Prime
Vigogo wengine Chadema watarajiwa kutimka

Muktasari:
- Taarifa ambazo Mwananchi limedokezwa baadhi ya makada wa Chadema wenye nafasi mbalimbali kuanzia leo Ijumaa wataanza kutangaza kujiondoa ndani ya chama hicho ili kutafuta jukwaa jingine la kisiasa.
Dar es Salaam. Baada ya vigogo waandamizi kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanaofuata sasa ni baadhi ya viongozi wa kanda, mikoa na wilaya, Mwananchi limedokezwa.
Jumatano ya Mei 7, 2025, wanachama wa Chadema waliokuwa kwenye sekretarieti wakati wa uongozi wa Freeman Mbowe, walitangaza kuondoka ndani ya chama hicho kwa sababu kimeshindwa kufuata malengo ya kuanzishwa kwake.
Mbali na hao, pia, baadhi ya viongozi wa kitaifa wanaowakilisha mabaraza ya Chadema ya Bawacha (Baraza la Wanawake la Chadema), Bavicha (Baraza la Vijana la Chadema) na Bazecha (Baraza la Wazee la Chadema) nao wako mbioni kutimka katika chama hicho, lakini huenda likawa kundi la mwisho.

Wanachama hao ni waliokuwa manaibu makatibu wakuu Tanzania Bara na Zanzibar, Salum Mwalimu na Benson Kigaila, aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi na Mambo ya Nje, John Mrema. Wengine ni aliyekuwa katibu wa sekretarieti, Julius Mwita na aliyekuwa Katibu wa Bawacha, Catherine Ruge.
Makada hao wameeleza sababu iliyowasukuma kujivua uanachama wao wa Chadema ni uongozi wa Tundu Lissu kushindwa kuishi misingi ya kuanzishwa kwake.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa amesema kuondoka kwa makada hao hakuna pengo lolole waliloliacha ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Pia, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche jana Alhamisi akiwa ziarani mkoani Kagera alisema walichokisema kina Mrema hakina ukweli bali wamefika bei na wana taarifa kuna wengine pia watafuata.
Uwepo wa kundi jingine la viongozi watakojiuvua uanachama ulidokezwa na Mwalimu akisema: “Sio sisi tu, kuna gharika linakuja...hawataweza kuizuia kwa hasira, watu wamegundua maana kila ukiwashauri kitu, unaaambiwa wewe ni timu fulani au msaliti.
“Hawataki kushaurika, wao wanalolitaka ndilo linalokuwa, No reforms, no election, sasa ukijaribu kushauri unaambiwa wewe umetumwa kuzuia ajenda ya bila mabadiliko hakuna uchaguzi,” amesema Mwalimu, aliyewahi kuwa mgombea mwenza wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Tayari kina Mrema na wajumbe wenzake waliokuwa wakiunda sekretarieti, wametangaza kujiondoa Chadema na walisema wanakwenda kutafuta jukwaaa jingine la kuendeleza harakati za siasa, licha ya kutotaja chama watakachojiunga kwa hatua ya sasa.
Wakati vuguvugu la vigogo hao kujivua uanachama wa Chadema halijapoa, imeelezwa vigogo wengine walioko katika uongozi wa kanda, mabaraza, mikoa na wilaya wapo mbioni kuwafuata.
Mmoja wa makada waandamizi (jina limehifadhiwa), ameliambia Mwananchi kituo kinachofuata ni viongozi wa ngazi za chini kujiuzulu nyadhifa zao na kujivua uanachama ili kutafuta jukwaa jingine.
“Wiki hii itakuwa 'busy' maana tunakwenda kwa ‘series’ (hatua), wameanza waliokuwa wajumbe wa sekretarieti, wanaofuata ni wale viongozi wa kanda.
“Wakimaliza hao, watafuata viongozi wa mikoa, watafuata wa wilaya. Lile gharika alilosema Mwalimu ndio linakuja, watu wakae mkao wa kula maana wamechoshwa na yanayoendelea ndani ya Chadema,” amesema mtoa taarifa huyo.

Hata hivyo, Mwananchi inazo taarifa zinazodai baadhi ya vigogo wa kamati ya utendaji za kanda, mikoa, wilaya wanaoondoka huenda wakaanza kufanya mikutano na wanahabari kuanzia leo Ijumaa, Mei 9, 2025 hadi Jumatatu kwa lengo la kujivua uanachama.
Wakati kukiwa na vuguvugu hilo, Jumatano, Kanda ya Kaskazini ya Chadema inayoundwa na mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro ilitangaza kumsimamisha ukatibu wa mkoa wa Kilimanjaro Basil Lema kwa madai ya utovu wa nidhamu na kimaadili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma, Lema anadaiwa kushawishi viongozi wa majimbo kujiondoa ili kujiunga na chama kingine na kwamba shauri lake limepelekwa katika kamati ya maadili ya kanda ili kufanyiwa kazi.
Kada mwingine mwandamizi aliyezungumza na Mwananchi, amesema wakimaliza viongozi hao wanaofuata ni wale wa kanda (tunazihifadhi kwa sasa) ambao wapo mbioni kujivua uanachama wa Chadema.
Miongoni mwa viongozi wa kanda watakaojivua uenyekiti kwa hatua za mwanzo ni pamoja wahazini na makamu wenyeviti. Tayari mhazini wa Kanda ya Pwani, Patrick Assenga ameonyeshwa mlango wa kutokea baada ya kupewa barua ya kuvuliwa uanachama.
Wakati Assenga akivuliwa uanachama, Mwananchi linafahamu mmoja wa kigogo wa kanda ya kaskazini amepewa barua ya kutakiwa kujieleza kwa nini asichukuliwe hatua kwa kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho.
Hata hivyo, Assenga amevuliwa uanachama na tawi lake, huku yeye akisema haiwezekani kwani kwa nafasi yake ya uongozi ndani ya kanda ya pwani mamlaka yake ni kamati kuu hivyo waliomvua wanapaswa kusoma katiba ya chama vizuri.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini baadhi ya viongozi wanaojivua uanachama ni kundi lile linalomuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alishindwa kutetea nafasi hiyo mbele ya Lissu katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama hicho.

