Kampeni za Samia kutua Singida kesho
Muktasari:
- Hadi sasa, Samia amefanya mikutano yake ya kampeni mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa ambako amepata mapokezi makubwa kutoka kwa makada wa chama hicho na wananchi kwa jumla
Dodoma. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuendelea na kampeni zake za uchaguzi kesho Septemba 9, 2025 katika Mkoa wa Singida akitarajiwa kutoa ahadi zake kwa wananchi na kuwaomba kura.
Samia na timu yake ya kampeni wataanza mikutano ya kampeni Jimbo la Bahi lililopo Mkoa wa Dodoma kabla ya kuingia Singida katika majimbo ya Manyoni, Ikungi na Singida Mjini.
Hadi sasa, Samia amefanya mikutano yake ya kampeni mikoa ya Morogoro, Dodoma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa ambako amepata mapokezi makubwa kutoka kwa makada wa chama hicho na wananchi kwa jumla.
Singida ni mkoa wenye jumla ya majimbo manane ya uchaguzi ambayo ni Singida Mjini, Ilongero, Iramba Mashariki, Iramba Magharibi, Ikungi Mashariki, Ikungi Magharibi, Manyoni na Itigi.
Shughuli kubwa za wananchi hao ni kilimo cha mazao ya chakula kama mahindi, mtama, uwele pamoja na alizeti, zao linalowaingiza kwenye biashara ya mafuta ya kura na kujenga uchumi wa viwanda vidogo vinavyotumia malighafi hiyo.
Mkoa huo wenye jumla ya watu milioni 2, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, umekuwa ngome ya CCM kwa muda mrefu na katika uchaguzi mkuu ujao, inatarajia kuvuna kura za kutosha kwa nafasi ya urais, wabunge na madiwani.
Kama ilivyo mikoa mingine, Singida pia inakabiliwa na changamoto za huduma za kijamii kama maji na miundombinu ya barabara, licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuhakikisha huduma hizo zinaboreshwa.
Matumaini ya wananchi katika mkoa huo ni kuona Rais ajaye anahakikisha wanapata maji ya uhakika. Pia, wanatamani wajengewe barabara za ndani za kutosha ili mji huo ukue na uwe na mwonekano mzuri.
"Singida hatuna wasiwasi kabisa, kule ni ngome yetu kama ilivyo hapa Dodoma. Mama (Samia) amefanya kazi kubwa ya kusogeza huduma kwa wananchi, hiyo tu inatosha kumfanya apate kura za kishindo katika mkoa huo," amesema Leonard Nkungu, kada wa CCM anayeishi Dodoma.
Fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Singida ni pamoja na uwezekao wa kuvuna umeme wa upepo, moja ya vyanzo vya nishati safi inayopigiwa chapuo na mgombea huyo wa urais kupitia CCM.
Pia, kilimo ni fursa kwa wananchi wa Singida kwenye mazao yenye soko kama alizeti, mahindi na uwele.
Wakati CCM kikiendelea na kampeni zake, vyama vingine pia vinaendelea kufanya kampeni katika mikoa mbalimbali nchini.
Kampeni hizi zitakazochukua miezi miwili, zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, 2025 na Oktoba 29, 2025 ndiyo siku ya kupiga kura.
Mshindi katika uchaguzi huo, anatarajiwa kuunda Serikali itakayoliongoza Taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hadi sasa, wagombea 17 wameteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.