Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Muungano: Siku 22,280 za majaribu, mikasa na ushindi

Leo, Aprili 26, 2025, imetimia miaka 61 tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane kupata dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambayo kuanzia Desemba 1964 ilianza kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mzunguko wa Kalenda ya Gregory, ambayo inatumika Tanzania na sehemu kubwa ya ulimwengu, mwaka mmoja una siku 365, halafu kila baada ya miaka minne, mwaka unakuwa na siku 366. Kimahesabu, miaka 61 ni siku 22,280.

Hesabu hizo zinakupa wiki 428 na siku tano tangu Muungano uzaliwe. Tarakimu hizo zimetimia baada ya majaribu mengi. Kutimia kwa miaka 61, maana yake ushindi dhidi ya majaribu mengi. Kuweka kumbukumbu sawa, Hati ya Muungano ilisainiwa Aprili 22, 1964.

Muungano wa Tanzania unabaki kuwa kielelezo cha kipekee Afrika. Serikali ya Shirikisho la Ethiopia na Eritrea, ilidumu kwa miaka 10 tu; Septemba 15, 1952, mpaka Novemba 14, 1962. Kisha zikafuata nyakati za vita na kuwindana kwa miaka takriban 20.

Shirikisho la Senegal na Gambia (Senegambia Confederation), lilisainiwa Desemba 12, 1981, likazaliwa rasmi Februari 1, 1982, halafu likavunjika Septemba 30, 1989. Hesabu inaleta majibu kuwa Senegambia haikufikisha hata miaka minane.

Kuna Muungano wa Dola za Kiafrika (Union of African States) au Muungano wa Ghana, Guinea na Mali, uliohusisha nchi tatu; Ghana, Guinea na Mali. Ulizaliwa Novemba 23, 1958, ukafa Mei 1963. Uhai wake ulikuwa miaka minne na miezi sita.

Mifano ya muungano wa nchi na mashirikisho, kuzaliwa kwake hadi kufa, ni kuonesha upekee wa Muungano wa Tanzania ulivyoweza kutimiza miongo sita, na tayari upo kwenye moja ya 10, kuelekea kutimiza miongo saba.

Zipo sababu nyingi za kudumu kwa Muungano wa Tanzania, mojawapo ikiwa ni undugu asilia wa Watanzania wa pande zote, lakini muhimu zaidi ni misingi iliyojengwa kwa nguzo za kuushikilia Muungano.

Kuuleta mfano wa karibu, Muungano wa Ghana, Guinea na Mali ulivunjika kwa sababu ya kile ambacho Rais wa Guinea wakati huo, Ahmed Sekou Toure, alikieleza kwamba aliyekuwa Rais wa Ghana, Kwame Nkrumah, aliamua mambo kivyake bila kushirikisha wenzake. Rais wa Mali, Modibo Keita, naye akashikilia dola yake.

Muungano wa Tanzania ulizaliwa kwa maafikiano ya pande mbili; Rais wa Tanganyika akiwa Mwalimu Julius Nyerere, Zanzibar ikiongozwa na Sheikh Abeid Karume. Kisha, Nyerere akawa Rais wa Tanzania, Karume Makamu wa Rais wa Tanzania, vilevile Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Nyerere alibaki kuwa Rais wa Tanzania, wakati Zanzibar ilibadili marais watatu: Karume, Sheikh Aboud Jumbe na Ali Mwinyi. Halafu, Mwinyi akawa Rais wa Muungano, Zanzibar ikibadili marais wawili: Idris Wakil na Salmin Amour.

Rais wa Tatu wa Tanzania, Benjamin Mkapa, aliongoza kipindi ambacho Zanzibar ilibadili marais wawili: Amour na Amani Karume. Rais wa Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, alifanya kazi na marais wawili wa Zanzibar: Karume na Dk Ali Shein.

Rais wa Tano, Dk John Magufuli, alifanya kazi na marais wawili wa Zanzibar, Dk Shein na Dk Hussein Mwinyi kwa kipindi kifupi, halafu Rais Samia Suluhu Hassan anaongoza dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwa na Dk Mwinyi.

Mabadiliko ya viongozi, zama kwa zama, bila Muungano kutetereka au kuwepo mazingira ya kukaribia kuvunjika, inatosheleza kutoa sifa kwa misingi iliyojengwa, licha ya ukweli kwamba manung’uniko yamekuwepo kipindi chote cha miaka 61.


Majaribu ya nyakati

Ipo nusura ya Muungano isiyoimbwa. Ni zama za chama kimoja na kuzaliwa kwa CCM, Februari 5, 1977, yakiwa ni matokeo ya kuviunganisha vyama vya Afro Shiraz Party (ASP) na Tanganyika African National Union (Tanu).

Mwaka 1984, Muungano wa Tanzania uliingia kwenye majaribu, baada ya Jumbe (Rais wa Zanzibar), kugundulika alikuwa na rasimu ya Katiba kibindoni, iliyobeba mapendekezo ya dola yenye serikali tatu.