Katika mkutano wake na wanahabari, Kigaila alidokeza hali ya kisiasa ndani ya chama hicho imegubikwa na kile alichokiita ‘ubaguzi mkubwa’ dhidi ya wanachama wanaohusishwa na upande wa Mbowe ambao wamekuwa wakitengwa kuanzia ngazi ya kamati Kuu hadi mashinani.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa chama hicho, Januari 21, 2025, Chadema kimekuwa katika hali ya sintofahamu na mvutano uliyosababisha kuibuka kwa makundi mawili yanayomuunga mkono Lissu na Mbowe.
Mvutano uliongezeka zaidi baada ya uongozi wa Chadema kuishikilia ajenda ya No reforms, no election, ‘Bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ hatua iliyosababisha kuibuka kwa kundi la G55 linalotaka chama hicho kishiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba, likisema kuzuia uchaguzi ni jambo lisilowezekana.
Uwepo G55 ulisababisha mgawanyiko ndani ya Chadema kwa baadhi ya makada wakiwemo wajumbe wa kamati kuu kuonyesha kutokubaliana na msimamo wa No reforms, no election huku wengine wakiunga mkono ajenda hiyo.
Mojawapo mwa sababu inayodaiwa kuwasukuma baadhi ya makada kuondoka Chadema ni pamoja na kusaka jukwaa jipya ili kutimiza ndoto zao za kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani ambapo wanaamini wakiendelea kusalia katika chama hicho hawatafanikiwa.
Kutofanikiwa huko kunatokana na msimamo uliotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) iliyosema Chadema hakitashiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, baada ya kugomea kusaini Kanuni za Uchaguzi wa mwaka huu.
Alichokisema Heche
Akihutubia mikutano ya hadhara ya kampeni ya No reforms, no election kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Kyerwa na Karagwe jana Alhamisi, Heche amesema baadhi ya makada hao wamefika bei baada ya kupokea ahadi ya nafasi za uongozi, fedha na vifaa vya kampeni katika uchaguzi mkuu ujao.
Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini ametaja sababu nyingine iliyowakimbiza baadhi ya waliokuwa makada hao kuwa ni hasira ya kukosa nafasi za ujumbe kwenye Sekretarieti mpya ya Chadema.
"Baadhi ya waliotangaza kujiondoa Chadema wamedumu kwenye sekretarieti kwa miaka kati ya 17 hadi 22; sasa uongozi mpya umewateuwa wanaChamadema wengine kushika nafasi hizo imekuwa nongwa," amesema Heche.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akisalimiana na wananchi wa Omurushaka Wilaya ya Karagwe waliomzuia njiani akiwa njiani kwenda mjini Kayanga yaliyo Makao Makuu ya Wilaya ya Karagwe. Heche na msafara wake alikuwa anatoka Nkwenda wilayani Kyerwa. Picha na Peter Saramba
Amewataka Watanzania kutokatishwa tamaa na wanaofika bei na kusaliti imani ya kupigania mabadiliko ya kimfumo kwenye uongozi wa nchi kwa sababu viongozi na makada wa Chadema waliosalia wataendeleza mapambano bila kuchoka wala kurudi nyuma.
Amesema tayari wanazo taarifa kuwa viongozi na makada kadhaa wa Chadema wanashawishiwa kujivua uanachama kwa ahadi mbalimbali ikiwemo fedha na vyeo.
"Sisi hatutatetereka wala kurudi nyuma katika mapambano ya kudai haki, usawa kwa wote na ustawi wa Watanzania," amesema Heche.
Amesema milango iko wazi kwa wote wanaosukumwa na tamaa ya nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao waondoke kwa sababu fursa hiyo hawataipata kupitia Chadema iwapo hakutafanyika mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi unaotoa fursa sawa kwa vyama na wagombea wote.
"Tunataarifa baadhi ya walioondoka wamepata ahadi ya kusaidiwa kifedha na vifaa yakiwemo magari na pikipiki ili wagombee ubunge; sasa wajiulize iwapo kweli watashinda baada ya kuhamia vyama vingine kwa sheria na mfumo huu huu kama hawakuweza wakiwa ndani ya Chadema inaungwa mkono na Watanzania wengi," amesema Heche.
Amesema licha ya mbinu zinazofanyika kuwadhoofisha, viongozi wa Chadema hawatarudi nyuma katika kampeni ya No reforms, no election hadi mabadiliko yatakapofanyika.