Prime
Saa 10 za hekaheka Kisutu Chadema na Polisi

Dar es Salaam. Ni zaidi ya saa 10 za hekaheka Kisutu, ndivyo unavyoweza kusimulia kilichotokea katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mvutano baina wa viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam umesababisha taharuki maeneo mbalimbali, hususan katikati ya jiji.

Viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema walijitokeza mahakamani hapo kufuatilia kesi za mwenyekiti wao, Tundu Lissu za uhaini na ile ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
Askari polisi kuanzia jana asubuhi hadi jioni walitanda ndani na nje ya Mahakama hiyo kuzuia wasiohusika kuingia mahakamani; hata waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia kuifuatilia.
Katika eneo la Mahakama, kwenda mataa ya Ohio hadi Posta mpya karibu na Hoteli ya Holiday Inn na kurudi eneo la Maktaba, polisi hawakuruhusu mkusanyiko au mtu yeyote bila maelezo ya kueleweka.

Wakiwa na mbwa zaidi ya 10, farasi wanne na polisi wengine wakiwa na bunduki na virungu walitanda maeneo hayo kuzuia mikusanyiko na kukamata baadhi ya watu ambao walijitokeza kwenye eneo hilo.
Mwananchi, iliyokuwa eneo la tukio muda wote ilishuhudia hekaheka hizo kwa zaidi ya saa 10 kuanzia saa moja asubuhi, baadhi ya raia wakikamatwa na kupakizwa kwenye difenda ya polisi iliyokuwa na kazi moja tu ya kuondoka na raia waliokamatwa kwa kushindwa kutii amri.
Saa 2:31 asubuhi, Mwananchi ilimshuhudia mtu mmoja akibishana na polisi huku akipiga kelele akidai yuko tayari wamuue, lakini anachotaka ni kujua hatima ya Lissu.
Kijana huyo alitishiwa mbwa, kabla ya kukamatwa na kupewa kipigo kisha kusukumizwa kwenye difenda na polisi kuondoka naye, sambamba na baadhi ya raia waliokamatwa wengine wakiwa wanawake.
Waandishi wa habari pia walitakiwa kusimama umbali wa takribani mita 100 kutoka lilipo geti la Mahakama, na kutii agizo hilo huku trafiki wa usalama barabarani wakiwa makini kuhakikisha eneo hilo halina foleni.

Hadi kufika saa nne asubuhi, polisi walifanikiwa kudhibiti mikusanyiko, wakitumia mbwa wawili kuwatawanya raia, huku mbwa wengine takribani wanane wakiwa kwenye gari mbili tofauti, moja ikiwa upande wa Barabara ya Bibi Titi na gari jingine lenye mbwa likiwa nje ya ukuta wa Mahakama hiyo.
Askari wengine wakiwa na farasi wanne walikuwa wakizunguka muda wote eneo la nje ya Mahakama na maeneo jirani kuimarisha ulinzi, huku wengine wengi wakiwa kwenye magari tofauti ya polisi wakiwa na virungu na wengine bunduki, mara kadhaa wakipokezana kushuka na kukamata raia waliohisi wako pale kufuatilia kesi ya Lissu.

Hali hiyo ilisababisha taharuki kwa wapita njia wengine, hususan watembea kwa miguu ambao baadhi yao hawakuwa wakifahamu kinachoendelea.
Mikusanyiko isiyo rasmi ilitawanywa, walioonekana kukaidi walikutana na vipigo.
Tangu jana asubuhi hadi jioni, Mwananchi ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuzungumzia hali ya ulinzi bila mafanikio, kwa kuwa ofisini kwake hakuwapo na wala simu yake ya mkononi alipopigiwa haikupokewa.
Chadema wanena
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu kama Boni Yai amesema baadhi yao wameumizwa na wamepelekwa hospitali.

