Prime
Marufuku ya bidhaa za Malawi na Afrika Kusini kilio kwa wauza ‘apple’, chaanza

Muktasari:
- Wafanyabiashara wasema wanatafakari cha kufanya, washauri Serikali kushughulikia changamoto iliyopo.
Dar es Salaam. Marufuku iliyotolewa na Serikali kwa bidhaa za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, imewaathiri wafanyabiashara wa tufaa (apple) na zabibu jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kupitia kituo cha luninga cha Azam, Aprili 23 mwaka huu alitangaza kuanza utekelezaji wa zuio kwa bidhaa hizo baada ya Aprili 17 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kueleza ifikapo siku hiyo Serikali ya Tanzania itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka mataifa hayo.
Akitoa zuio hilo, Bashe amesema hatua hiyo haitahatarisha usalama wa nchi wala wa chakula, akieleza hakuna Mtanzania atakayekufa kwa kukosa tufaa au zabibu za Afrika Kusini.
Wafanyabiashara wa matunda hayo katika Barabara ya Mandela, Dar es Salaam waliozungumza na Mwananchi walisema tufaa hazipatikani sokoni na hata zilizopo bei ilikuwa juu.
“Nafikiri hali hii ilianza mapema kwa sababu wiki mbili zilizopita yalianza mabadiliko ya kutopatikana apple nyekundu, hatukujua sababu. Siku nne baadaye gharama zikapanda ghafla,” amesema Thomas Jackson, mchuuzi wa matunda hayo eneo la taa za kuongoza magari Tabata.
Amesema awali walikuwa wakinunua boksi la tufaa ndogo 100 kwa Sh90,000 na lile la kubwa 90 kwa Sh100,000 lakini bei ilipanda kwa Sh100,000 na Sh110,000 mtawalia.
Licha ya kupanda kwa gharama, alisema jana, sokoni hakukuwa na matunda hayo.
“Nimeambiwa hadi Serikali itakaporuhusu uingizaji wa bidhaa kutoka Afrika Kusini na sijui itakuwa lini? Naomba Serikali ifanye mazungumzo na viongozi wenzao kumaliza tatizo hili, maana wengine tunaogopa kubadilisha biashara kwa haraka,” alisema.
Daudi Kipingu, anayeuza tufaa eneo la Buguruni Darajani amesema hakuwahi kufikiria siku moja bidhaa hiyo ingeweza kupotea sokoni ghafla.
“Ni mabadiliko magumu kwangu, apple ilikuwa bidhaa ya haraka. Watu walikuwa wanakuja hata usiku kununua sasa biashara imeporomoka, ninalazimika kubadilika ili kuendelea na maisha,” amesema.
Sixtus Huruma, mchuuzi wa matunda hayo eneo la External, Ubungo amesema alimaliza mzigo aliokuwa nao akitarajia kuchukua mwingine leo (jana) lakini alipigiwa simu na rafiki yake kuwa matunda hayo kwa sasa hakuna.
"Asubuhi nilijiandaa kwenda kufuata mzigo Kariakoo, Mtaa wa Aggrey lakini nikaambiwa hakuna kitu, hali ni mbaya Serikali imekataza matunda kuingia nchini," amesema.
Amesema anaitegemea biashara hiyo kuendesha maisha yake na kwamba, alikuwa na wateja wake maalumu, hivyo kwa sasa haelewi ni nini atafanya.
Kwa upande wao, wakulima na wafanyabiashara wa mazao mkoani Mbeya wameunga mkono uamuzi wa Serikali, licha ya kuwa una athari kwa uchumi.
Mfanyabiashara wa ndizi na parachichi, Ipyana Mwalukasa amesema: "Uamuzi wa Waziri wa Kilimo ni sahihi, lakini ikumbukwe athari ya kiuchumi itajitokeza kwa kuzingatia ukosefu wa masoko ya uhakika ya ndani na asilimia kubwa ya wafanyabiashara wana mikopo."
Amesema wakati wa utekelezaji wa zuio hilo, Serikali iangalie njia mbadala ya kuwanusuru kwa kuelekeza halmashauri kuweka mifumo mizuri ya kusaka masoko ya ndani.
"Asilimia kubwa mazao kama ndizi, tangawizi na parachichi zinazolimwa Rungwe, soko lake kubwa liko Malawi ambako ndiko kimbilio kwa miaka yote," amesema.
Mfanyabiashara, Mary Azamera amesema Serikali wakati imeweka zuio itafute njia mbadala ya kuokoa wakulima.
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara wa Kilimo na Viwanda (TCCIA) mpaka wa Kasumuru, Josephat Mwakalinga amesema hali iliyopo ni changamoto kwa wafanyabiashara na wakazi wa eneo la mpakani.
"Kimsingi hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania ni kulinda masilahi ya Taifa. Tunaamini mwafaka utapatikana kwa pande zote mbili kukaa meza moja kutafuta suluhisho," amesema.
Kwa nini zuio
Bashe alisema Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwamo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi.
“Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi,” alisema.
Kuhusu Afrika Kusini alisema: “Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi nchini Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka 10 katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda masilahi ya nchi yetu.”
Imeandikwa na Devotha Kihwelo (Dar), Hawa Mathias na Saddam Sadick (Mbeya)