Alipwa mapunjo ya nauli ya Sh500,000 aliyosotea kwa miaka 31

Askari magereza mstaafu Christina Mjema (90) akizungumza baada ya kupatiwa mafao yake ya nauli ya mizigo ya Sh500,000 aliyosotea kwa miaka 31 tangu astaafu mwaka 1994. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Malipo hayo ya nauli ya mizigo ya Sh500,000 kutoka Gereza la Babati mkoani Manyara hadi nyumbani kwao Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro amepatiwa Christina Mjema aliyekuwa askari Magereza, baada ya kustaafu mwaka 1994.
Babati. Askari mstaafu wa Jeshi la magereza, Christina Mjema (90) amepatiwa malipo yake ya nauli ya mizigo Sh500,000 ya kutoka gereza la Babati mkoani Manyara hadi nyumbani kwao Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, baada ya kudai kwa miaka 31.
Mjema tangu mwaka 1994 amekuwa akidai malipo yake ya nauli ya usafiri wa mizigo, hatimaye mwaka huu akiyasotea kwa zaidi ya miaka 31 amefanikiwa kulipwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga kuingilia kati.
Baada ya kusota kwa miaka 30 akifuatilia malipo hayo, alifikisha kilio chake wa Sendiga ambaye aliwasiliana na Jeshi la Magereza hadi wakatoa fedha hizo za nauli ya mizigo.
Hata hivyo, Mjema akizungumza na waandishi wa habari Aprili 22, 2025 amewahimiza watendaji walioko serikalini kutenda haki katika kutatua kero za wananchi.
Akipokea fedha hizo taslimu ambayo ni malipo aliyodai ni mapunjo ya nauli ya kusafirisha mizigo baada ya kustaafu mwaka 1994 Jeshi la Magereza amesema kutenda haki ni kumcha Mwenyezi Mungu.
"Naomba maisha marefu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwani kupitia Mkuu wa Mkoa, Queen Sendiga nimewasilisha kero yangu na kulipwa fedha zote nashukuru nimepata haki yangu," amesema Mjema.
Akilizungumzia hilo, Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Manyara, Solomon Mwamdingu alibainisha kuwa malipo hayo ni nauli ya kutoka Gereza la Babati alikokuwa akifanyia kazi hadi nyumbani kwao wilayani Same mkoani Kilimanjaro.
"Hii iliyotumika ni busara isipokuwa kama ana madai mengine ya msingi atalazimika kuwasilisha katika vyombo vingine vya sheria ila siyo Jeshi la Magereza," amesema Mwamdingu.
Mjema amekiri kupokea fedha hizo mbele ya Sendiga kwa kusaini nyaraka za malipo huku akisoma maandishi vizuri pasipokupoteza uoni.
"Nimepokea fedha hizo Sh500,000 na hivi sasa sitakuwa na madai mengine kwa ajili ya gharama za kusafirisha mizigo tena dhidi ya Magereza," amesema Mjema.
Sendiga amefafanua kuwa hiyo ni hatua ya kielelezo cha Serikali katika kutatua kero za wananchi kupitia malalamiko ya Mjema yaliyodumu kwa zaidi ya miaka 31.
Sendiga ameeleza kwamba baada ya kupokea malalamiko hayo aliyafanyia kazi kwa ukaribu hadi mama huyo akafanikiwa kupatiwa haki yake.
Mkazi wa mjini Babati, Lucia Mandoo amesema baadhi ya watumishi wenye kupenda rushwa ndiyo wanasababisha matukio kama haya ya madai ya mafao ya muda mrefu.
"Mtu anakaa muda mrefu hivyo akifuatilia mafao ya nauli ilihali wakati anastaafu wahusika walikuwa wanatambua kwamba anapaswa kutoka kazini kurudi nyumbani kwao," amesema Mandoo
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa (CCM) Mkoa wa Manyara, Christina Masagasi amesisitiza kudumisha mahusiano kati ya wananchi na chama hicho katika kutatua kero zao.