Prime
Mnyukano bungeni na joto la urais CCM 2030
Muktasari:
- Imedaiwa kuwa, kuna kiongozi anazunguka makanisani na kutumia majina ya viongozi wastaafu kutafuta huruma ya wananchi na kufanya usaliti wake, kiasi cha kukwaza maendeleo
Dar es Salaam. Vuguvugu la urais mwaka 2030 kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM), limeibukia bungeni na kusababisha mnyukano ndani ya muhimili huo wa kutunga na kusimamia utekelezwaji wa sheria.
Mnyukano huo, uliibuliwa na mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Simai Mohamed Said aliyedai kuna kiongozi ndani ya Serikali anafanya usaliti akimwita Yuda bila kumtaja jina.
Katika hoja yake hiyo, amedai kiongozi huyo anazunguka makanisani na kutumia majina ya viongozi wastaafu kutafuta huruma ya wananchi na kufanya usaliti wake, kiasi cha kukwaza maendeleo.
Itakumbukwa, Simai huyo huyo, Mei 22, 2026 ndiye aliyeibuka na hoja ya kuwasihi wana CCM wasiyumbishwe na siasa za urais wa mwaka 2030, akisisitiza yeyote anayeanza harakati hizo na kumdharau Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, hatafanikiwa.
Hoja hizo za Simai bungeni zimeibua mjadala hata nje ya muhimili huo. Wapo wanaohoji Yuda huyo ni nani? Wengine wanaonya hatari ya tuhuma hizo, kadhalika wapo wanaosema kinachosemwa na mbunge huyo ni dalili ya upepo mchafu ndani ya CCM kuelekea urais wa 2030.
Vuguvugu la urais 2030, liliwahi kumwibua Makamu Mwenyekiki wa CCM Bara, Stephen Wasira Machi 27, 2026 alipowaonya makada wa chama hicho waache harakati za mapema za kujipanga kwa urais wa mwaka 2030.
Siku mbili kabla ya kauli ya Wasira, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda akiwa mkoani Arusha, aliwaambia wanaojipanga kwa urais mwaka 2030, hawatafanikiwa katika mbio hizo.
Hata Rais Samia naye, alizungumzia hilo Desemba 2, 2025 katika mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam, alipowatahadharisha wateule wake wenye nia ya urais 2030, waachie nafasi alizowapa, ili wafanye harakati hizo wakiwa nje ya Serikali.
Kauli ya Simai
Katika mchango wake katika bajeti ya Wizara ya Fedha juzi Jumanne Juni 2, 2026, mbunge huyo Simai kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar amesema ndani ya Serikali kuna viongozi wasaliti aliowafananisha na Yuda.
“Leo nambatiza mmoja aliyekuwepo ndani ya Serikali, ni Yuda. Nasema hivyo kwanini, sisi tunataka maendeleo ya nchi yetu, kosa la mama ni wapi? Kwa sababu ya kumuamini mtu kumbe ni Yuda,” amehoji.
Amesisitiza kiongozi huyo msaliti ameibuka hadi katika nyumba za ibada akitafuta huruma za watu na kutumia majina ya viongozi wastaafu ilimradi aoneshe anapendwa.
“Leo anapita akitaka kutuaminisha sisi kwamba, Rais Magufuli (hayati John, Rais wa awamu ya tano) alimpenda sana yeye Yuda. Kama alimpenda kweli mbona alimrusha huko nje ya dunia huko alitupwa, huko alitupwa,” amesema.
Amesema waliompenda hayati Magufuli wanajulikana na hadi sasa wapo, hivyo kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 21, 2021 aachwe apumzike kwa amani kwa kuwa alifanya kazi nzuri.
“Yuda aache kutumia majina ya watu, tuamkeni wabunge na tusiogope, mimi siwezi kutia ulimi wangu puani. Haya maendeleo tunayoyataka lazima tuhakikishe Serikali inapata utulivu, mawaziri wanakuwa na amani na sisi tunaacha kuchonganishwa,” amesema Simai.
Hata hivyo, hoja ya Simai, imekosolewa na mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu aliyewasihi wabunge wa CCM kutoruhusu homa yao ya siasa za 2030, iharibu mijadala ya Bunge.
“Kuna ladha katika siasa, lakini tukitia chumvi sana na sasa ndio kwanza kunakucha hakuna wizara tutajadili humu ndani,” amesema Ado.
