Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko: Msikubali kugawanywa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Esilalei, wilayani Monduli leo Jumatano Aprili 23, 2025 wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji katika ziara yake  mkoani Arusha,kuelekea maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Muktasari:

  • Watanzania wanaendelea kushuhudia Muungano uliodumu kwa miaka 61 bila kutetereka.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka wananchi kutogawanywa kwa itikadi ya dini wala siasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, ubunge na udiwani kwa manufaa ya Taifa.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumatano, Aprili 23, 2025, wilayani Monduli, mkoani Arusha, wakati akizungumza na wananchi kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizindua mradi wa maji katika Kijiji cha Esilalei, Dk Biteko amesema: “Ninatamani kuona hatugawanyiki na mtu yeyote wala hatuwekwi kwenye makundi ya dini wala ukabila.

“Nataka niwaombe wananchi wa Monduli pendaneni na shirikianeni na uchaguzi utakapofika uchaguzi chagueni kwa haki.”

Pia ametoa shime kwa wananchi wa Monduli kuutunza mradi huo wa maji wa Esilalei, huku akisema: “Nawapongeza Wizara ya Maji na Ruwasa kwa kusimamia mradi huu mzuri na wa uhakika, bila shaka, mtaona itakapofika Desemba, mwaka huu, awamu ya pili ya mradi itakuwa imekamilika.”

Amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inawapenda wananchi wa Monduli, na inawapongeza kwa uchapakazi wao kwenye kilimo na ufugaji.

Aidha, amewataka wachape kazi, na kwani Serikali imefikisha mradi huo wa maji kwa kuwa inapenda kuona mifugo yao inastawi.

Amesema ametumwa na Rais Samia, awaambie kuwa anawahakikishia wananchi hao kwamba wafugaji nchini wanatakiwa kuwa daraja la juu kama walivyo wananchi wengine.

“Amenituma niwaambie kila mnachohitaji, Serikali ndiyo inapaswa iwapatie ikiwamo nyenzo kama maji, umeme na barabara ili mfanikishe shughuli zenu, tayari Rais Samia ameapa kuwa Serikali anayoiongoza itawapatia nyenzo hizo,” amesema Naibu Waziri Mkuu huyo.

Kuhusu umeme, Dk Biteko amesema vijiji vyote vya Wilaya ya Monduli vimeshapata umeme, na kati ya vitongoji 236, vitongoji 72 vimepata huduma hiyo, na vilivyosalia vitapata huduma hiyo baada ya uchaguzi mkuu.

Akijibu ombi la Mbunge wa Monduli, Freddy Lowasa, Dk Biteko amesema; “Nguzo za umeme 20 alizoomba mheshimiwa mbunge, namwambia, kuanzia Alhamisi (kesho) hadi wiki inayokuja, tutaanza kuona watu wa hapa wanapata umeme bila masharti yoyote; katika maisha, tunapimwa kwa kazi si kwa maneno.”

Akizungumzia Muungano, Dk Biteko amesema umeshadumu kwa miaka 61, ni wa kipekee duniani kwa kuwa mataifa kadhaa yamejaribu kuungana lakini yameshindwa.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, amesema amefurahia wilaya hiyo kupata maji kwa kuwa maji ni uhai.

Hivyo, ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha inasaidia pia mifugo kupata maji.

Naye Mbunge wa Monduli, Freddy Lowasa, amesema kazi iliyofanywa na Serikali wilayani Monduli ni kubwa.

Amesema upatikanaji wa maji ulikuwa changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili wakazi wa maeneo hayo kwa muda mrefu, kwa kuwa huduma ya maji ilikuwa kero kuu kwao.

“Kwa miaka mingi, maji yamekuwa kero kubwa katika wilaya yetu, kwa kupata mradi huu, tunaomba umpelekee shukrani zetu Rais Samia,” amesema Lowassa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Festo Kiswaga, amesema wilaya hiyo ni moja yenye changamoto ya maji, na kuwa mradi huo utamaliza kero hiyo.

“Changamoto ya maji ya kunywa, na hasa kwa mifugo, iliwakabili wananchi wa Monduli ila wafugaji hawa wamepata maji na mifugo yao imepata sehemu salama ya kunywesha maji, kwani huwezi kutenganisha mfugaji na mifugo yao. Tunashukuru kwa mradi huu,”amesema.

Mmoja wa wananchi hao, Namnyaki Mollel, amesema awali kinamama walikuwa wakikumbana na changamoto ya kufuata maji umbali mrefu na kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.

“Kiukweli, mradi huu utatuokoa sisi wanawake na kutuwezesha kufanya shughuli za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kusaka maji, tutaondokana na adha hiyo kubwa iliyotukabili kwa muda mrefu,” amesema.