Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 10 ya Majaliwa ilivyoonyesha upekee

Muktasari:

  • Julai 2, 2025, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitangaza hatagombea tena ubunge wa Ruangwa. Alianza kuwawakilisha wananchi wa Ruangwa tangu mwaka 2010.

Dar es Salaam. Miaka 10 ya Kassim Majaliwa kama Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ya kipekee machoni mwa Watanzania, kuanzia kwenye uteuzi wake hadi sasa anapoondoka katika ofisi hiyo.

Pia, utendaji wake katika kipindi hicho umempambanua kama kiongozi anayetaka kuona matokeo na amepambana kuhakikisha wabadhirifu wa mali za umma na wazembe wanachukuliwa hatua za kinidhamu.

Jana Jumatano, Julai 2, 2025, Majaliwa alitangaza kutogombea tena ubunge katika Jimbo la Ruangwa kwa kile alichoeleza kuwa anatoa nafasi kwa wana-Ruangwa wengine wapenda maendeleo ili waunganishe nguvu katika kuleta maendeleo jimboni humo.

Uamuzi huo unamaanisha Majaliwa hataweza kuendelea kuwa Waziri Mkuu baada ya uchaguzi mkuu, kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kwamba Waziri Mkuu lazima awe mbunge wa jimbo.

Akiwa Waziri Mkuu wa 10 baada ya uhuru wa Tanzania, Majaliwa amefanya kazi na marais wawili--hayati John Magufuli, aliyemteua kwa mara ya kwanza kuwa Waziri Mkuu, na Samia Suluhu Hassan, aliyechukua madaraka baada ya kifo cha mtangulizi wake.

Magufuli alimteua Majaliwa katika awamu zake zote mbili, mara ya kwanza ilikuwa Novemba 19, 2015 na mara ya pili Novemba 16, 2020. Hata Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021, aliendelea naye, akimwacha katika nafasi hiyo.

Jambo la kipekee katika uteuzi wake ni kwamba jina lake lilipelekwa bungeni kwa Spika wa Bunge wa wakati huo, Job Ndugai, moja kwa moja na Mpambe wa Rais (ADC), tofauti na ilivyozoeleka miaka ya nyuma.

Majaliwa (64) aliteuliwa kushika nafasi hiyo akitoka kwenye nafasi ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi). Kwa sasa Tamisemi iko ofisi ya Rais. Kwa maneno mengine, ni kwamba hakuwahi kuwa waziri kamili, kama ilivyokuwa kwa mawaziri wakuu waliomtangulia.

Licha ya hilo, amefanya kazi kwa miaka 10, akifikia rekodi ya pekee iliyokuwa ikishikiliwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, aliyehudumu katika nafasi hiyo wakati wa Serikali ya awamu ya tatu (1985–1995).

Atakavyokumbukwa

Mwanahabari mkongwe, Absalom Kibanda amesema Majaliwa amefanikiwa kuondoka katika nafasi hiyo bila msukumo wa kashfa nyuma yake, kama ilivyokuwa kwa mawaziri wakuu waliomtangulia.

Amesema kama ilivyokuwa kwa Cleopa Msuya, Majaliwa pia amefanya kazi na marais wawili wenye hulka na mitazamo tofauti, hivyo ameweza kuishi na kufanya nao kazi kwa kadri ya mazingira na maelekezo yao.

“Kikubwa ni hulka yake binafsi ya kuwa na utulivu. Pia, nimejifunza kwamba Majaliwa akienda mikoani alikuwa ni kiongozi anayeogopwa kuliko hata viongozi wengine wakuu wa kitaifa, hasa zama hizi za Rais Samia,” amesema.

Ameongeza ni Waziri Mkuu muungwana ambaye anasimamia kazi, hivyo atakumbukwa zaidi kwa kuchapa kazi na kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kusudiwa.

Kuhusu aina ya Waziri Mkuu anayehitajika baada ya Majaliwa, Kibanda amesema Tanzania inahitaji kiongozi atakayebeba lawama zote za Serikali kabla haijamfikia Rais Samia mwenyewe.

