Lissu kizimbani tena leo, Polisi, Chadema wakitunishiana msuli

Muktasari:
- Tundu Lissu anakabiliwa na kesi mbili, moja ya uhaini na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni. Leo Alhamisi anatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa ajili ya kesi hizo mbili lakini katika hatua mbili tofauti.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu (57), anayekabiliwa na kesi za jinai, leo Alhamisi, Aprili 24, 2025 anatarajiwa kupandishwa tena kizimbani.
Lissu anakabiliwa na kesi mbili tofauti za jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mkoa wa Dar es Salaam, moja akikabiliwa na shtaka moja la uhaini na nyingine akikabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uwongo mitandaoni.
Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka hayo, Aprili 10, 2025. Kesi hizo zote zimepangwa kuendelea leo Alhamisi katika hatua tofautitofauti.
Wakati kesi ya uhaini imepangwa kwa ajili ya kutajwa kuangalia maendeleo ya upelelezi, kama umeshakamilika ili kuendelea na hatua zinazofuata, kesi ya mashtaka ya kuchapisha tarifa za uongo mitandaoni imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi.
Lissu anatarajiwa kupandishwa kizimbani mahakamani hapo leo kwa ajili ya kesi hizo, huku kukiwa na msigano wa misimamo baina ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na wanachama pamoja na wafuasi wa chama hicho kuhusiana na uhudhuriaji wa kesi hizo.

Viongozi wa Chadema hususan makamu mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche kwa nyakati na maeneo tofauti amekuwa akitoa wito na kuwahamasisha wanachama na wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi mahakamani leo kufuatilia kesi hizo.
Mbali na Heche, viongozi na wanachama wengine wakiwemo wa mikoani wamekuwa wakihamasishana kusafiri kwenda jijini kufuatilia kesi hizo.
Lakini kufuatia wito huo, Jeshi la Polisi Dar es Salaam, kupitia Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro, limepiga marufuku mkusanyiko mahakamani hapo kwa madai kuna mipango ya kufanya vurugu.
Kamanda Muliro alinukuliwa na vyombo vya habari Aprili 17, 2025 akionya watakaokaidi na kuitikia wito huo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Onyo hilo la Kamanda Muliro limepingwa na viongozi wa Chadema na wafuasi wao kwa kile walichodai Katiba na sheria za nchi zinawaruhusu na kulitaka Jeshi la Polisi kuwaacha ili kwenda kusikiliza kesi ya kiongozi wao.
Mashtaka yanayomkabili Lissu
Katika kesi ya kwanza Lissu alisomewa shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawishi, Franco Kiswaga, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kuwa:
"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...,kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...,kwa hiyo tunaenda kikinukisha...,sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."
Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo na inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Franco Kiswaga, kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwemo kukamilika upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza.
Kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana, Lissu anaendelea kubaki mahabusu kwa muda usiojulikana wakati kesi hiyo ikiendelea au itakapoamuriwa vinginevyo.
Katika kesi ya pili, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.
Mashtaka hayo yote matatu ni ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kuyatenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa nia ya kulaghai umma.
Katika shtaka la kwanza yamenukuliwa maneno aliyoyachapisha Lissu kuwa:
"Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa' kwa maelekezo ya Rais," wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na yanapotosha umma.
Shtaka la pili anadaiwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na kupotosha umma kuwa:
"Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi."
Katika shtaka la tatu anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa kuwa:
"Majaji ni MA-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.
Katika mashtaka hayo alipoulizwa na hakimu iwapo ni kweli au si kweli, Lissu hakukana bali alisema maneno hayo si kosa hivyo sio kweli (kwamba ametenda makosa hayo).
Upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika, hivyo leo Alhamisi anatarajiwa kusomewa maelezo ya awali ya kesi kabla ya kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa ushahidi.
Katika kesi hiyo, Lissu aliachiwa kwa dhamana baada ya kutekeleza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja mwenye kitambulisho cha Taifa ( Nida) na barua ya serikali za mitaa aliyesaini bondi ya Sh5 milioni.
Hata hivyo, alilazimika kupelekwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na shtaka la uhaini katika kesi nyingine lisilo na dhamana.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi