Prime
'Kama la ugaidi liliwezekana, kwa nini la uhaini lisiwezekane'

Naweza kusema ni kipindi kigumu ambacho Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinapitia kwa sasa.
Ni wazi kuwa chama hiki hivi sasa kinapitia wakati mgumu baada ya Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu kushtakiwa kwa kesi ya uhaini.
Lakini nikilitazama kwa kina sakata hili, naona kuna haja ya kuwasaidia Chadema.
Hata kama chama hicho kimeamua kutoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, milango inapaswa kuwa wazi kwa wanachama wao binafsi wanaotaka kushiriki.
Hii ni kwa sababu, wanachama na wafuasi wa chama hicho bado wanayo haki yao ya msingi ya kidemokrasia, haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kwa kipindi kijacho cha miaka mitano.
Napenda kuwatoa wasiwasi kwamba, zaidi ya kuwa mwandishi na mtangazaji wa kujitegemea, mimi pia ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea.
Hapa hatuzungumzii kesi yoyote iliyoko mahakamani, bali tunajadili masuala ya kisheria na haki za raia.
Nianze kwa kueleza kuhusu makosa mawili makubwa kabisa katika Katiba yetu, kosa la kuua na kosa la uhaini, ambayo yote hupewa adhabu ya kifo, yaani capital punishment.
Kwa Tanzania, adhabu hii hutekelezwa kwa kunyongwa hadi kufa katika Gereza la Isanga, lililopo mjini Dodoma.
Hata hivyo, adhabu ya kunyongwa haitekelezwi hadi Rais asaini hati ya kifo. Baada ya kusainiwa, mfungwa hupimwa na daktari bingwa wa hospitali ya serikali ili kuthibitisha kuwa yuko katika hali nzuri kiafya kabla ya kutekelezwa kwa adhabu hiyo.
Kwa mfano, katika utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambao ulidumu kwa miaka 23, alisaini hati mbili tu za kunyongwa.
Rais Ali Hassan Mwinyi, aliyeongoza kwa miaka 10, alisaini hati kadhaa.
Lakini tangu wakati wa marais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Dk John Magufuli hadi Rais Samia Suluhu Hassan, hakuna hati ya kifo iliyosainiwa.
Hali hii ndiyo inayowasukuma watetezi wa haki za binadamu kuendelea kupendekeza adhabu hii ya kifo ifutwe kabisa.
Uhaini ni nini?
Kosa la uhaini linatajwa katika Sura ya Saba, Kifungu cha 39 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).
Kifungu hicho kinasema mtu yeyote aliye ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano, anapojaribu kumuua Rais, kuanzisha vita dhidi ya nchi, au kushawishi, kuchochea, kushauri, au kusaidia jaribio lolote linalolenga kumwondoa Rais madarakani kwa nguvu, anakuwa ametenda kosa la uhaini.
Ni muhimu kufahamu kuwa sio kila kauli ya kisiasa ni uhaini. Ili kosa la uhaini litimie kisheria, lazima kuwe na viashiria viwili muhimu vya jinai:
Kwanza ni kitendo halisi cha jinai na pili ni nia ya kutenda jinai. Kwa hiyo, mtu akisema kwamba ataifanya nchi isitawalike au uchaguzi usifanyike, hiyo inaweza kuwa ni kauli ya uchochezi (sedition), lakini siyo uhaini, isipokuwa kama kuna mipango ya vitendo vya kweli vya kuiangusha serikali kwa nguvu.
Kumkamata mtu na kumfungulia mashtaka ya uhaini kunaiweka nchi katika hali ya tahadhari na huweza kuathiri taswira yake kimataifa. Ndiyo maana, tunapaswa kuwa waangalifu sana kabla ya kutumia kosa hili zito kwa wanasiasa au wanaharakati, vinginevyo ni kumchafulia Rais wa nchi sifa yake ya kuwa kiongozi mnyenyekevu na mpatanishi aliyeliponya Taifa hili.
Tangu tupate uhuru, Tanzania imewahi kuwa na kesi tano tu za uhaini, naweza kusema ya sita ni hii iliyotokea juzi.
Itakumbukwa Tanzania ilishakuwa na kesi ya uasi ya jeshi la KAR ya Januari 18, 1964, ambayo ilishughulikiwa kijeshi.
Kesi ya pili ni ile ya mwaka 1971 dhidi ya Bibi Titi Mohamed, John Lifa Chipaka, Michael Kamaliza na wenzao na ya tatu ilikuwa dhidi ya Juma Thomas Zangira.
Kesi ya tano ni ile ya mwaka 1982 ya watu 38, wakiongozwa na Pius Lugangira na Hatibu Ghandi na ya sita ni ya Zanzibar dhidi ya viongozi wa CUF, akiwamo Seif Sharif Hamad, baadaye ikatupiliwa mbali kwa msingi kwamba Zanzibar sio nchi, hivyo kosa la uhaini haliwezi kutendeka humo.
Sasa tuna kesi ya sita, iliyotajwa wiki iliyopita. Somo muhimu kuelekea uchaguzi mkuu:
Watanzania, wanasiasa, wanaharakati na viongozi, wawe waangalifu na kauli na matendo yao hasa kipindi hiki.
Wanapaswa kufuata Katiba, sheria, taratibu na kanuni ili kulinda amani na utulivu wa nchi, chokochoko hazistahili.
Ombi kwa Rais Samia
Kama aliweza kulitatua tatizo la ugaidi, ambalo lilikuwa zito zaidi na lilishafikia hatua ya watu kuhukumiwa, basi hili la sasa ni dogo zaidi.
Kwa busara zake, binafsi ninamuomba afanye jambo kwa kuweka mazingira ya kisiasa sawa ili tuondokane na kelele hizi za kila kona.
Hakuna anayelazimisha Chadema kushiriki uchaguzi.
Kama hawataki, basi wachague wao wenyewe kutojihusisha, lakini milango ya kushiriki isiwe imefungwa kwa nguvu za mamlaka. Hii itaondoa kisingizio cha lawama zisizokwisha.
Mungu mbariki Rais Samia katika kutimiza wajibu wake kwa hekima na busara.