“Tunahitaji Waziri Mkuu ambaye atakuwa tayari kuwajibika au kuwajibishwa, siyo kwa maana ya kujiuzulu, bali kwa maana ya utendaji. Kwamba hili kalitenda Waziri Mkuu, hili ni kwa sababu ya Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo, tunahitaji Waziri Mkuu ambaye atakuwa ngao kwa Rais, si kwa maana ya kumlinda, ni kiutendaji. Na kama kutakuwa na sifa, basi azibebe sifa hizo kama ilivyokuwa wakati wa Edward Lowassa ambaye anapewa sifa kwa shule za kata na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, licha ya kwamba zilikuwa zama za Rais Jakaya Kikwete,” amesema.

Kwa upande wake, Balozi mstaafu, Dk Benson Bana amesema sifa kubwa aliyonayo Majaliwa ni uongozi, na kwa uamuzi wa kuachia ngazi, anastahili kupongezwa kwa sababu anatoa fundisho kwa viongozi wengine kutong’ang’ania ofisini.

“Majaliwa ameonyesha njia. Huwezi ukawa mbunge miaka 30, kana kwamba wanawake wengine hawakuzaa watoto. Wapo watu wanataka kuwa wabunge wa maisha, dhana ambayo imekataliwa. Kwa hiyo Majaliwa anawakumbusha wengine,” amesema.

Dk Bana ameongeza kwamba kiongozi mzuri ni yule anayetayarisha warithi wake. Amesema Rais Samia katika hotuba yake akifunga shughuli za Bunge, alimwelezea kama kiongozi msikivu, mwadilifu na anayetekeleza yale anayoambiwa.

“Haikuwa rahisi kwa hayati Magufuli kumuibua mtu aliyekuwa naibu waziri kuwa Waziri Mkuu. Ni karama alizonazo Majaliwa ambazo wengine hawana,” amesema Dk Bana, aliyekuwa akiiwakilisha Tanzania nchini Nigeria.

Ameongeza Majaliwa ni mfuatiliaji mzuri. Kila akienda mahali unaona sura ya usikivu, sura ya ufuatiliaji, sura ya kuelekeza na kuchukua hatua pale inapostahili kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Humsikii na skendo zozote, humsikii na kundi lolote, Majaliwa amekuwa ni kiongozi wa mfano,” amesema.

Mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema Majaliwa amejitahidi kuchapa kazi kwa kusimamia shughuli za Serikali za kila siku na pia amewasimamia vizuri mawaziri walio chini yake na kuendeleza ushirikiano na Bunge.

“Ni mtu mtulivu, mchapakazi na anaonekana ana busara, yuko vizuri, Watanzania watamkumbuka kwa kusimamia miradi ya Serikali,” amesema Dk Kyauke, akiongeza kuwa kazi yake inambeba.

Kuhusu kazi anayoweza kuifanya baada ya kustaafu, Dk Kyauke amesema ataamua mwenyewe, kwani anahitaji kuendelea na kazi za kisiasa kama ilivyokuwa kwa Sumaye, atafanya hivyo. Akiamua kustaafu, pia utakuwa ni uamuzi wa busara.


CCM wampongeza

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amempongeza Majaliwa kwa uamuzi aliochukua na kwamba amefanya kazi nzuri katika kipindi chote cha uongozi wake.

“Amefanya kazi nzuri kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu, akifanya kazi nzuri wakati wa awamu ya tano ya hayati John Magufuli, lakini awamu ya sita kafanya vizuri na Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Makalla.

Makalla amesema mara ya kwanza Majaliwa kufanya kazi na Rais Samia ni tangu akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, na baada ya hapo waliendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

“Hakuna mashaka yoyote juu ya utendaji wake. Amefanya vipindi viwili na naamini ameona ni busara yeye mwenyewe kuona ametimiza mchango wake kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10, na kule kwake Ruangwa kuna vijana wamechukua fomu,” amesema.

Amesema uamuzi huo amependekeza mwenyewe kwa kuamua kutochukua fomu, na chama kinampongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika jimbo lake, na pia kitaifa kama msimamizi wa shughuli za Serikali.

“Tunampongeza kwa kazi alizofanya Ruangwa mkoani Lindi kwenye jimbo lake, nimeenda limebadilika, na anaicha ikiwa na timu Ligi Kuu Tanzania Bara, Namungo, na Tanzania amefanya kazi awamu ya tano na sita. Tunashukuru kwa mchango wake na nchi yetu kwa uchapa kazi wake na niseme ni uamuzi mzuri na wa busara,” amesema.