Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi awatwisha zigo wajumbe wa CCM

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wajumbe watakaopiga kura za maoni kuamua kuhusu kupatikana kwa wagombea wanaokubalika na wananchi.

Mara. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wajumbe watakaopiga kura za maoni, wachague wagombea kwa kuwasikiliza wananchi wanamtaka nani apitishwe ili wampigie kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Sababu ya kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, ni kiu ya chama hicho katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu, kupata wagombea watakaokubalika na wananchi na sio wanaopitishwa kwa nguvu ya fedha zao, huku akiwasisitiza wajumbe wafanikishe hilo.

Amesema chama hicho kinatambua kuwepo kwa wabunge wake waliopitishwa na kushinda uchaguzi, lakini wamehudumu kwa miaka mitano bila kurudi majimboni walipo wananchi waliowachagua.

Sambamba na hilo, ameeleza ni msimamo wa CCM kuenzi na kuakisi maono, mtazamo na falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili kuendelea kuiona Tanzania yenye amani, mshikamano na umoja.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiahiriki Ibada fupi katika kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere nyumbani kwake Mwitongo mkoani Mara

Dk Nchimbi ameyasema hayo leo, Alhamisi Aprili 24, 2025 alipozungumza na wananchi wa Kiabakari kuhitimisha siku ya tatu ya ziara yake katika Mkoa wa Mara.

Katika kufanikisha kiu ya CCM kupata wagombea watakaokubalika na wananchi, amesema kumefanywa maboresho ya kikanuni kuongeza idadi ya wajumbe watakaopiga kura za maoni.

Idadi iliyopo sasa, amesema inaondoa kasumba waliyokuwa nayo baadhi ya wagombea, kuhesabu wajumbe na kuwapa fedha ili wawachague.

"Kulikuwa na watu ndani ya miaka mitano hawafanyi kazi wanaishia kuhesabu kwamba wajumbe wangapi awape fedha wampitishe, sasa hivi tumewaongezea wajumbe kama kuwapa fedha, kwa sasa utawapa wangapi," amesema.

Hata hivyo, Dk Nchimbi amesema pamoja maoni ya mjumbe binafsi, siku ya kura za maoni, wananchi wasiogope kuwaambia wanataka nani akapigiwe kura ili apitishwe kwa sababu ndiye hitaji lao.

"Waambieni bila woga kwamba tuleteeni mtu fulani tutampa kura zote," amesema.

Amesema wajumbe nao wanapaswa kuhakikisha wanasikiliza kauli za wananchi wanapoenda kupiga kura za maoni.

"Tukifanya hivi, CCM itapata wagombea watakaokubalika na kupigiwa kura nyingi na wananchi," ameeleza Dk Nchimbi.

Mtendaji Mkuu huyo wa CCM, amewasihi wajumbe wakati wa kura za maoni, wahakikishe wanawachagua watu kwa sifa za kweli, badala ya misingi ya makabila yao, dini na utajiri.

Amesema wanapaswa kuchagua watu kwa misingi ya kuwatumikia na ni jukumu la wajumbe kuleta wagombea wanaokubalika mbele ya wananchi.

Ameambatanisha ujumbe wake huo na msisitizo wake kwa wananchi kujiandikisha daftari la kudumu la wapiga kura, ili watakapoletewa wagombea wanaowataka wawe na haki ya kuwapigia kura.

Awali, akizungumza baada ya ukaguzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Tehama cha Mwalimu Nyerere (MJNUAT), Dk Nchimbi amesema Tanzania isingekuwa ilivyo sasa kama sio juhudi za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Kwa sababu ya misingi aliyoiweka, amesema CCM itaendelea kumuenzi na kuakisi falsafa zake ili kuleta amani, mshikamano na umoja katika taifa.

"CCM kamwe haitaacha misingi ya Baba wa Taifa na itajinasibisha na kazi nzuri iliyofanywa naye na itamuenzi kwa kila namna," ameeleza.


Amesema hakuna mfano mwingine kuhusu mambo yaliyofanywa na Baba wa Taifa nchini, kwani imewafanya Watanzania waone fahari kujitambulisha kwa utaifa wao.

"Ni hamu yangu kuona kwamba Watanzania tunaendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu maono yake yana nia njema kwa nchi yetu," amesema.

Akizungumzia mradi wa ujenzi wa MJNUAT, Meneja wa mradi huo, Osward Bujiku amesema miradi yote inagharimu kiasi cha Sh96 bilioni ikihusisha ujenzi wa majengo na miundombinu mingine katika mikataba mitano.

Kati ya mikataba hiyo, amesema wa kwanza unagharimu Sh20.5 bilioni ukihusisha majengo saba, wa pili ni Sh16.9 bilioni kwa majengo manne.

Mikataba mingine, amesema unagharimu Sh20.5 na mwingine ni Sh8.7 bilioni na jumla ni Sh96 bilioni.

Amesema miradi yote hiyo inatekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi Tanzania (HEET).

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi amesema historia ya ujenzi wa chuo hicho ilianza mwaka 2010 wakati wa utawala wa awamu ya nne.

Ameeleza baadaye awamu ya sita, Rais Samia akaelekeza mradi huo lazima uanze na ukamilike na fedha zikatolewa.

"Ni matarajio yetu kuwa mradi utakamilika kama ilivyokusudiwa na Oktoba kundi la kwanza la wanafunzi wanatakiwa kufika hapa watafika," amesema.

Katika ziara hiyo, Dk Nchimbi alizuru na kufanya ibada fupi katika kaburi la Baba wa Taifa nyumbani kwake Mwitongo mkoani Mara.

Akizungumza nyumbani hapo, mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere amesema sio Dk Nchimbi pekee ni viongozi wengi wa CCM na Serikali wamekuwa wakitembelea eneo hilo.


Hatua hiyo, amesema inathibitisha kuwa chama hicho na Serikali vinathamini mchango wa mwasisi huyo wa taifa kwa yale aliyoyafanya alipokuwa hai.

Kuhusu hatua ya Dk Nchimbi kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu, Madaraka amesema ni jambo jema na anamtakia kila la kheri katika safari hiyo.

"Nasikia faraja kwa sababu sio kila sehemu unaweza kutembelewa na viongozi kila wakati ni heshima na tunaomba hali ya kumuenzi Baba wa Taifa iendelee kwa kuwa alikuwa kiongozi na alifanya mazuri katika taifa," amesema.