Biteko: Tudumishe Muungano

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, akizungumza katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru leo Alhamisi Aprili 25,2025 wakati wa ziara yake mkoani Arusha kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Muktasari:
- Amesema kuwa kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ni muhimu kuendelea kubaki kama Taifa moja kwa kudumisha amani, mshikamano na upendo kama ulivyoasisiwa na waasisi wa Muungano.
Arumeru. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka wananchi kuendelea kudumisha na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kudumisha mshikamano na amani kwa maslahi mapana ya Taifa ili kuendelea kutekeleza malengo ya waasisi wa Muungano.
Dk Biteko ameyasema hayo leo ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake mkoani Arusha, kuelekea miaka 61 ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Dk Biteko amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya manufaa ya mshikamano na umoja.
"Tunapoelekea miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, tuendelee kubaki kama taifa moja, Muungano ambao wazee wetu waliuasisi, tuendelee kuuenzi, tuutunze ili tuudhihirishe," amesema
"Tunu ya Muungano ndiyo inatufanya tuwe hapa leo, tuendelee kushikamana, tukumbatie amani, mshikamano wazee wetu walitupatia taifa moja tunapendana na tuna amani," amesema.
"Tusijaribu kuchezea amani, amani inapaswa kulindwa kwa gharama yoyoyote miaka 61 ya Muungano iwe kielelezo cha amani.
Akiwa hospitalini hapo Dk Biteko alikagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya afya na kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na kuwaheshimu watoa huduma.
Amesisitiza kuwa kuwa watoa huduma wa afya wakiwemo madaktari na manesi na kuwataka kuwatia moyo na kuungwa mkono katika kazi hiyo muhimu.
“Tuendelee kuboresha hospitali, Rais ameonesha njia, awa madaktari mnaowaona, manesi na wale wanaotuhudumia ni binadamu, kuna wakati wanachoka. Kuna wakati jibu la mtu wa kwanza, wa pili, wa tatu na wa nne haliwezi kufanana," amesema.
"Hata nyumbani kwako hauwezi kufananisha, tuna wagonjwa wengine wakija wanajiona kama wao ndio wagonjwa pekee, akiambiwa apange foleni anakasirika, akitoka pale anajirekodi tunanyanyaswa...muwatunze, wapeni ushirikiano, hakuna mtu asiyependa kutiwa moyo,” amesema Dk Biteko.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi ya Tengeru, amesema wananchi siyo mtu anayelalamika akisema anataka hiki ni anataka maendeleo na ni wajibu wa Serikali kuyatekeleza.
"Watanzania wanahitaji barabara nzuri,maji safi na salama, nishati ya umeme ya uhakika, wanataka wakienda hospitali watibiwe na ndiyo msukumo wa Rais.
"Sikio la serikali ni pana linalosikia sana, tumefundishwa kusema kidofo kutenda mengi.
Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema Muungano umelenga manufaa katika nyanja za jamii hivyo hawana budi kuuadhimisha kwa kujivunia miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema maboresho ya hospitali hiyo ya wilaya imeongeza idadi ya wagonjwa kutokana na huduma zinazotolewa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika Stendi Tengeru, amesema Mkoa wa Arusha umetenga fedha kutoka kwenye mapato yake ya ndani ambapo zitajumuishwa na za Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara.
"Barabara zimeendelea kuwa siasa,mkoa umeweka nguvu zake zote viongozi wenu wakiwemo wabunge na madiwani kipaumbele kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni barabara ili kuwe na miundombinu ya kuwezesha kupata maendeleo,"amesema.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Meru, Dk Elisante Fabian akitoa taarifa ya utekelezaji wa miundombinu ya hospitali hiyo, amesema mwaka 2023/24 walipokea Sh900 milioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma.
Amesema ukarabati huo ilianza Februari Mosi 2024 na umeanza kutoa huduma Januari Mosi, 2025.
Amesema mradi umehusisha ujenzi wa miundombinu ya majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), maabara bohari ya dawa na kichomea taka na kuwa maboresho yamesaidia utoaji huduma za afya kwa wagonjwa wa nje hadi kufikia 12,000 sawa na ongezeko la wagonjwa 6,400 waliohudumiwa Januari hadi Machi 2024 kabla ya maboresho," amesema.
Mmoja wa wananchi kutoka eneo la Calista Boniface amesema wazee wameboreshewa huduma awali wazee hawakuwa wakipewa kipaumbele cha huduma.
"Awali tulikuwa tukitembea umbali mrefu kufata huduma na hata ambazo tulikuwa tukifuata hazikuwepo zote hali iliyotulazimu kufuata huduma hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru ila maboresho ya huduma yamefanyika huduma zote tunapata hapa hatufuati mbali," amesema.