Prime
Mawaziri wa Kikwete, JPM wanavyopambana kurejea mjengoni

Muktasari:
- Miongoni mwa mawaziri hao wa zamani walioibuka kuonyesha nia ya kuutaka ubunge, yumo William Ngeleja, Aggrey Mwanri, Stephen Masele, Lazaro Nyalandu, Lawrence Masha na Dk Charles Tizeba.
Dar es Salaam. Ukiacha makundi ya vijana, wanazuoni, watumishi wa umma na wanataaluma mbalimbali, uchukuaji fomu za ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), umewaibua mawaziri kadhaa ambao pengine walishasahaulika katika medani za siasa.
Unaweza kusema kuwa mchakato huo umeamsha hamu ya viongozi hao wengi waliowahi kuhudumu katika wizara kadhaa, katika awamu mbalimbali za Serikali hasa ya nne na tano chini ya marais, Jakaya Kikwete na hayati John Magufuli.
Miongoni mwa mawaziri hao wa zamani walioibuka kuonyesha nia ya kuutaka ubunge, yumo William Ngeleja, Aggrey Mwanri, Stephen Masele, Lazaro Nyalandu, Lawrence Masha na Dk Charles Tizeba.
Ingawa baadhi yao, walijitokeza katika mchakato wa uchukuaji fomu katika Uchaguzi Mkuu 2020 bila mafanikio, wamerudi tena mwaka huu, kuomba ridhaa ya CCM iwapitishe wapeperushe bendera yake.
Ipo hoja kuwa, wingi wa makundi wakiwemo mawaziri hao wa zamani wanaoutaka ubunge, unachochewa na maslahi makubwa yaliyopo kwenye shughuli ya ubunge, kwa mujibu wa mkufunzi wa uongozi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Mkakati wa Taasisi ya Twaweza, Dk Baruan Mshale.
Mwanazuoni huyo anaona, wengine huutaka ubunge wakidhani ndiyo kazi inayomweka huru zaidi mtu bila kufuatiliwa, kwa kuwa hakuna anayekusimamia muda wa kuingia na kutoka kazini.
"Kwenye ubunge unaweza usiende ofisini hakuna anayekuhoji, inachukuliwa kuwa kazi yenye maslahi makubwa, lakini inamweka huru mtendaji wake kuifanya au asifanye na hana cha kupoteza," amesema Dk Baruan.
Sababu nyingine ya wingi huo ni kile alichoeleza wapo wenye matumaini ya kuwa mawaziri iwapo wataupata ubunge, hivyo vikumbo vinavyoendelea haviilengi nafasi moja pekee, kuna malengo ya kuupata uwaziri.
Wakati mchambuzi wa siasa na jamii, Ramadhani Manyeko amesema kurejea kwa watu hao inaoonekana hawakuridhika uamuzi wa chama kwa sababu baadhi yao walishinda katika kura, lakini majina hayakurudi mwaka 2020.
Ingawa ni haki yao kuwania uongozi, wamejipima na kujiona kwamba bado wana nafasi, hasa ukizingatia kwamba Mwenyekiti wa sasa wa CCM ni Rais Samia Suluhu Hassan, na wanaamini kuwa haki itatendeka.
"Wanaamini haki itatendeka na wakati walihisi kuonewa, ila hawakuwahi kutoka hadharani kulalamikka kwa sababu CCM chama dola. Ingawa watu wao wa karibu walisikika wakidai kulikuwa uonevu mkubwa kwenye mchakato huo.
"Sasa wameamua kujiuliza kwa awamu nyingine, wengi wao wanaamini bado wana ushawishi na kukubalika. Wengine wanaitumia kama fursa, hawaamini kushinda bali wanaitumia kama fursa nyingine ikiwemo kupata teuzi," amesema.
Waliokuwa mawaziri wenyewe
Mchakato huo wa ndani wa CCM mwaka huu, umemuibua waziri wa zamani wa nishati na madini, William Ngeleja, ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005.
Ubunge wake ulimsababishia kuukwaa wadhifa wa uwaziri, alipoteuliwa na Rais Kikwete mwaka 2007 hadi 2008 lilipovunjika baraza la mawaziri, baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu kwa kashfa ya Escrow.
Baadaye Kikwete alimrudisha Ngeleja katika wadhifa huo alipoongoza hadi mwaka 2010 na aliteuliwa tena baada ya uchaguzi wa mwaka huo, kuendelea na uwaziri wa nishati na madini hadi 2012, kabla ya kurithiwa na Profesa Sospeter Muhongo.
Ngeleja amejitokeza kuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Sengerema, atakakochuana na Hamis Tabasamu anayewania kutetea nafasi yake aliyoikalia kuanzia mwaka 2020.
