Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mama asimulia mwanaye aliyeuawa kwa kipigo…

Muktasari:

  • Enock ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto sita,alisoma hadi kidato cha nne katika shule ya Sekondari Runzewe na hadi anafikwa na mauti alikuwa akinakili nyimbo kwenye CD kama sehemu ya kujikimu na maisha.

Bukombe. “Mama nimepigwa sana… mama nisaidie, sijaleta vitu, nimekuja mama yangu unisaidie, nakufa nisaidie.”

Hayo yalikuwa maneno ya mwisho ya Enock Mhangwa (25), mkazi wa Kijiji cha Uyovu wilayani Bukombe mkoani Geita, akimuomba msaada mama yake mzazi alipofikishwa nyumbani kwao akiwa taabani.

Enock ambaye picha yake mjongeo ilienea kwenye mitandao ya kijamii jana, alionekana akipigwa na watu wanaodaiwa kuwa viongozi wa kijiji wakisaidiana na askari mgambo kwa tuhuma za kuiba kompyuta mpakato.

“Mwanangu Enock kabla hajafa alikuwa na maumivu makali sana, amepigwa sehemu zote za mwili,” anasimulia Kulwa Baseke, mama mzazi wa Enock.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime leo Ijumaa ilieleza kwamba, mpaka jana usiku, watu wawili walikuwa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Ferdinand Antony, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika na Hussen Ally.

Misime amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine, akiwamo Mtendaji wa Kijiji cha Uyovu na askari mgambo wawili ambao walitoweka baada ya tukio.

Mwandishi wa Mwananchi alifika nyumbani kwa Kulwa Beseke ambaye ni mama wa marehemu katika Kijiji cha Uyovu, leo Ijumaa Julai 4, 2025, anasema alikuwa na watoto sita lakini sasa amebaki na watano kwamba hawezi kusahau jinsi alivyomwona Enock akilia kwa maumivu akiwa hana hata nguvu za kukaa mwenyewe kutokana na kipgo.

Akisimulia jinsi alivyozipata taarifa za tukio,  Baseke amesema siku ya tukio, Juni 23, 2025, mchana alipokea simu kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji cha Uyovu akimwomba afike ofisini kwake.

Amesema alimuuliza mtendaji huyo kuna tatizo gani, ndipo akafahamishwa kuwa mwanawe Enock anatumiwa kwa wizi wa kompyuta.

“Nikamwambia niko mjini na nina mtoto mgonjwa, siwezi kufika haraka. Nilimweleza kuwa kwa kuwa Enock yupo sehemu salama ningeweza kwenda baadaye,” anasimulia.

Anasema baada ya kumpeleka mtoto mgonjwa nyumbani na kuchukua dawa, aliwaambia watoto wake wengine wamuandalie chakula ili aweze kula. Hata hivyo, kabla hajaanza kula, alipigiwa tena simu akielekezwa kwenda kumuaga mwanawe.

Anadai alipouliza kwa nini aitwe kumuaga mtoto, aliambiwa yupo kwenye pori jirani na shule.

Kulwa Baseke mama wa Enock Mhangwa akionyesha kaburi alilozikwa mwanae baada ya kushambuliwa kwa kipigo na viongozi wa kijiji wakimtuhumu kwa wizi.

“Wakati naongea na mtendaji kwenye simu nilisikia sauti ya mwanangu akilia na kunita mama huku wakimlazimisha aseme viko wapi. Nilimsikia mtu akimpiga kwa kitu. Nilishindwa kula, nikaamka kujiandaa, lakini hata kabla sijatoka nje walikuwa wameshamleta nyumbani,” anasimulia Kulwa.

Anasema Enock alipofikishwa nyumbani hakuwa na nguvu hata za kusimama, alianguka na walimvuta jirani na mama yake huku wakimlazimisha aseme alikoficha vitu alivyodaiwa kuiba.

“Nilimuuliza mwanangu kama kweli kaiba na kama kavileta, aniambie viko wapi. Aliniambia mama sijaleta kitu chochote, nimekuja unisaidie, nimepigwa sana,” anasema.

Mama huyo anasema baada ya mtoto kuomba msaada, watu hao walidai kuwa wamelazimika kumleta kwa sababu ameiba na wakamtaka awalipe Sh200,000 ili wamuachie huru, akasema hana fedha hizo.

“Hali ya mwanangu iliendelea kuwa mbaya. Niliwaambia siwezi kuwapa hiyo pesa, twende polisi wakapate PF3 kwa kuwa alikuwa hata akikalishwa anaanguka,” anasema.

Anasema walipofika kituo cha polisi, askari waliwataka wampeleke hospitali.

Anasema walimpeleka Kituo cha Afya Uyovu ambako alilazwa, lakini Juni 24, 2025 alifariki dunia na kuzikwa Juni 26 nyumbani kwao Uyovu.

Kulwa amesema ripoti ya daktari ilieleza kuwa sababu ya kifo chake ni kuvilia damu ndani kwa ndani kulikosababishwa na majeraha aliyoyapata.

“Naomba serikali inisaidie haki ipatikane. Viongozi wa kijiji ndio tunawategemea kama walinzi wetu,” anasema huku machozi yakimtoka.

“Enock alikuwa mtoto niliyemtegemea. Hakuwa ameoa, alikuwa bado kijana mdogo. Sina neno na mtu, lakini naomba haki itendeke,” anaongeza kwa uchungu.

Enock alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto sita katika familia hiyo. Alisoma hadi kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Runzewe na alikuwa akifanya kazi ya kunakili nyimbo kwenye CD. Kwa mujibu wa mama yake, kabla ya tukio hilo hakuwahi kutuhumiwa kwa wizi wala kushikiliwa kwa kosa lolote la uhalifu.


Ushuhuda wa Jirani

Rosmary Misalaba, jirani wa familia hiyo, amethibitisha kushuhudia Enock akiletwa akiwa hoi mbele ya nyumba yao.

“Alipofika getini alianguka. Wakamwambia amka uingie ndani. Aliingia kwa shida sana. Mama yake aliwauliza kulikoni, wakasema ameiba kompyuta na walitaka aseme mbele ya mama yake,” amedai Rosmary.

Amedai kuwa viongozi hao walidai wapewe Sh200,000 kama fidia ya kifaa kilichoibiwa, lakini mama yake alikataa akisema hana fedha hiyo na kuwataka waende polisi.

“Walimtoa kijana na kuondoka naye, lakini Enock alikuwa hata hawezi kutembea vizuri, akijiburuza tu,” amesimulia jirani huyo.

Rosmary amesema siku iliyofuata alisikia kilio kutoka kwa mama yake na alipohoji alipewa taarifa kwamba Enock amefariki dunia.

“Enock alikuwa kijana mpole, hakuwa mtu wa fujo wala wizi. Kifo chake kimetusikitisha sana,” amesema.


Kauli ya Mwenyekiti wa Kijiji

Mwenyekiti wa Kijiji cha Uyovu, Sostenes Maendeleo  amesema alishirikiana na wananchi kushughulikia mazishi ya Enock nyumbani kwao huku serikali ikiendelea na taratibu za uchunguzi.

Amewaasa wananchi waepuke tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yakekama kuna mtu wanamshuku kwa uhalifu watoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.

“Hili suala kwa sasa liko mikononi mwa polisi kwa uchunguzi. Naomba wananchi wangu wasijichukulie sheria mkononi, zipo mamlaka zinazoweza kufanya kazi hiyo,” amesema Maendeleo.