Dk Nchimbi: Hazina ikamilishe malipo ya fidia kwa wananchi Bunda

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na wananchi wa Bunda, aliposimama kuwasalimia, akiwa njiani kuelekea Musoma, leo Jumanne Aprili 22, 2025.
Muktasari:
- Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetaka kukamilishwa haraka kwa malipo ya fidia za wananchi waliopisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ajili ya uhifadhi na uendelezaji wake.
Bunda. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, amemtaka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, kuhakikisha anafanikisha upatikanaji wa fedha za kumalizia malipo ya fidia kwa wananchi wa Nyatwale.
Amesema kwa uzoefu wake, anaamini haitachukua siku 14 kwa Dk Nchemba kutoa fedha za malipo ya fidia hiyo, kwa kuwa mara zote akimwagiza huwa hapitishi siku hizo.
Fedha hizo ni sehemu ya malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa ajili ya uhifadhi na uendelezaji wake.
Dk Nchimbi amesema hayo leo, Jumanne Aprili 22, 2025, alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara, alikoenda kwa ziara ya kikazi.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na wananchi wa Bunda, aliposimama kuwasalimia, akiwa njiani kuelekea Musoma, leo Jumanne Aprili 22, 2025.
Amesema tayari asilimia 90 ya fidia hizo zimeshalipwa, na iliyobaki ni kidogo, na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshaelekeza zilipwe.
"Namuelekeza Waziri wa Fedha (Dk Nchemba) huko aliko, hizo fedha zitoke. Bahati nzuri sikuwahi kumwagiza zikapita siku 14 hajatekeleza," amesema.
Pia, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ashirikiane na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana, kumaliza changamoto zilizopo.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuhakikisha wanadai haki zao kwa kufuata utaratibu, kwa kuwa Serikali iko mbioni kufanikisha hilo.
"Kama mtu ana malalamiko afuate utaratibu mzuri. Bahati nzuri mna mkuu wa mkoa mzuri," amesema.
Sambamba na hilo, amesema kwa kawaida mwaka wa uchaguzi huwa na maneno mengi, yakiwemo yasiyofaa kwa Taifa.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza na wananchi wa Bunda, aliposimama kuwasalimia, akiwa njiani kuelekea Musoma, leo Jumanne Aprili 22, 2025.
Amewataka wananchi kuhakikisha hawafuati maneno ya wanasiasa yatakayohatarisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, amewataka wasiyakatae maneno hayo kwa hasira, badala yake wawaeleweshe wanasiasa hao athari za maneno hayo kila wanapopata nafasi.
Katika mkutano huo, Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa, amewataka wananchi kuhakikisha wanajitenga na mitazamo hasi dhidi ya Taifa.
Amewataka kuhakikisha wanalinda amani katika uchaguzi na wayaepuke maneno yanayohatarisha umoja wa kitaifa.
Dk Nchimbi yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku sita itakayohusisha wilaya zote tano mkoani humo, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Mwisho.Dk Nchimbi yupo mkoani Mara kwa ziara ya siku sita itakayohusisha wilaya zote tano mkoani humo, kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.