Sumaye aonya
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameonya Bunge lisitumike kama chombo cha kuchafuana kisiasa, kwa sababu hilo si miongoni mwa majukumu ya muhimili huo.
Amesema hata kanuni za Bunge, zinakataza kutoa tuhuma ambazo huna uhakika nazo na katika mazingira yaliyotokea, mbunge alipaswa kuombwa ushahidi wa anachokizungumza.
“Kanuni zinakataza kutoa tuhuma ambazo huna uhakika na ilitakiwa huyo mbunge aliposema hayo, Spika amsimamishe au mbunge mwingine amsimamishe kumtaka aoneshe ushahidi wa tuhuma za usaliti anazozitoa,” amesema.
Sumaye, aliyekuwa mtendaji mkuu wa Serikali kwa muongo mmoja, amesema kanuni hizo pia, zinakataza kumsema vibaya au kumtuhumu mtu ambaye hayuko ndani ya Bunge kwa wakati huo, kwani anakosa nafasi ya kujitetea.
“Pia, kanuni za Bunge zinakataza kumzungumzia vibaya mtu ambaye hayupo bungeni, kwani hawezi kujitetea,” amesema.
Wangeyamaliza ndani
Mtaalamu wa utatuzi wa Migogoro, Deus Kibamba amesema alitarajia tuhuma na hoja za Simai zingetolewa ndani ya vikao vya CCM ili kuyamaliza.
“Bunge ni sehemu ya kutoa ushauri wa maendeleo kwa Serikali, lakini hoja aliyoiwasilisha haikuwa katika mahala pake. Alipaswa kutumia vikao vya chama kwa kuwa ni mjumbe wa vikao mbalimbali vya chama,” amesema.
Kibamba amesema mjadala huo haukuwa unahusu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), bali ulihusu Wizara ya Fedha, hivyo wengi walitarajia mbunge huyo angejikita katika masuala ya mapato.
“Nilishangazwa na hotuba yake yote. Najiuliza, nani alimtuma Simai? Je, alikuwa ametumwa na mtu aliyekuwa akimtetea, au alizungumza kwa mtazamo wake kama Mzanzibari? Kama Simai alitumwa na mtu yeyote, basi hali hiyo si nzuri kwa mujibu wa sayansi ya siasa,” amesema.
Amesema Watanzania wanafahamu kuwepo kwa mpasuko wa kisiasa unaoendelea kujitokeza katika mazingira hayo.
Amesisitiza CCM inapaswa kumwandikia barua Simai ili kujua alimaanisha nini na alimlenga nani aliyemwita Yuda ili kuepusha mgogoro kuimarika zaidi.
Bunge halikuwa jukwaa sahihi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Onesmo Kyauke amesema Bunge si mahali sahihi pa kutoa tuhuma au kuzungumzia mafumbo ya kisiasa, kufanya hivyo ni kuutumia vibaya muhimili huo.
“Aliyekuwa anaongoza kikao hicho alikosea kumruhusu kuendelea kuzungumza, kwa sababu mambo yanayozungumzwa bungeni huingia kwenye rekodi rasmi,” amesema.
Kyauke amesema maelezo yaliyotolewa yalifanana zaidi na taarabu za kisiasa na hayakupaswa kuwasilishwa katika ukumbi huo, ambao jukumu lake kuu ni kujadili na kutatua changamoto za wananchi.
“Kama kweli kulikuwa na tatizo ndani ya CCM, chama hicho kina idara na mifumo yake ya kushughulikia matatizo. Si sahihi kwa mbunge ambaye si sehemu ya utawala kulalamikia jambo hilo bungeni. Hata kama tatizo lingekuwepo, CCM ina utaratibu wake wa kulishughulikia,” amesema.
Kumekosekana kuaminiana
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa George Kahangwa amesema tuhuma hizo zinaweza kuiyumbisha Serikali, hivyo kushusha kiwango cha utendaji.
“Utendaji wa Serikali hautakuwa wa kawaida kwa sababu hali ya kuaminiana haitakuwepo. Ikiwa huna imani na mwenzako mnayefanya kazi pamoja, kunakuwa na tatizo. Hali inavyoonekana inaashiria kuwa kuna siri zinazovuja kutoka ndani ya Baraza la Mawaziri,” amesema.
Ili kurejesha hali ya kuaminiana, amesema Rais anaweza kulivunja Baraza la Mawaziri na kuunda jipya, hatua inayoweza kusaidia kurejesha imani miongoni mwa viongozi.
