Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bidhaa za kilimo kutoka Malawi, Afrika Kusini marufuku Tanzania

Muktasari:

  • Marufuku hiyo imeanza leo Jumatano Aprili 23, 2025 imekuja baada ya kupita siku saba zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa mataifa hayo mawili.

Dar es Salaam. Sasa ni rasmi Tanzania imezuia bidhaa zote za kilimo kusafirishwa kwenda nchi za Malawi na Afrika Kusini, huku pia ikipiga marufuku kuingizwa nchini bidhaa kutoka mataifa hayo. Uamuzi huo umetangazwa leo Aprili 23, 2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe baada ya Malawi na Afrika Kusini kuzuia wafanyabiashara wa Tanzania kuingiza bidhaa za kilimo kwenye nchi hizo.

Wiki iliyopita Malawi na Afrika Kusini zilizuia shehena ya ndizi kutoka Tanzania kuingia kwenye nchi hizo hivyo, Waziri Bashe kutangaza siku saba akizitaka nchi hizo kuruhusu mazao hayo ama Tanzania itachukua hatua.

Hata hivyo, hadi kufikia leo Jumatano ambayo ndio siku ya mwisho, mataifa hayo yameendelea kushikilia msimamo huo hivyo, Tanzania kuamua kujibu mapigo.

Akizungumza na kituo cha luninga cha Azam Tv, Bashe amesema Afrika Kusini imekuwa ikiingiza Tanzania matunda mbalimbali yakiwemo zabibu na tofaa (apple), hivyo kuanzia sasa  ni marufuku bidhaa hizo kuingia nchini.

"Hatutaruhusu zao lolote linalotoka Afrika Kusini likihusiana na kilimo kuingia nchini," amesema Bashe.

Kuhusu Malawi, Waziri Bashe amesema nchi hiyo haijafuta notisi walioitoa hivyo amepiga marufuku mazao yoyote ya kilimo yanayotoka katika taifa hilo, kuingia nchini.

"Pia hatutaruhusu zao lolote la usafirishaji kupita ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Malawi.

"Wakati Malawi wanawakatalia wafanyabiashara wa Tanzania kupeleka mahindi kwao, wao  kupitia WFP (Shirika la Mpango wa Chakula Duniani) wananunua mahindi kwa hoja ya njaa, sasa mahindi yote walioyanunua hayatakwenda," amesema

Bashe amekazia kuwa Tanzania haitaruhusu shirika hilo kupeleka mahindi Malawi hadi pale watakapofungua soko la bidhaa kutoka Tanzania.

"Mei Mosi 2025 Malawi walikuwa wanaanza kuchukua mbolea kwa ajili ya maandalizi ya msimu wao wa kilimo kutoka Tanzania, hatutaruhusu mbolea kwenda nchi hiyo," amesema Bashe.

Kwa mujibu wa Bashe, hatua hiyo haitahatarisha usalama wa nchi wala wa chakula, akisema hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa tofaa au zabibu za Afrika Kusini.

"Tunachukua hatua hii kulinda biashara zetu, hii ni biashara," amesisitiza Bashe.

Hata hivyo, Bashe amesema wakati mazungumzo yanayoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabiti Kombo, yakiendelea na mataifa hayo, Serikali ya Tanzania haiwezi kuishi kizuizini.