Prime
Wazee Zanzibar wasimulia hali halisi ya Muungano

Unguja. Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wazee wa kisiwani Unguja wanasema matunda ya muungano huo ni makubwa na yenye manufaa kwa wananchi, hivyo wanapaswa kuulinda kwa juhudi na nguvu zote.
Tanzania ilizaliwa Aprili 26, 1964, baada ya viongozi wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar, kuchanganya udongo wa pande zote mbili kama ishara ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ingawa kuna baadhi ya changamoto ndogo zinazojitokeza na kusababisha mashaka kwa baadhi ya watu, wazee hao wanasema ni muhimu masuala hayo kushughulikiwa kwa utaratibu maalumu ili kuhakikisha kuwa kila upande unanufaika na faida za Muungano.
Mwalimu Nyerere, aliyeiongoza Tanganyika kupata Uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1961, aliweka msingi wa Muungano huo pamoja na Sheikh Karume, aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Zanzibar, inayoundwa na visiwa vya Unguja na Pemba, iliungana na Tanganyika miezi mitatu baada ya mapinduzi hayo, na hivyo kuunda taifa moja lenye mshikamano.
Sauti ya wazee
Katika maadhimisho haya ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wazee mbalimbali wanasisitiza kuwa Muungano huu ni hazina ya kihistoria na kiutamaduni, hivyo unapaswa kutunzwa na kuenziwa kwa mujibu wa maono ya waasisi wake, licha ya wao kutokuwa hai.
Mzee Abubakar Haji Bobea, aliyewahi kuwa mwandishi wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, anasema kwa sasa masuala ya uendeshaji wa Serikali zote mbili yanaendelea kwa mafanikio na kwamba viongozi waliopo wanaonyesha dhamira ya dhati katika kushughulikia mambo hayo kwa upana na umakini.
“Kuna umakini mkubwa katika kusimamia Muungano. Hakuna kiongozi mwenye akili timamu atakayekubali Muungano huu uvunjike. Tumetoka mbali na tumeona matunda yake. Ni lazima tuendelee nao hadi mwisho,” anasema Bobea.
Licha ya mafanikio yaliyopo, mzee huyo aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, anasema bado zipo changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, hususan katika nyanja za kibiashara kati ya pande mbili za Muungano.
Anasema Zanzibar ni nchi ndogo na shughuli nyingi za kiuchumi zinategemea soko la Tanzania Bara, lakini bado yapo matatizo ya kiutawala na kisheria yanayokwamisha uingizaji wa bidhaa kutoka upande mmoja kwenda mwingine, jambo linalowaumiza wananchi wa kipato cha chini.
“Asili ya Wazanzibari ni watu wa upendo. Mfano, mtu anaposafiri kutoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam akiwa na zawadi au hata televisheni, bado analazimika kulipia ushuru. Hili linazua changamoto kwa wananchi wa kawaida,” anasema.
Anaongeza kuwa kuna baadhi ya watu wanaosafiri kutoka Bara kwenda Zanzibar na mizigo midogo, kama korosho, lakini hulazimika kulipa ushuru bila kupata faida yoyote, jambo linaloweka doa katika utekelezaji wa Muungano.
Hivyo, anasisitiza hayo ni masuala yanayopaswa kuangaliwa kwa undani, kwa sababu Muungano unapaswa kuwa wa upendo na mshikamano wa kweli.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi), Hamza Hassan Juma, anasema Muungano umeleta mafanikio makubwa kwa Zanzibar, kwa kuwa mambo mengi muhimu yamepatikana.
“Wanaosema Muungano hauna faida nawashangaa. Kuna mambo mengi ya pamoja yanayotekelezwa kupitia Muungano huu. Serikali itaendelea kuudumisha na kushughulikia changamoto zote zinazojitokeza ili kufanikisha malengo ya waasisi wake,” anasema.
Naye Mzee Omar Mohamed Said anasema wananchi wanapaswa kutambua kuwa Muungano huu si tu wa kiserikali, bali pia kuna mwingiliano mkubwa wa kijamii na kiuchumi.
“Tusisingizie unafiki. Ukifuatilia kwa makini, Muungano una umuhimu mkubwa, isipokuwa kwa wale wanaobeba ajenda binafsi mioyoni mwao ndio wanaweza kuubeza,” anasema.
Mzee Said anatoa wito kwa viongozi wakuu wa pande zote mbili kukaa pamoja na kutoa mwongozo juu ya maeneo yenye changamoto ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Anasisitiza hakuna mfumo mkamilifu kwa asilimia 100, lakini hatua kubwa zimepigwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mwingiliano na fursa za biashara zisizo na masharti magumu.
“Wale wanaotaka kuvunja Muungano huenda wana ajenda zao binafsi, si kwa maslahi ya Taifa. Ni muhimu kuendelea kutoa elimu kuhusu asili na umuhimu wa Muungano kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Muungano ni maisha, hakuna kitu chenye thamani kama hicho,” anasisitiza mzee huyo.
Mzee Haji Shaibu Hamad anaongeza kuwa ni muhimu kuendeleza amani na upendo uliopo, sambamba na kuimarisha Muungano kwa kushughulikia kero zinazojitokeza.
“Muungano una manufaa makubwa kwa pande zote mbili. Ni vyema pia kuangalia aina ya Muungano unaokubalika kwa wote, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kusonga mbele peke yake duniani. Muungano unapaswa kuwa wa maridhiano na wa kutoa furaha kwa pande zote mbili,” anasema.
Anasema Muungano huu ni fursa kubwa kwa Watanzania wote, lakini pia kuna haja ya kutoa fursa zaidi za maendeleo kwa Zanzibar na kuhakikisha usawa unazingatiwa katika kila hatua.
“Kinachotekelezwa Bara kinapaswa pia kufanyika Zanzibar. Hii inaonyesha mwelekeo mmoja wa kitaifa. Hata usalama unaweza kuwa hatarini iwapo Muungano utavunjika, kwani Zanzibar ni kisiwa na hivyo inaweza kuingiliwa kwa urahisi,” anasema.
Kwa upande wake, Mzee Muhidini Muhidin, mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), anasema kuwa Muungano umeleta mabadiliko makubwa hata kwa watendaji wa Serikali kutoka pande zote mbili, kupitia kubadilishana uzoefu.