Wengine watano wajivua uanachama wa Chadema, wamlaumu Heche

Muktasari:
- Kundi hilo, linaungana na kundi la kwanza lilotangaza kuhama Mei, 7, 2025 lililowajumuisha viongozi waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Dar es Salaam. Makada wengine watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na aliyekuwa katibu wa kundi la G55, Edward Kinabo wametangaza kujivua uanachama wa chama hicho, huku wakimnyooshea kidole Makamu Mwenyekiti, John Heche kwa madai kwamba amekuwa akitoa maneno yanayochoche chuki na mgawanyiko badala ya kuwaunganisha wanachama.
Wengine walioungana na Kinabo ni aliyekuwa miongoni mwa mameneja wa Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Freeman Mbowe katika uchaguzi wa ndani ya chama hicho na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema Wilaya ya Temeke, Eliya Gregory.
Vilevile, yumo Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) Wilaya ya Ilala, Rachel Kitamkadala, mjumbe wa mkutano mkuu taifa, Grace Ngola na mjumbe wa mkutano mkuu taifa kupitia Bawacha, Salma Sharif.

Kundi hilo, linaungana na kundi la kwanza lilotangaza kuhama Mei, 7, 2025 lililowajumuisha viongozi waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya aliyekuwa mwenyekiti, Freeman Mbowe.
Viongozi hayo ni pamoja na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu ambao walidai uwepo wa ubaguzi, udikiteta na ukiukwaji wa Katiba ya chama unaofanywa na uongozi mpya.
Mbali na hao, yumo pia aliyekuwa Katibu wa Bawacha Taifa, Catherine Ruge, aliyekuwa katibu wa sekretarieti, Julis Mwita na aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Uenezi, John Mrema. Nao walisisitiza kwamba kuondoka kwao si mwisho wa mapambano, bali wanatafakari jukwaa lingine la kwenda.
Taarifa zilizopo ni kwamba makada hao wanafanya mazungumzo na vyama mbalimbali na huenda wakahamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kinachoongozwa na Hashim Rungwe.
Hata hivyo, akiwa Karagwe mkoani Kagera, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amewashukia makada hao waliotangaza kujivua uanachama na kutaja sababu za kuhama kwao kuwa wamefika bei na hasira ya kukosa nafasi za ujumbe kwenye sekretarieti mpya.
Heche anayeendelea na mikutano ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu operesheni yao ya “No reforms, no election” Kanda ya Victoria, alisema pamoja na kuhama kwao, aliwataka Watanzania kutokatishwa tamaa na wanaofika bei na kusaliti imani ya kupigania mabadiliko ya kimfumo kwenye uongozi wa nchi, bali waendelee kupambana.
Wakizungumzia uamuzi wao leo Mei 9, 2025 Dar es Salaam kwenye mkutano wa vyombo vya habari wa kutangaza uamuzi huo, Kinabo amesema gari la Chadema limechoka, halina “spea mpya”, wanakwenda kupanda gari lingine.
“Natangaza rasmi kuagana na gharika la Chadema, halina matumaini mapya tena, kwa umoja wetu, tunaenda kwenye chama kingine, tunaenda kupanda gari lingine mpya, tutaunganisha nguvu zetu tulizotokana nazo huku na kukifanya kuwa kikubwa,” amesema Kinabo.

