Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma: Bima ya afya itajumuisha kifurushi cha chakula

Mgombea Ubunge Dodoma Mjini, Aisha Madoga

Muktasari:

  • Chama hicho kimesema endapo kitaunda Serikali chakula kitakuwa sehemu ya matibabu kwenye bima ya afya.

Dodoma. Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Devotha Minja, amesema iwapo chama hicho kitaingia madarakani, bima ya afya kwa Watanzania itakuwa na kifurushi cha chakula, ili kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora sambamba na huduma za afya.

Akizungumza leo Jumapili, Septemba 7, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Dodoma Mjini, Minja amesema Serikali ya Chaumma italeta hati punguzo kwenye vyakula muhimu badala ya bidhaa zisizo na kipaumbele kwa wananchi.

“Mtu mwenye njaa hawezi kufikiri kuhusu vyandarua vilivyopunguzwa kodi, bali anahitaji shibe. Ndiyo maana tumesema kila bima ya afya itakayokuwa inamilikiwa na Mtanzania lazima iwe na kifurushi cha chakula. Wanaohitaji vyandarua ni wale waliokwisha shiba, si watu wenye njaa,” amesema, huku akishangiliwa kwa kauli na wananchi waliosikika wakisema, “inawezekana!”

Mbali na hilo, Minja ameahidi kuwa hati punguzo pia zitatolewa kwenye vifaa vya ujenzi, ili kila mwananchi amudu gharama za kujenga makazi bora.

Amesema ndani ya kipindi kifupi baada ya kuingia Ikulu, Chaumma itashughulikia changamoto ya ajira pamoja na tatizo la upatikanaji wa chakula, akisisitiza kuwa bima ya afya ya wote haitakuwa kama ilivyo sasa, akitaja kwamba inakabiliwa na changamoto lukuki.

Aidha, amebainisha kuwa chama hicho kimejipanga kulifanya Jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kuchimba visima vitakavyosaidia kilimo cha umwagiliaji na upatikanaji wa maji ya uhakika.

Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa Dodoma Mjini kupitia Chaumma, Aisha Madoga, amesema anafahamu changamoto zinazowakabili wakazi wa jimbo hilo, likiwamo la ardhi, ukosefu wa huduma bora za kijamii na mifumo mibovu ya maji taka.

“Mitandao ya maji taka imejaa na kuathiri wakazi wa Dodoma ambao hulipa kodi kila siku. Nitahakikisha ninasimama kwa niaba ya wananchi kuwasemea matatizo yao na siyo kuwatetea viongozi waliopo madarakani,” amesema mgombea ubunge huyo.

Madoga amewaomba wananchi kumpa ridhaa ili awe sauti ya kweli ya wananchi bungeni, akisisitiza kuwa hawapaswi kuwapa majukumu watu wasioweza kuyatekeleza.

Naye Katibu wa Chaumma Mkoa wa Dodoma, Mathias Nyakapala, amesema chama cha siasa kazi yake ni kusimamia ilani, hivyo atahakikisha ahadi za Chaumma zinasimamiwa ipasavyo bungeni kwa maslahi ya wananchi.

Amesema changamoto ya wafanyabiashara kutozwa tozo nyingi inatokana na viongozi waliopo kushindwa kuwajibika, na akasisitiza kuwa Chaumma italeta mabadiliko yatakayowanufaisha wananchi wote.