Polisi waimarisha ulinzi Kisutu, kesi ya Lissu ikisikilizwa kimtandao

Muktasari:
- Leo Alhamisi, Aprili 24, 2025, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam itasikiliza kesi mbili kwa njia ya mtandao zinazomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, pia Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama hiyo.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeimarisha ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Aprili 24, 2025, ambapo kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, inatarajiwa kutajwa wakati wowote kuanzia sasa.
Maeneo ya ndani na pembezoni mwa mahakama hiyo yamezingirwa na askari wenye silaha, virungu na mbwa wa polisi, pia wapitanjia wakizuiwa kusogea karibu.
Katika lango kuu la kuingilia mahakamani, ni mawakili pekee ndio wanaoruhusiwa kuingia, huku waandishi wa habari nao wakizuiwa kushuhudia mwenendo wa kesi hiyo itakayoendeshwa kwa njia ya mtandao.
"Haturuhusu mtu yeyote kuingia mahakamani zaidi ya mawakili," amesema mmoja wa askari waliokuwa getini, akiwa ameambatana na zaidi ya askari 15 waliokuwa wakilinda eneo hilo.

Mwananchi imeshuhudia tukio la kijana mmoja aliyekuwa akibishana na polisi, huku akipaza sauti akisema yuko tayari kuuawa, lakini anachotaka ni kujua hatima ya Tundu Lissu.
Hata hivyo, kijana huyo alifukuzwa kwa kutumia mbwa wa polisi waliokuwa kwenye doria mahakamani hapo.
Mbali na ulinzi huo kuimarishwa katika Mahakama hiyo, pia katika Barabara ya Bibi Titi eneo Akiba, Baridi, magari kadhaa ya Polisi yameegeshwa pembezoni mwa barabara yakiwa na askari.
Vilevile eneo la Fire katika Barabara ya Morogoro hali na kama ilivyo eneo la Akiba na Baridi, ambao magari kadhaa ya Jeshi la Polisi yamepaki pembezoni mwa barabara huku yakiwa na askari.
Mwananchi imeshuhudia magari matano yakiwa na askari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambao baadhi yao yalishusha askari na kuondoka na mengine yakibakia eneo hilo.
Aidha, Mwananchi imeshuhudia baadhi ya wafuasi wa Chadema wakikamatwa na kupelekwa vituoni huku Jeshi la hilo likionya raia yeyote kutosogea karibu na mahakama hiyo.
Mtandao wa Chadema umeripoti baadhi ya waliokamatwa ni Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche akiwa daraja la Salender kuelekea Kisutu, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika yeye anadaiwa kukamatwa akiwa maeneo ya Fire na John Pambalu, Mkurugenzi wa Mafunzo, Oganaizesheni na Uchaguzi.
Pia, Elizabeth Mambosho, Katibu wa Chama Wilaya Ilala na Lucas Ngoto, mwenyekiti wa chama hicho kanda ya Serengeti.

Kwa sasa baadhi ya kesi zimeanza kuitwa Mahakamani hapo, huku kesi zenye washtakiwa ambao hawana dhamana ambao wapo rumande, wakiitwa kwenda kusikiliza kwa njia ya video.
Jitihada za Mwananchi kupata Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Jumanne Muliro zinaendelea kujua idadi ya waliokamatwa na hatima yao.
Endelea kufuatilia Mwananchi