Dk Biteko aridhishwa utatuzi wa migogoro ya ardhi Monduli

Migogoro ya ardhi imekuwa kero kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mikakati kumaliza tatizo hilo.
Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa jitihada za kutatua migogoro ya ardhi ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.

Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati ametoa pongezi hizo jana Jumatano Aprili 23, 2025 wilayani Monduli, mkoani Arusha wakati akihutubia wananchi baada ya kuzindua Shule Mpya ya Sekondari ya Migungani iliyopo wilayani humo.
“Naomba kuwapongeza tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri sana hapa wilayani kwa masilahi mapana ya wananchi wa Monduli. Nimejulishwa kuwa, mmefanya mengi mno ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi hapa wilayani. Nimejulishwa kuwa sehemu kubwa ya changamoto hizi mmefanikiwa kuzitatua hongereni sana,” amesema Dk Biteko.
Ameipongeza pia kamati ya kutatua kero za wananchi inayoongozwa na mkuu wa wilaya ikiwa na wataalamu ambayo imejiwekea utaratibu wa kupokea kero kutoka kwa wananchi na kuzipatia ufumbuzi, ambapo ameitaka pia iratibu shughuli ya utoaji elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ardhi.

Akiwa shuleni hapo, Dk Biteko amewapongeza wananchi kwa kujenga Sekondari Migungani na kufikia asilimia 85 ya ujenzi huku Serikali ikichangia Sh500 milioni.
“Sote tunafahamu kuwa, elimu ni msingi mkubwa wa maendeleo. Sisi wana Monduli tayari tunayo shule yetu hii ambayo imeshakamilika. Hii ni miongoni mwa shule zilizopo wilayani hapa ambazo zitaendelea kutupatia elimu kwa vijana wetu,” amesema Dk Biteko.
Ameongeza kuwa shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 hivyo, amewataka wanafunzi kutunza miundombinu sambamba na kujifunza kwa bidii ili wajiandae kuwa wazalendo na raia wema, huku wakiwa na uwezo wa kutafuta majibu ya matatizo watakayokumbana nayo.
Kuhusu miradi ya umeme wilayani humo, amesema kuwa mwaka huu Serikali inatarajia kujenga mradi mkubwa wa umeme kwa lengo la kuuongezea nguvu umeme unaopatikana ili uweze kufika Loliondo na kusaidia wilaya hiyo kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo muhimu kiuchumi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga amesema wilaya hiyo ni tegemeo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wamekuwa wakishirikiana na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.

Pia, amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara, hospitali, shule na kuwa wilaya hiyo ni kati ya zinazofanya vizuri katika elimu.
Pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kuwekeza katika elimu nchini.