Mwalimu: Kususia uchaguzi ni kuwasaliti wananchi
Salum Mwalimu akihutubia wananchi katika ofisi ya Chaumma Mkoa wa Arusha, leo Ijumaa Agosti 22, 2025.
Muktasari:
- Salum Mwalimu amesisitiza umuhimu upinzani kushiriki uchaguzi, asema kuiacha CCM ipite bila kupingwa ni kusaliti wananchi.
Arusha. Mtiania urais wa Tanzania wa Chaumma, Salum Mwalimu ametoa msimamo wa chama chake kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ili kuwapa haki wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
Mwalimu amemtaja aliyekuwa kiongozi mkuu wa upinzani visiwani Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa alikuwa na msimamo thabiti katika ndoto yake ya kupigania mageuzi Zanzibar.
"Kususia uchaguzi ni kuwasaliti wananchi kwa kuwaachia CCM ipite bila kupingwa, wakose haki ya kuchagua viongozi wa kuwapigania," amesema na kuongeza;
"Maalim Seif Shariff Hamad, alisimama imara, licha ya dosari na mifumo mibovu ya uchaguzi, hakususia uchaguzi, aliamini kuwa CCM haitaondoka kwa kuisusia uchaguzi ili ipite bila kupingwa," amesema.
Ameweka wazi kuwa, chama cha siasa kinachosusia uchaguzi kinakuwa katika hali mbaya inayoweza kukifanya kipoteze nguvu yake ya ushawishi.
"Vyama vikuu vya upinzani vilivyowahi kujiona vimekua vikasusia uchaguzi vingi vimekufa, tumeona Zimbabwe, Morgan Tvangirai alisusa uchaguzi akapotea, Kiiza Besigye wa Uganda alisusa uchaguzi naye akapotea akaibuka Boby Wine, na sisi hatutaingia kwenye huo mtego," amesema na kusisitiza;
"Twendeni kwenye uchaguzi tukapige kura tupate viongozi wazuri tupiganie reforms (mabadiliko) tukiwa kwenye mfumo," amesisitiza.
Mwanasiasa huyo anaendelea na ziara yake mikoa ya kasikazini mwa nchi tangu alipoingia jana Alhamis akitokea Dodoma, katika ziara yake ya kutafuta wadhamini.
Kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge nchini, mtiania wa kiti cha urais anatakiwa kudhaminiwa na Watanzania 200 waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kutoka mikoa isiyopungua 10 nchini, miwili ikiwa ya Zanzibar.