Boni Yai akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema amedai kuwa, baadhi ya waliokamatwa walikutana na kipigo na kwenda kutelekezwa maeneo mbalimbali, ikiwamo Ununio, Mabwepande, Temeke na Bagamoyo.
Amesema waliojeruhiwa wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na chama hicho kitagharimia matibabu yao.
“Wale wote waliojeruhiwa kwa kwenda Kisutu kufuatilia kesi ya mwenyekiti wetu Lissu wote Chadema itagharimia matibabu yao. Kwa taarifa wako kama wanane na wengine hatujui walipo,” amedai Boni Yai, huku akilaani vitendo hivyo.
Amesema wana haki ya kwenda kufuatilia kesi ya kiongozi wao, kwa kuwa hakuna sehemu ambayo wamevunja sheria na kuliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha wanatenda haki.
Mwananchi ilifika idara ya wagonjwa wa dharura Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala na kukuta baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiwa wamesindikiza wenzao wanaodaiwa kujeruhiwa baada ya kushambuliwa na polisi.
Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Ntele Benjamin amesema baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema walikamatwa na polisi walipokuwa wanakwenda mahakamani.
“Hawa walikamatwa kwa nyakati tofauti, wapo waliopelekwa Ununio, wengine wakapelekwa Mabwepande, huko walipigwa na kuumizwa, tulipata taarifa za kushambuliwa kwao na sasa wako hapa kwa ajili ya matibabu,” amesema.
Akisimulia ilivyokuwa mahakamani Kisutu, mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Manyoni, Dan Butale amesema walifika kwenye viunga vya Mahakama asubuhi na kuzuiwa kuingia ndani kwa kile walichoambiwa hakuna kesi.
“Tulikuta askari wengi wakatuambia hapa hakuna kesi, wakati tukiendelea kuzungumza nao nikasogea pembeni kupokea simu ili niwaelekeze wengine mahali nilipo, ile nageuka nakuta wenzangu wamezingirwa na kubebwa wakaingizwa kwenye gari la polisi.
Mwananchi ilifika ofisini kwa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Zavery Benela ambaye amekataa kuzungumzia suala hilo akieleza hana taarifa rasmi.

“Hao wamekuja kama wagonjwa wengine, hawana PF3 ya polisi au nyaraka yoyote, hivyo siwezi kuzungumza chochote watahudumiwa,” amesema.
Mgombea urais ACT azuiwa
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alijikuta akikwama kuingia mahakamani kufuatilia kesi hiyo ya Lissu, iliyokuwa ikiendeshwa kwa njia ya mtandao, kwa kuwa polisi hawakumruhusu kuingia.
Akiwa nje ya geti la Mahakama hiyo, upande wa uelekeo wa mataa ya Ohio, Semu alishuka kwenye gari lake kwa lengo la kuzungumza na wanahabari.
Askari watatu wa kike wa kutuliza ghasia walimzuia wakitaka aondoke eneo hilo. Kiongozi huyo ambaye amechukua fomu kuwania urais kupitia ACT Wazalendo, alikataa na kudai eneo hilo si la Mahakama, hivyo amesimama kihalali na asilazimishwe kuondoka. Wakati mvutano huo ukiendelea, askari wengine takribani saba, wanaume wakiwa kwenye gari ya polisi walisogea kwenye kusanyiko hilo bila kuzungumza chochote, huku wawili kati yao wakishuka na kutawanya kusanyiko hilo kwa kuwatishia mbwa, Semu na waandishi wa habari.
Wakati wakifanya hivyo, mmoja wa viongozi wa ACT-Wazalendo aliwafokea askari akiwatuhumu kuwatishia mbwa na kumfungulia kiongozi huyo mlango wa gari ili apande waondoke.

Waandishi pia walikimbia kukwepa kudhuriwa na mbwa hao wa Polisi kabla ya Semu kuondoka eneo hilo saa 5:25 asubuhi. Baada ya Semu kuondoka, askari wenye mbwa nao walisogea upande mwingine kuendelea na majukumu yao, huku waandishi wa habari wakikimbilia kwenye korido za majengo yaliyo jirani na Mahakama hiyo.
Wakati huo mvua ilikuwa imeanza kunyesha katika viunga hivyo vya Mahakama ya Kisutu.
Lissu alivyogoma kesi kusikilizwa mtandaoni
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (57), amepinga kesi zake kuendeshwa kwa njia ya mtandao (video conference), huku akiwa mahabusu, badala yake afikishwe mahakamani.
Lissu, ambaye yuko mahabusu ya Gereza la Ukonga anakabiliwa na kesi mbili za jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu. Kesi hizo ni kuchapisha taarifa za uwongo mitandaoni na nyingine ya uhaini.
Hata hivyo, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo haikuweza kuendelea jana kwa hatua ya usikilizwaji wa awali, baada ya Lissu kukataa kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao.
Jopo la mawakili zaidi ya 20 linalomwakilisha Lissu, likiongozwa na Wakili Mpale Mpoki lilimuunga mkono mteja wao na kuwasilisha hoja za kisheria kupinga kesi kuendeshwa kwa utaratibu huo, huku nalo likitaka afikishwe mahakamani.
Pia, mwanasiasa wa Kenya ambaye kitaaluma ni mwanasheria, Martha Karua alikuwapo mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini haikuweza kuendelea katika hatua hiyo.
Badala yake, Hakimu Mhini aliiahirisha hadi Aprili 28, 2025 kwa ajili ya upande wa Jamhuri kujibu hoja za mawakili wa utetezi kuhusu kesi hiyo kuendeshwa kwa njia ya mtandao.

