Mayele aipeleka Pyramids fainali CAFCL, Mamelodi yaivua ubingwa Ahly

Muktasari:
- Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika anapata kiasi cha Dola 4 milioni na mshindi wa pili anapata Dola 2 milioni.
Dar es Salaam. Mshambuliaji Fiston Mayele ameibuka shujaa wa Pyramids FC baada ya kuifungia mabao mawili likiwemo la ushindi dhidi ya Orlando Pirates katika mchezo ambao timu yake imepata ushindi wa mabao 3-2 leo, Aprili 25, 2025 katika Uwanja wa Juni 30 jijini Cairo, Misri.
Mayele alifunga bao hilo la ushindi la Pyramids FC katika dakika ya 84 akimalizia kwa shuti kali mpira uliotemwa na kipa Sipho Chaine wa Orlando Pirates.
Ni mchezo ambao Pyramids FC ililazimika kusawazisha mara mbili baada ya kutanguliwa kufungwa mabao na baadaye ikapata bao la ushindi kupitia Mayele.
Orlando Pirates walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Relebohile Mofokeng ktika dakika ya 41 lakini Mayele alisawazisha katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.
Orlando Pirates walipata bao la pili katika dakika ya 52 kupitia kwa Mohau Nkota ambalo lilisawazishwa na Ramadan Sobhi katika ya 57.
Iliwalazimu Pyramids kusubiria bao la tatu la Mayele ambalo limewavusha kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 kwa vile mechi ya kwanza ambayo timu hizo zilicheza Afrika Kusini wiki iliyopita ilimalizika kwa sare tasa.
Katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri, wenyeji Al Ahly walivuliwa ubingwa na Mamelodi Sundowns baada ya mechi baina yao kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mamelodi wamebebwa na kanuni ya bao la ugenini kwa vile mechi ya kwanza ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Al Ahly ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mohamed Taher lakini katika dakika ya 89, mchezaji wao Yassr Ibrahim alijifunga na kuipatia Mamelodi Sundowns bao lililowavusha.
Katika fainali, Mamelodi Sundowns itaanzia nyumbani Pretoria, Afrika ya Kusini, Mei 24, 2025 na mechi ya marudiano, Pyramids FC itakuwa nyumbani Cairo, Juni Mosi mwaka huu.