Aggrey Mwanri
Mwanri amewahi kuhudumu kwa nafasi ya ubunge wa Siha kwa miaka 15 kuanzia 2000 hadi 2015. Akiwa na nafasi hiyo, aliteuliwa na Kikwete kuwa Naibu wa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi- wakati huo).
Kati ya mwaka 2010 hadi 2015, Mwanri alikuwa ofisi moja na Kassim Majaliwa aliyekuwa akishughulikia sekta ya elimu katika Tamisemi.
Mwaka 2015 alishindwa kutetea ubunge mbele ya Dk Godwin Mollel aliyekuwa Chadema wakati huo.
Mwanri amerudi tena Siha kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM imteue kupeperusha bendera katika kinyang'anyiro cha ubunge katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
Naibu waziri hiyo wa zamani atachuana na Dk Godwin Mollel ambaye naye ameshachukua fomu kutetea nafasi yake pamoja na makanda wengine
Stephen Masele
Ukiacha Mwanri, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Stephen Masele naye anautaka tena ubunge wa Shinyanga Mjini.
Mbali na wizara hiyo, Masele amewahi pia kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Katika kura za maoni ndani ya CCM, Masele aliongoza, lakini jina lililorudi baada ya vikao vya juu vya chama ni la Patrobas Katambi ambao wote wanachuana tena.
Lazaro Nyalandu
Baada ya ukimya wa kitambo kidogo katika ulingo wa siasa, waziri wa zamani wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu amerudi tena kuomba ridhaa ya CCM imteue kuwania ubunge.
Historia ya Nyalandu katika wadhifa wa ubunge ni ndefu kiasi, kwani amehudumu kwa zaidi ya muongo mmoja tangu 2000 hadi 2017, alipojiuzulu na kujiunga na Chadema.
Mwaka 2021 alirejea CCM na sasa anaomba ridhaa ya kuwania ubunge katika jimbo jipya la Ilongero mkoani Singida.
Ezekiel Maige
Huyu naye amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, lakini alianza na nafasi ya unaibu waziri wa wizara hiyo chini ya Rais Kikwete. Maige amejitokeza kuomba ridhaa ya ubunge wa Msalala.
Lawrence Masha
Masha aliyechukua fomu kuomba ubunge wa Nyamagana, aliingia bungeni mwaka 2005 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, akitajwa kuwa ndiye waziri mdogo.
Mwaka 2010 alishindwa kutetea nafasi yake mbele ya Ezekia Wenje wa Chadema. Tangu mwaka 2020, jimbo la Nyamagana linaongozwa na Stanslaus Mabula wa CCM ambaye pia amechukua fomu kutetea ubunge wake.
Dk Steven Kabwe
Aliwahi kuwa mbunge wa Serengeti na Naibu Waziri wa Afya, lakini mwaka 2015 alishindwa kutete kiti mbele ya Marwa Warioba wa Chadema. Sasa analitaka tena jimbo hilo ambalo linaongozwa na Jeremiah Amsabi wa CCM. Amsabi naye amejitosa kutetea nafasi hiyo.
Christopher Chiza
Amewahi kuwa mbunge wa Buyungu Kigoma kuanzia 2005 hadi 2015 aliposhindwa mbele ya Kasuku Bilago wa Chadema, ambaye sasa ni marehemu.
Amewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Umwagiliaji mwaka 2012 hadi 2015
Dk Charles Tizeba
Amewahi kuwa mbunge Buchosa na Waziri wa Kilimo. Mwaka 2020, aliangushwa na Eric Shigongo wa CCM, ambaye pia amechukua fomu kutetea ubunge wake tena.
Kangi Lugola
Amewahi kuwa mbunge wa Mwibara mkoani Mara kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. Aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, kabla ya kupandisha hadhi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Dk Titus Kamani
Huyu amewahi kuwa mbunge wa Busega mwaka 2010 hadi 2015. Mwaka 2015-2020 alishindwa na Raphael Chegeni ambaye naye mwaka 2020 aliangushwa. Wote wawili wamejitosa tena kuwania ubunge. Amewahi kuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo kuanzia mwaka 2014 hadi 2015.
Godfrey Zambi
Amewahi kuwa mbunge wa Mbozi mkoani Songwe, kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2015 aliposhindwa kutetea nafasi hiyo mbele ya Pascal Haonga wa Chadema. Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo
Mary Mwanjelwa
Alikuwa mbunge wa viti maalumu katika awamu zilizopita, amewahi kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), pia amewahi kuwa naibu waziri wa kilimo.
Charles Kitwanga
Amewahi kuwa mbunge wa Misungwi, Mkoa wa Mwanza, kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. Mwaka 2020 alishindwa katika kura za maoni na Alexander Mnyeti.
Mwanasiasa huyo amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia, ukiachana na wadhifa huo Kitwanga amebobea kwenye utalaamu wa teknolojia ya habari.
Kitwanga amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Naibu Waziri wa Madini wa Nishati na Madini.