Hakimu Mhini ameielekeza Jamhuri kuwasilisha hoja zake tarehe hiyo kwa njia ya mtandao.
Pia, Mahakama imeuzuia upande wa utetezi kusambaza nakala ya maelezo ya awali ya kesi hiyo ambayo mshtakiwa anatarajiwa kusomewa. Mahakama hiyo ilitoa amri ya zuio hilo kufuatia maombi yaliyotolewa na upande wa Jamhuri.
Mchuano wa mawakili ulivyokuwa
Baada ya Mahakama na mawakili wa utetezi kuingia katika ukumbi wa mitambo ya kuendesha kesi kwa njia ya mtandao, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema amesema upande wa mashtaka ulikuwa tayari kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Lakini, mshtakiwa hakufika katika chumba cha mitambo ya kusikilizia kesi kwa njia ya mtandao katika Gereza la Ukonga.
Wakili Mrema amehoji mbona mshtakiwa haonekani mtandaoni, ndipo Hakimu Mhini akamtaka Ofisa wa Jeshi la Magereza mwenye dhamana ya kuwasimamia mahabusu ambao, kesi zao zinasikilizwa kwa njia ya mtandao ajibu swali hilo.
Akijibu swali hilo, ofisa huyo ameieleza Mahakama kuwa, Lissu amegoma kesi yake kusikilizwa kwa njia hiyo, anataka afikishwe mahakamani ili isikilizwe kwa utaratibu wa kawaida. Baada ya maelezo hayo, wakili Mrema ameomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kuendelea na hatua hiyo.
Hakimu Mhini aliridhia kuendelea na kesi hata bila Lissu kuonekana kwenye picha (video) mtandaoni.
Hata hivyo, mawakili wa Lissu nao wameunga mkono msimamo wa mteja wao, huku wakiwasilisha hoja kupinga kusomewa maelezo ya awali kwa njia hiyo, wakidai ni kinyume na sheria.
Wamedai kuwa, sheria inaelekeza kuwa katika hatua hiyo ya usikilizwaji wa awali, mshtakiwa anapaswa kufikishwa mahakamani.
“Hata kama mshtakiwa angekuwepo mtandaoni, leo tusingeweza kuendelea kwa sababu ingekuwa ni kinyume na sheria, kwani sheria inataka maelezo ya awali yasomwe mshtakiwa mwenyewe akiwepo,” amedai wakili Mpoki.
Amefafanua kuwa, baada ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali, anapaswa kusaini nakala ya hoja zinazobishaniwa na zisizobishaniwa.
Baada ya hoja za mawakili wa utetezi, uongozi wa jopo la waendesha mashtaka kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga uliomba upewe muda wa kujibu hoja za upande wa utetezi.
Pia, wakili Katuga ameiomba Mahakama itoea amri kuwaelekeza upande wa utetezi wasisambaze mitandaoni nakala ya maelezo ya awali wanayotarajia kumsomea mshtakiwa, waliyowapatia kwa sababu bado hayajasomwa mahakamani.

Hakimu Mhini amekubaliana na hoja, akielekeza upande wa mashtaka uwasilishe majibu ya utetezi Aprili 28, 2025 kupitia kiungo (link) cha mfumo wa Mahakama wa uwasilishaji nyaraka za mashauri (e-filing) watakayotumiwa.
“Naelekeza upande wa utetezi usisambaze mitandaoni nakala ya maelezo ya awali, kwa sababu bado hayajasomwa mahakamani,” alisema Hakimu Mhini na kuelekeza kuwa, Mahakama itapanga tarehe ya kutoa uamuzi wake, Aprili 28, 2025.
Katika kesi ya uhaini, Mahakama hiyo iliamuru itaendeshwa kwa njia ya mtandao. Uamuzi huo ulitolewa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kiswaga ametoa uamuzi huo jana jioni baada ya kutupilia mbali ombi lililowekwa na mawakili wa upande wa utetezi, ambalo waliomba kesi hiyo iendeshwe kwa njia ya kawaida na sio kwa njia ya video. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 6, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Mashitaka ya Lissu
Katika kesi ya pili, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uwongo, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.
Mashtaka hayo yote matatu ni ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa Youtube kwa nia ya kulaghai umma.

Katika shitaka la kwanza, Lissu amenukuliwa maneno aliyoyachapisha kuwa: “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais.”
Shtaka la pili anadaiwa kuwa siku hiyo alichapisha taarifa za uwongo na za kupotosha umma kuwa: “Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi.”
Katika shtaka la tatu anadaiwa kuwa siku hiyohiyo alichapisha taarifa kuwa: “Majaji ni ma-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.”
Katika kesi hiyo, Lissu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutekeleza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho cha Taifa (Nida) na barua ya Serikali za mtaa aliyesaini bondi ya Sh5 milioni.
Hata hivyo, alilazimika kupelekwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na shtaka la uhaini katika kesi nyingine lisilo na dhamana.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Baraka Loshilaa na Elizabeth Edward