Mwinyi: Amani ni msingi mkuu maendeleo sekta ya miundombinu

Muktasari:
- Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewataka Watanzania kuendelea kuitunza na kuilinda amani, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo yanayopatikana kwenye sekta mbalimbali.
Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema amani ya Tanzania ndiyo msingi mkuu wa maendeleo yatakayopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo ya miundombinu.
Dk Mwinyi ameeleza hayo leo, Ijumaa Aprili 25, 2025, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Kibada–Mwasonga–Kimbiji kwa kiwango cha lami.
Uwekaji wa jiwe la msingi katika barabara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Muungano wa miaka 61 zinazoadhimishwa Aprili 26 ya kila mwaka.
"Hatua hii ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, ninayoiwekea jiwe la msingi leo, na utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo, ni matokeo ya kuendelea kwa amani katika nchi yetu."
"Amani tuliyonayo imewezesha Serikali kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Natoa wito kwa Watanzania tuendelee kuitunza amani hiyo ili nchi yetu ipige hatua za maendeleo," amesema.
Dk Mwinyi amesisitiza kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi, hivyo wananchi wana wajibu wa kuendelea kuilinda amani sambamba na kuhakikisha mchakato huo hauwi chanzo cha kuhatarisha amani ya Tanzania.
"Tuzingatie kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo tuendelee kudumisha amani iliyopo," amesema Dk Mwinyi.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi ametumia nafasi hiyo kuhimiza kuendeleza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ikiwemo kupatia ufumbuzi changamoto mbalimbali kama ambavyo viongozi waliomtangulia walivyofanya.
Ametaka kuendeleza ushirikiano huo kwa maslahi ya vizazi vijavyo, akisema miongoni mwa matunda ya Muungano ni pamoja na kuimarika kwa umoja na amani.
"Hizi ni tunu muhimu ambazo sote tuna wajibu wa kuzilinda. Umoja wa Watanzania una manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili wanaonufaika na fursa mbalimbali za kisiasa.
"Kutokana na hilo, hakuna mwananchi hata mmoja anayekosa faida za Muungano kwa namna moja au nyingine," amesisitiza Dk Mwinyi.
Kuhusu barabara hiyo
Dk Mwinyi ameitaka Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha wanaisimamia vyema ujenzi wa barabara hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta amesema barabara iliyozinduliwa na Dk Mwinyi ina urefu wa kilomita 41 (Kibada–Mwasonga hadi Kimbiji).
"Sehemu ya barabara kuanzia Kibada hadi Songani yenye urefu wa km 26.7 na sehemu ya pili inaanzia Songani kupitia Kijaka hadi Kimbiji yenye urefu wa km 14.3. Ujenzi wa sehemu zote mbili za mradi unatekelezwa kwa pamoja," amesema.
Besta amesema ujenzi wa barabara hiyo ulianza Aprili 10, 2024, na ulipangwa kukamilika Desemba 9, 2025, lakini kutokana na sababu mbalimbali za mkataba, mkandarasi amewasilisha ombi la nyongeza ya mkataba wa miezi mitano.
Mkandarasi wa mradi huo ni Estim Construction Company Limited kwa Sh83.8 bilioni na msimamizi wa mradi ni Tanroads Engineering Consulting Unit kwa Sh1.7 bilioni.
Mtendaji huyo amesema kupitia mradi huo, ajira 331 zimetolewa, kati ya hizo, 326 ni Watanzania na raia wa kigeni ni watano.
Maoni ya wananchi
Joseph Audax, mkazi wa Kigamboni amesema barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa wilaya hiyo.
"Barabara hii kwa muda mrefu imekuwa changamoto kwetu. Ujenzi wake utatusaidia kuimarisha uchumi wetu, kupunguza gharama za usafiri na kufika kwenye shughuli za kiuchumi kwa haraka," amesema.
Naye Mageni Charles amesema Kibada hadi Kimbiji nauli wanayotumia ni Sh1,000 kutokana na ubovu wa barabara, na ujenzi ukikamilika utakuwa na manufaa kwa wananchi.
Kauli ya Chalamila
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema mkoa huo upo salama japo yapo maswali yaliyoibuka juu ya wingi wa askari mtaani.
"Kuna watu walitaka kukinukisha. Tukasema ili ukinukishe, lazima ukubali kunuka hadi leo sijaona wa kukinukisha," amesema.
Amesema Rais Samia amedhamiria kulinda amani ya mkoa na hakuna mtu yeyote atakayefanya lolote kuharibu amani ya mkoa huo.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Chalamila amesema miundombinu ya Kibada hadi Kimbiji ilikuwa changamoto kwa wananchi wa Kigamboni, hivyo kuanza kwa ujenzi wake ni matumaini kwa wakazi wa wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.
Kuhusu umeme, Chalamila amesema Dar es Salaam haina shida yoyote ya umeme hasa upande wa Kigamboni, ambayo sasa imekuwa kimbilio la wawekezaji, ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo tatizo la umeme lilikuwa kubwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa amesema ujenzi wa barabara hiyo ni mfano wa miradi mikubwa ya barabara inayotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake.
"Barabara hii imekuwa kero kwa muda mrefu na sasa inakwenda kuisha. Itakuwa fursa muhimu ya kukuza uchumi na kuimarisha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam," amesema.