Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya uhaini ya Lissu ya kwanza tangu kurejea mfumo wa vyama vingi Tanzania

Dar es Salaam. Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chadema ameingia katika historia baada ya kushtakiwa kwa uhaini, ikiwa ni kesi ya kwanza dhidi ya kiongozi wa kisiasa kwa Tanzania Bara tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.

Kesi nyingine kubwa dhidi ya wanasiasa wa upinzani zilikuwa za ugaidi, moja ikimkabili aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mwaka 2024 na nyingine dhidi ya aliyekuwa mkurugenzi wa ulinzi wa chama hicho, Wilfred Lwakatare mwaka 2013.

Hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar, viongozi 18 wa Chama cha Wananchi (CUF) walishtakiwa kwa uhaini mwishoni mwa mwaka 1999 na mwanzoni mwa 2000, kabla ya mashtaka yao kufutwa na Mahakama ya Rufani kwa hoja kwamba Zanzibar si dola kamili, hivyo isingewezekana kuwepo uhaini.

Viongozi hao, Khamis Ali Machano na wengine 17, walikuwa wakituhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali ya Zanzibar.

Kabla ya kurejea mfumo wa vyama vingi, Tanzania imewahi kushuhudia kesi kadhaa za uhaini zinazohusisha wanasiasa, wanajeshi na watumishi wa umma.

Juni 8, 1970, Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu Philip Telford Georges ilisikiliza kesi ya uhaini dhidi ya Bibi Titi Mohamed na Gray Likungu Mattaka, John Dunstan Lifa Chipaka, Michael Marshall Mowbray Kamaliza, Eliyah Dunstan Lifa Chipaka, William Makori Chacha na Alfred Philip Milinga.

Walikuwa wakituhumiwa kupanga njama za kuiangusha Serikali na kumuua Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere. Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, alihusishwa, lakini alikuwa ameikimbia nchi.

Kesi nyingine ya uhaini ilifunguliwa mwaka 1983 dhidi ya watu 19 waliofikishwa mahakamani kujibu shtaka la uhaini, wakituhumiwa kutaka kumpindua Mwalimu Nyerere wengi wao walipatikana na hatia.

Washtakiwa hao walikuwa Kapteni Christopher Kadego, Luteni Eugene Maganga, Suleiman Kamando, Kapteni Vitalis Mapunda,  Kapteni Roderic Roberts,  Paschal Chaika na  Luteni John Chitunguli.

Wengine ni Luteni Mark Mkude, Kapteni Oswald Mbogoro, Kapteni Zacharia Hans Pope, Badru Kajaje, Christopher Ngaiza na Luteni Gervas Rweyongeza.

Pia walikuwemo Luteni Otmar Haule, George Banyikwa, Zera Banyikwa, Luteni Nimrod Faraji, Livinus Rugaimukamu na Hatty McGhee.

Pia, Lissu ambaye amefunguliwa mashtaka ya uhaini jana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, anaingia kwenye orodha ya wanasiasa wengine wa Afrika waliowahi kufunguliwa kesi za uhaini.

Miongoni mwao ni Hakainde Hichilema wa Zambia (kabla hajawa Rais), Kizza Besigye na Bobi Wine wa Uganda, Rais wa zamani wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma.

Mashtaka ya uhaini dhidi ya wanasiasa barani Afrika yameendelea kuwa kielelezo cha changamoto zinazowakumba viongozi mbalimbali hasa wa vyama vya upinzani kutokana na kushiriki katika mapambano ya kisiasa dhidi ya watawala wanaojipambanua kwamba wanalinda usalama wa mataifa husika.

Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema, mwanasiasa na kiongozi wa Chama cha United Party for National Development (UPND), aliwahi kushtakiwa kwa kesi ya uhaini mwaka 2017. Hichilema alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na jaribio la kupindua Serikali ya Rais Edgar Lungu na alikamatwa kwa kushiriki katika maandamano yaliyoashiria kusababisha vurugu. Hichilema alifungwa kwa miezi kadha na katika uchaguzi wa 2021, alishinda na kuwa Rais wa Zambia.

Dk Kizza Besigye wa Uganda amekumbwa na mashtaka ya uhaini mara kadhaa kutokana na mapambano yake dhidi ya Rais Yoweri Museveni. Mashtaka dhidi ya Besigye yalianza baada ya kushiriki katika maandamano ya kupinga uchaguzi wa Rais Museveni na kudai kuwa uchaguzi ulifanyika kwa udanganyifu.

Besigye amekuwa akikamatwa na kuzuiliwa mara kadhaa na sasa anashtakiwa katika makosa kama hayo kwenye Mahakama ya Kijeshi nchini humo.

Pia, Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ni mwanamuziki na kiongozi wa upinzani nchini Uganda ambaye amekumbwa na mashtaka ya uhaini. Alikamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2021. Bobi Wine alishutumiwa kwa kushiriki katika maandamano ambayo Serikali ilisema yalikuwa ni tishio kwa usalama wa taifa.

Mwanasiasa mwingine aliyekumbana na kesi ya uhaini ni Rais wa zamani wa Sierra Leone, Ernest Bai Koroma, ambaye alikumbwa na mashtaka ya uhaini mwaka 2024 baada ya kuhusishwa na jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali ya Rais Julius Maada Bio.

Mashtaka dhidi ya Koroma yalitokana na madai kwamba walinzi wake walihusika katika kuandaa njama za mapinduzi.

Mwanasheria maarufu wa Kenya, Miguna Miguna, alikamatwa na kushitakiwa kwa uhaini baada ya kumtangaza Raila Odinga kuwa Rais wa wananchi mwaka 2017, jambo lililokuwa kinyume na matokeo rasmi ya uchaguzi.

Miguna alishtakiwa kwa kuhusika na njama za kuunda Serikali mbadala, jambo lililozua mgawanyiko mkubwa katika siasa za Kenya kabla ya kutimuliwa nchini humo kwenda uhamishoni Canada.