Samia: 4R zisiwe kigezo kuvunja sheria

Rais Samia Suluhu Hassan.
Muktasari:
- Maadhimisho ya Muungano kwa mwaka huu yataadhimishwa kwa ngazi ya mikoa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kutekelezwa falsafa ya 4R kunakwenda sambamba na kuzingatiwa kwa Katiba na sheria za nchi, kamwe haiwezi kuwa kisingizio cha kuvunja sheria au kujenga mazingira yanayohatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi.
Amesema hayo leo Ijumaa Aprili 25, 2025 alipohutubia Taifa katika maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.
“Demokrasia yetu imeendelea kukua na kuimarika hususani kupitia falsafa yetu ya 4R, ambayo itaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kukuza ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu,” amesema.
Amesema Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasimamiwa na mihimili mitatu ya Serikali, Bunge na Mahakama. Kwa pamoja kama nchi, imeamua uendeshaji wa shughuli za nchi ushirikishe taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, taasisi za kidini na za kiraia.
“Shughuli zote zinazofanywa na taasisi hizi zinaongozwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar, Sheria na kanuni zinazotungwa na miongozo na makubaliano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” amesema.
“Nyenzo hizi nilizozitaja zimeeleza masharti na mipaka ya kazi kwa taasisi mbalimbali zinazofanya shughuli zake hapa nchini. Ili kuiwezesha Serikali kuendelea kulinda haki za kiraia ikiwemo haki ya kujieleza na kutoa maoni, ni vyema sote tusivuke nje ya mipaka yetu. Tusisahau kwamba mfumo wa Dola yetu ni kuongozana, kusimamiana na kuwajibishana,” amesema.
Amesema mwaka wa 61 wa Muungano umeangukia katika uchaguzi mkuu, ni matumaini yake sifa ya nchi itaendelea
kudumishwa kuwa ni kitovu cha amani na nchi ya kidemokrasia iliyojengeka juu ya misingi ya uhuru na haki.
“Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mahitaji yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yanapatikana kwa ukamilifu na kwa wakati. Aidha, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya utulivu na amani katika kipindi chote cha matayarisho hadi wakati wa uchaguzi, ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
“Wito wangu kwenu wananchi, mjitokeze kwa wingi kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, kujitokeza kugombea na hadi kupiga kura,” amesema.
Amewataka viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.
“Uchaguzi huu uwe ni fursa ya kuimarisha zaidi umoja na demokrasia yetu ili tupate viongozi bora na walio imara. Kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha migogoro, chuki, mivutano na uvunjifu wa amani ndani ya vyama, baina ya vyama au nchini kwa ujumla.
“Niseme kuwa, hakuna alie juu ya sheria na wote tunatakiwa kuendesha shughuli zetu za kisiasa tukizingatia kuwa amani na usalama wa nchi ndiyo kipaumbele cha kwanza,” amesema.
Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu amesema Serikali imeamua kuyapa maadhimisho haya kaulimbiu isemayo: "Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano wetu ni dhamana, heshima na tunu ya Taifa: Shiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025".
Amesema maadhimisho yatafanyika katika mikoa yote ya Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali wataungana na wananchi katika shughuli za uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Pia yamefanyika makongamano, michezo na shughuli za kitamaduni nchi nzima.
“Katika ngazi ya kitaifa, kesho Aprili 26, kwa niaba ya Serikali na wananchi kwa ujumla, nitatunuku nishani za Muungano kwa Watanzania wenzetu kama ishara ya kutambua utumishi na mchango wao katika ujenzi wa Taifa letu na katika kudumisha Muungano wetu,” amesema.