguza msongamano wa magari kwa kujenga miundombinu bora ya barabara kuunganisha bandari hiyo na KIA, hatua ambayo itarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema

Vilevile, amesema Serikali atakayoiunda haitazingatia matumizi ya kifahari kama vile ununuzi wa ndege au madaraja yasiyo na tija ya moja kwa moja kwa wananchi wa kawaida, bali itajielekeza kujenga uchumi wa maeneo unaotegemea shughuli za wananchi wa kipato cha chini.

“Dhamira yangu ni kupunguza umaskini wa kipato. Serikali yangu haitakuwa ya mafaili ya warsha na safari, bali ya mikakati ya kukuza uchumi wa wananchi,” amesema.

Ameeleza watendaji wa serikali atakayounda hatawaruhusu kuwa na matumizi yasiyo na tija ya rasilimali za umma, akisisitiza kila mtumishi wa umma atapimwa kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa maeneo husika na kuwaondoa wananchi kutoka katika lindi la umaskini.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chaumma, John Mrema, amesema hoja kuwa mgombea urais wa chama hicho (Mwalimu) bado ni kijana hawezi kumudu majukumu ya nafasi hiyo, haina msingi ila ni propaganda.

Amesema uwezo wa kuongoza haupimwi kwa umri bali kwa dira, dhamira na uwezo wa kutetea maslahi ya wananchi.

Mgombea ubunge wa Vunjo, Grace Kihwelu aliyewania nafasi hiyo mwaka 2020 kupitia Chadema na sasa anarudi akiwa Chaumma, amesema ni muhimu kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Vunjo.

"Naijua Vunjo kwa sababu mimi ni mwana-Vunjo. Tunajua changamoto zetu. Tuna barabara fupi ambayo ikijengwa inaweza kutufikisha Moshi Mjini kwa haraka, lakini hakuna kinachoendelea. Mvua zikinyesha ni shida tupu," amesema.

Amesema wakazi wa Vunjo wanalima vitunguu na nyanya lakini wanakosa soko la uhakika, hali inayowakosesha faida licha ya juhudi zao za kujitafutia kipato.

"Tunahitaji mabadiliko ya kweli. Huduma za afya ni changamoto kubwa, lakini Chaumma tukipata dola, watu watatibiwa bure. Kikubwa ni kuwaomba wana-Vunjo watuunge mkono," amesema.

Amesema wananchi wa Vunjo wanastahili kuwa na wawakilishi wanaoelewa changamoto zao na walio tayari kuzitatua, si wale wanaotafuta uzoefu wa kisiasa pekee.

"Wabunge tunaoletewa mara nyingi wanakwenda kupata uzoefu na kurudi. Chagueni Chaumma ili tusiuziwe mbuzi kwenye gunia," amesema.

Ameahidi akipewa ridhaa kuongoza jimbo hilo atahakikisha kuna soko la uhakika la mazao ya wananchi, upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo na wataalamu wa kuwashauri wakulima ili kuongeza tija.