Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malima azionya asasi, mashirika ya kiraia kuelekea uchaguzi mkuu

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Adamu Malima

Muktasari:

  • Ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya taasisi zitakazojihusisha na matamko au vitendo vya kuchochea vurugu.

Morogoro. Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amezitaka taasisi zisizo za kiserikali (NGO) kutoshirikiana na wanaharakati wa kisiasa wenye nia ya kuvuruga amani na utulivu wa mkoa huo.

Akizungumza katika mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humo leo Jumamosi Julai 5, 2025 Malima amesisitiza kuwa mchango wa asasi za kiraia unatambulika, lakini ni muhimu zifanye kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi.

Ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya taasisi zitakazojihusisha na matamko au vitendo vya kuchochea vurugu.

“Nikisikia shirika au asasi yoyote inayosema ‘itakinukisha’ au kuungana na wanaotoa kauli za kuchochea vurugu, hao watakuwa wangu, nitakabiliana nao. Lakini shirika au asasi inayofuata sheria na kulinda amani, hao ndio marafiki zangu na ninawahitaji kuendeleza mkoa huu,” amesema Malima.

Ameongeza kuwa anatoa ushirikiano kamili kwa mashirika yanayopambana na ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na yanayosaidia kulinda maadili ya jamii.

“Nikiona asasi inayochochea vitendo visivyoendana na utamaduni wetu, hiyo hainifai, nitaiondoa kisheria,” ameongeza kwa msisitizo.

Malima amezitaka asasi zenyewe kuwa waangalizi wa mwenendo wa wenzao kwa kukemeana na kuelimishana kabla ya Serikali kuingilia kati.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Morogoro, Otanamusu Nicholaus amesema mashirika hayo kwa kushirikiana na Serikali, yametekeleza miradi yenye thamani ya Sh30 bilioni kuanzia mwaka 2020 hadi 2025.

Miradi hiyo imehusisha sekta za afya, elimu, mazingira, haki za binadamu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Nicholaus amesema miradi hiyo imezingatia sheria na taratibu za nchi na kutekelezwa katika maeneo mbalimbali kwa kushirikiana na halmashauri.

Ametaja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na uboreshaji wa madarasa ya awali, mafunzo kwa walimu, vifaa vya kujifunzia, upandaji miti, uhifadhi wa vyanzo vya maji, uwezeshaji wa wanawake na vijana na uchimbaji wa visima vya maji.

Aidha, amesema zaidi ya mashirika 150 yamewasilisha taarifa za utekelezaji kwa vipindi mbalimbali vya mkataba, huku mkoa huo ukiwa na jumla ya NGO 571 zilizosajiliwa na kutambuliwa na Serikali, kati ya hizo 11 zikiwa ni za kimataifa, 457 kitaifa, 16 kimkoa na 24 za ngazi ya wilaya.

Akizungumza kwa niaba ya mashirika ya kisheria, mwakilishi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Morogoro, Joycerebecca Paul, ametoa wito kwa mashirika ya kiraia kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli ili kuongeza tija katika jamii.

“Tushirikiane kwa pamoja, tukitembea kwa umoja ndipo mafanikio yetu yataonekana na kutambulika. Umoja wetu ndio maendeleo yetu,” amesema Paul.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kushirikiana na mashirika hayo hasa wakati wa utekelezaji wa miradi katika ngazi za vijiji na vitongoji, akieleza kuwa mashirika hayo hayawezi kufanya kazi peke yao bila usaidizi wa viongozi wa maeneo husika.