Kada wa Chadema, Edward Kinabo na wenzake wakiwa wameshikana mikono ikiwa ni ishara ya umoja, baada ya kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho leo Ijumaa Mei 9, 2025 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Amesema ndani ya chama hicho hakuna heshima tena iliyojengeka kwa muda mrefu, lakini chuki za wenyewe kwa wenyewe zimetamalaki na zimekuwa kubwa kuliko mifumo kandamizi inayofanywa na dola na washindani wao wa kisiasa.
“Vita ya ndani imekuwa kubwa kuliko ya nje na yamekuwa yakifanyika hadharani na raia wamekuwa wakitushangaa kila uchao, chuki na makundi yamekuwa yakiibuka kiasi kwamba hatuwezi kurejesha upendo na heshima ile tuliyoijenga kwa wivu mkubwa,” amesema Kinabo.
Kwa mujibu wa Kinabo, chama hicho kwa muda mrefu kilikuwa kinatambulika kwa umahiri wa kujenga hoja, lakini kwa sasa sura na picha iliyojengeka ya kunoa viongozi wenye uwezo mbele ya uso wa dunia, haipo tena.
“Tunaungana na viongozi wetu waliotangaza kuhama, walipo tupo na watakapoenda tupo, ingawa bado tunatafakari jukwaa litakalokuwa bora kwenda kufanya siasa zetu. Tunaondoka lakini kuna wenzetu wanatufuata,” amesema Kinabo.
Amesema wanaondoka na wanaenda kujiunga na jukwaa lingine bora litakalosadifu misingi kulingana na ubora walionao katika kuwapigania Watanzania ili waneemeke na maisha mazuri kutokana na utajiri wa rasilimali zilizopo nchini.
Kwa upande wake, Gregory amesema hakuna masika isiyokuwa na mbu, wanaondoka wamechoka kuishi kama yatima na kuendelea kutengwa na uongozi mpya ambao hautaki kuunganisha wanachama.
“Najivua vyeo vyangu vyote ndani ya Chadema, nahama rasmi na nautangazia umma, Chadema si jukwaa sahihi la kidemokrasia, tunaenda kutafuta jukwaa lingine zuri na bora,” amesema Gregory.
Amesema ndani ya chama hicho limeibuka kundi ambalo linadhani lenyewe ni bora na wala halikosei na limekuwa likikingiwa kifua na pia lipo kundi lingine ambalo linaonekana ni wakosaji.
Kombora kwa Heche
Kinabo amesema Heche amekuwa akiongea uongo unaoeneza chuki na dharau dhidi ya kundi ambalo halikumuunga mkono katika uchaguzi wa ndani uliofanyika Januari 21, 2025 huku akisisiza kuwa kwa hadhi yake hakupaswa kusema uongo kwa viongozi waliomaliza muda wao.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akisalimiana na wananchi wa Omurushaka Wilaya ya Karagwe waliomzuia njiani akiwa njiani kwenda mjini Kayanga yaliyo Makao Makuu ya Wilaya ya Karagwe. Heche na msafara wake alikuwa anatoka Nkwenda wilayani Kyerwa. Picha na Peter Saramba
“Jana, akiwa Kagera, amesema viongozi waliohama waliokuwa wajumbe wa sekretarieti hawakuwa na nafasi na wanaondoka baada ya kukosa uongozi, ni jambo la kusikitisha kuwadharau viongozi kama hawa waliokitumikia chama kwa wivu mkubwa,” amesema Kinabo.
Amesema Heche anaeneza chuki za makusudi kama alivyokuwa akituhumiwa na makada wa chama hicho kwa muda mrefu.
“Anasema uongo bila sababu kwamba kina Kigaila hawana maana yeyote, ni uongo wa wazi kabisa, hawa watu walichaguliwa na kupigiwa kura na wajumbe wa Baraza Kuu la chama chetu baada ya kukidhi vigezo na kuonekana wana kitu, unasemaje wamefikia bei?” amehoji.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa ambazo Mwananchi imezipata, Chaumma wanakotaka kwenda bado vikao vinaendelea kwani uongozi wa chama hicho upo katika wakati mgumu wa kuliridhisha kundi la wanachama hao.
Inadaiwa kwamba baadhi ya makada hao wameweka masharti ili wajiunge na chama hicho ikiwemo kupewa nafasi za juu ndani ya chama, jambo ambalo limekuwa likijadiliwa na uongozi wa chama hicho ili kupata mwafaka.