Suala la Jumbe lilishughulikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM, Dodoma. Hali ingekuwaje kama CCM ingekuwa haijazaliwa? Jumbe angekuwa Mwenyekiti wa ASP, Nyerere Tanu. Halmashauri ya chama gani ingemshinikiza Jumbe kujiuzulu nyadhifa zote kwa tuhuma za usaliti wa Muungano?

Pengine, Jumbe angeondolewa kwa nguvu ya dola, ama kwa kulazimishwa kujiuzulu urais wa Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, au angewekwa kando kijeshi. Tendo lolote kati ya hayo lingebeba tafsiri ya mapinduzi.

Sakata la Jumbe, na matukio ya baadaye kama vile madai ya uwepo wa mpango wa kuuvunja Muungano na dhoruba la mpasuko visiwani mwaka 1988, lililosababisha aliyekuwa Waziri Kiongozi, Seif Sharif Hamad, kuvuliwa uanachama wa CCM, ni picha dhahiri kuwa kuzaliwa kwa CCM kulibeba nusura ya majaribu mengi ya Muungano.


Majaribu ya kibunge

Tanganyika haina Bunge wala Serikali. Vuguvugu la wabunge wa Tanzania Bara (Tanganyika), maarufu kama G55, kudai Serikali ya Tanganyika na Bunge lake nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano miaka ya 1990, lilizimwa na Mwalimu Nyerere.

Hali ya Tanganyika kukosa Bunge na Serikali husababisha wabunge wa Tanzania Bara wadhani Bunge la Tanzania ni la Tanganyika. Hili husababisha kauli zenye kuwaudhi wabunge wa Zanzibar.

Mwaka 2016, aliyekuwa Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy, alisema bungeni kuwa wabunge wa Zanzibar wasiwe wanahudhuria Bunge kipindi cha kujadili hoja ambazo si za Muungano. Alijielekeza zaidi kwenye bajeti za wizara, kwamba wasichangie zisizowahusu.

“Muda wa kujadili wizara ambazo siyo za Muungano mwende nje, mtupishe tubaki wenyewe. Tukimaliza tutawaita. Mnajadili Wizara ya Kilimo inawahusu? Wizara ya Maji inawahusu?” alisema Kessy, akishangiliwa na wabunge wengi wa CCM upande wa Tanzania Bara.

Mbunge aliyekuwa anawakilisha Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM), alimworodhesha Kessy katika kero za Muungano. Aliyekuwa Mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya, alisema kuwa kuna kauli zilizotolewa bungeni, zinafanya wabunge wa Zanzibar wajione ni daraja la pili, wakati wabunge wote ni sawa.

Kulikuwa na hoja ya sukari ya Zanzibar kuruhusiwa kuuzwa Tanzania Bara. Serikali ilisema sukari ya Zanzibar haitoshelezi mahitaji ya Wazanzibari, kwa hiyo haiwezekani kuuzwa Bara. Baadhi ya wabunge wa Zanzibar walisema takwimu za uzalishaji sukari visiwani humo zinakosewa, kwamba kiasi kinachozalishwa ni kikubwa kuliko mahitaji. Kessy katika hoja yake kuhusu sakata la sukari ya Zanzibar alisema kwamba sukari inayozalishwa Zanzibar ni kidogo na haiwatoshi Wazanzibari. Alisema: “Sukari mnalima tani 8,000 kwa mwaka, matumizi yenu ni tani 17,000. Au hamnywi chai? Kama hamna pesa ya kunywa chai semeni tuwasaidieni.”

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, badala ya kumjibu Kessy kwa hoja yake, wengine walifikia hatua ya kuishambulia Tanzania Bara. Yupo mjumbe alisema, na yupo kwenye kumbukumbu, kwamba Watanzania Bara ndio wana njaa, kwani wengi ni maskini.

Mwaka 2016, aliyekuwa Mbunge wa Temeke (CCM), Abdallah Mtolea, alisema Tanzania Bara ndiyo inayopaswa kuumizwa na Muungano kwa sababu inaibeba Zanzibar. Akasema anayebebwa hawezi kuchoka. Zipo kauli nyingi hutolewa kwa namna ya “sisi na wao” ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi. Ni hatari sana.

Aprili 2016, January Makamba, alipokuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, alipata kuonya kauli zenye kuukosea heshima Muungano. Alimtaja Kessy kwa jina, kwamba japo ni Mbunge wa CCM lakini kauli zake ni zenye kukosa utambuzi kuwa Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Pamoja na onyo hilo la January, kauli za kibaguzi zimekuwa majaribu makubwa ya Muungano, tena ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi. Yupo mbunge amewahi kushutumu: “Kazi yenu kupitisha magendo mnaleta huku kwetu.” Kauli ya hivyo ni kutoa hukumu kwamba Wazanzibari Tanzania Bara siyo kwao na wanaitumia kujinufaisha kwa biashara ya magendo. Je, Wazanzibari wote wanafanya magendo?

Nimepata kushuhudia mijadala ya Baraza la Wawakilishi, wajumbe wakijadili Muungano kwa chuki kubwa, utadhani ni kitu kisicho na manufaa kwao wala hakibebi historia yoyote. Pamoja na yote, Muungano umeendelea kudumu. Miaka 61 ni kielelezo cha ushindi dhidi ya majaribu mengi.