Serikali yaondoa zuio la mazao Malawi, Afrika Kusini

Muktasari:
- Baada ya kuanza utekelezaji wa zuio hilo Aprili 23, wafanyabiashara wa tufaa (apple) na zabibu jijini Dar es Salaam walipozungumza na Mwananchi walisema walikosa matunda hayo sokoni.
Dar es Salaam. Baada ya siku mbili za utekelezaji wa zuio kwa bidhaa za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, Serikali ya Tanzania imeliondoa kupisha majadiliano.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kupitia kituo cha runinga cha Azam, Aprili 23 alitangaza kuanza utekelezaji wa zuio kwa bidhaa hizo baada ya Aprili 17 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kueleza ifikapo siku hiyo Serikali ya Tanzania itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka mataifa hayo.
Katika taarifa ya Wizara ya Kilimo ya jana Aprili 25, 2025 iliyosainiwa na Waziri Bashe, imesema zuio hilo limeondolewa kuanzia leo Aprili 26.
Kutokana na zuio lililowekwa, amesema Serikali za Malawi na Afrika Kusini zimewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Kilimo za Tanzania ili kutafuta suluhisho.
Bashe amesema makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 2, 2025 utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma chini ya uratibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania.
Kuhusu Afrika Kusini, amesema majadiliano ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania yanaendelea kwa pamoja na Mamlaka za Afrika Kusini zinazohusiana na afya ya mimea na masoko.
"Kwa misingi hiyo, Wizara ya Kilimo inaondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Aprili 26, 2025 tukiamini majadiliano yanayoendelea yataleta suluhisho," imesema taarifa ya wizara.
Bashe amesema Serikali inawahakikishia wakulima na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kuwa, uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo kulingana na matakwa ya afya ya mimea, rasilimali za nchi zilizopo na mahusiano mapana ya kidiplomasia kwa faida ya wote.
Kwa nini zuio
Bashe alipotoa taarifa ya kusudio la kuweka zuio hilo Aprili 17, alisema Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwamo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi.
“Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi,” alisema.
Kuhusu Afrika Kusini alisema: “Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka 10 katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda masilahi ya nchi yetu.”
Baada ya kuanza utekelezaji wa zuio hilo Aprili 23, wafanyabiashara wa tufaa (apple) na zabibu jijini Dar es Salaam walipozungumza na Mwananchi walisema walikosa matunda hayo sokoni.
Hata hivyo, alipotangaza zuio Waziri Bashe alieleza hatua hiyo haitahatarisha usalama wa nchi wala wa chakula, kwani hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa tufaa au zabibu za Afrika Kusini.
Baadhi ya wafanyabiashara wa tufaa walisema hazipatikani sokoni na hata zilipokuwapo bei ilikuwa juu.
“Nafikiri hali hii ilianza mapema kwa sababu wiki mbili zilizopita yalianza mabadiliko ya kutopatikana apple nyekundu, hatukujua sababu. Siku nne baadaye gharama zikapanda ghafla,” amesema Thomas Jackson, mchuuzi wa matunda hayo eneo la taa za kuongoza magari Tabata.
Alisema awali walikuwa wakinunua boksi la tufaa ndogo 100 kwa Sh90,000 na lile la kubwa 90 kwa Sh100,000 lakini bei ilipanda kwa Sh100,000 na Sh110,000 mtawalia.
Licha ya kupanda kwa gharama, alisema Aprili 24, sokoni hapakuwa na matunda hayo.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Kilimo na Viwanda (TCCIA) mpaka wa Kasumuru, Josephat Mwakalinga akizungumza na Mwananchi Aprili 24 alisema hali iliyopo ni changamoto kwa wafanyabishara na wakazi wa eneo la mpakani.
"Kimsingi hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania ni kulinda masilahi ya Taifa. Tunaamini mwafaka utapatikana kwa pande zote mbili kukaa meza moja kutafuta suluhisho," alisema.