Amesema iwapo hatua za kuziba ufa hazitachukuliwa sasa, hali inaweza kuwa mbaya zaidi, hususan kwa anayehusishwa na tuhuma hizo.
“Kuna uwezekano wa kuzuka mgogoro mkubwa na inaweza kufikia hatua ya mtu anayehusishwa na tuhuma hizo kupelekwa bungeni na kushughulikiwa,” amesema.
Akifafanua hoja yake, Profesa Kahangwa amesema matukio kama hayo yamewahi kujitokeza katika nchi nyingine hivi karibuni ikiwamo Senegal, Rais Bassirou Diomaye Faye na aliyekuwa Waziri Mkuu wake, Ousmane Sonko, walitofautiana hadharani hadi Rais akamwondoa Waziri Mkuu huyo.
“Mwaka 2024, Kenya, Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais wake, Rigathi Gachagua, walitofautiana hadi Bunge likamwondoa Gachagua madarakani. Tanzania hatutaki kufikia hali kama hiyo. Ikiwa kuna tuhuma, ni vyema ziwe na ushahidi wa kutosha.
“Tuhuma hizi za usaliti zisipite bila kufafanuliwa, Watanzania wana haki ya kujua ukweli. Taratibu za kushughulikia tuhuma za usaliti zipo na pia zipo taratibu za kushughulikia tuhuma za uongo,” amesema.
Chanzo cha makundi
Profesa Kahangwa amesema kauli zilizotolewa zimeibua makundi na zinachochea chuki.
“Hawawezi kulivuka salama jambo hili ndani ya chama (CCM) kwa sababu tayari wameonekana kutofautiana na Watanzania wameona kuna tatizo kubwa. Tayari ndani ya CCM kuna dalili za kuibuka kwa makundi,” amesema.
Amesema hali hiyo inaonesha kuna masuala ambayo chama kinapaswa kuyatatua ndani ya mifumo yake badala ya kuyaacha yafikie vyombo vya dola.
“Tunatarajia CCM itamwita mwanachama wake kwa ajili ya mahojiano na baadaye kutoa taarifa kwa umma ili kuthibitisha tuhuma za usaliti alizozitoa, kwa kuwa ni tuhuma nzito zinazohitaji ufafanuzi,” amesema.
Amesema wapo viongozi waliowahi kutoa tuhuma nzito bungeni na kutakiwa kuzithibitisha miongoni mwao ni Augustino Mrema na Zitto Kabwe, hata mtoa tuhuma hizo aitwe ahojiwe na kuthibitisha tuhuma hizo.
“Athari nyingine ya tuhuma hizi ni kuibua taharuki kubwa miongoni mwa wananchi. Mtoa tuhuma anapaswa kuwajibika kwa kauli zake kwa kuitwa na kupewa nafasi ya kuzithibitisha. Vilevile, kauli hizo zinaweza kuwa zimehatarisha usalama wa anayetuhumiwa,” amesema.
Doyo aingilia kati
Akiwa mkoani Tanga, katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi Jumanne Juni 2, 2026 baada ya kuhitimisha ziara yake ya kichama mkoani humo, Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo amesema baadhi ya kauli zinazotolewa na wanasiasa katika majukwaa mbalimbali zimeibua mjadala kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.
“Kikatiba na kisheria kila mwenye sifa ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hata hivyo, tunaamini kipindi hiki ni muhimu zaidi kuelekeza nguvu katika maendeleo na ustawi wa wananchi,” amesema Doyo.
Mbeto anena
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo upande wa Zanzibar, Khamis Mbeto, amesema kwa kuwa mbunge anapozungumzia bungeni anakuwa na kinga, inakuwa vigumu kuingilia alichokisema.
Ugumu mwingine wa kuingilia hilo, amesema unatokana na ukweli kwamba, Simai hakutaja jina la huyo aliyemwita Yuda, akisisitiza iwapo angetaja mapema angeshapokea wito katika kamati ya maadili ya chama hicho kwa mahojiano.
Alipoulizwa iwapo wana mpango wa kumwita ili awatajie jina la huyo aliyemwita Yuda, Mbeto amesema huenda akaitwa baadaye baada ya mashauriano na mawasiliano ya viongozi wa chama hicho.
“Suala la kumwita ili kujua huyo Yuda aliyemtaja huenda baadaye likatokea lakini halijapangwa. Na jambo hilo ni la kitaalamu, lazima lihusishe mawasiliano ya viongozi na mashauriano kabla ya kulifanya,” amesema Mbeto.