Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jani la mahindi lilivyozima ndoto ya familia 

Muktasari:

  • Rose David, aliyekuwa mkulima hodari katika Kata ya Ntokela wilayani Rungwe, kwa miaka mitatu sasa ana upofu uliosababishwa na jani la mahindi lililojeruhi jicho lake.



Mbeya. Nyumba ndogo yenye nyufa ukutani ndiyo imekuwa makazi ya Rose David (40). Ndani yake kuna kimya kizito kinachobeba maumivu, simanzi na simulizi ya miaka mitatu ya maisha yaliyogeuka giza nene.

Wengi wanaomwona leo hawawezi kuamini kuwa miaka michache iliyopita alikuwa miongoni mwa wakulima hodari katika Kata ya Ntokela, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Kilimo kilikuwa uti wa mgongo wa familia yake. Kilimpatia chakula, kiliwasomesha watoto na kumpa matumaini ya maisha bora ya baadaye.

Lakini siku moja, asubuhi alipokuwa shambani akivuna mahindi, kila kitu kilibadilika. Leo anaishi na ulemavu wa kutoona, huku watoto wake wakigeuka tegemeo la familia.

Rose David (40), mwanamke mwenye ulemavu wa uoni hafifu na mkazi wa Kata ya Ntokela, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, akiwa amepiga magoti nje ya nyumba anayoishi. Picha na Hawa Mathias.

Rose anasema matatizo yalianza mwaka 2017 baada ya jicho lake la kushoto kuanza kusumbua. Alitafuta matibabu katika hospitali mbalimbali akaambiwa tatizo lilikuwa ndani ya jicho.

Mwaka 2024, alipokuwa akivuna mahindi kwa ajili ya chakula cha familia, jani la zao hilo lilichoma jicho lake la pili, ambalo tayari lilikuwa lina dalili za kuwa na changamoto kama lile la kushoto.

"Nilidhani ni jeraha la kawaida. Nilizunguka hospitali mbalimbali nikitafuta matibabu, nikaambiwa kuna kidonda ndani ya jicho. Baada ya hapo uwezo wangu wa kuona ukaendelea kupungua hadi nikapoteza kabisa nuru ya macho," anasema.

Anasema siku aliyogundua kuwa hawezi tena kuona ndiyo ilikuwa mwanzo wa maisha ambayo hakuwahi kuyatarajia.

"Hapo ndipo niligundua kuwa siwezi tena kulima, kufanya biashara wala kutafuta kipato. Nilijikuta nalazimika kukaa ndani muda wote, huku msaada wangu mkubwa ukiwa watoto, ambao pia waliacha masomo baada ya mimi kupata upofu wa kudumu," anasema.


Ndoto zakayeyuka

Rose anasema upofu haukumwathiri yeye pekee, bali uliigusa familia nzima.

Anasema kuanza kwa matatizo yake ya macho kulisababisha watoto wake wanne washindwe kuendelea na masomo kwa sababu familia haikuwa tena na uwezo wa kugharimia mahitaji ya shule.

Mtoto wake wa kwanza Amani David (26), aliacha shule akiwa darasa la sita, wa pili Ester David (19), aliishia darasa la tatu, Faidhia David (16) aliishia darasa la nne na Mwamini David (14) hakupata elimu, na sasa ndiye anaishi na wazazi wake na kutunza familia.

Muonekano wa nyumba anayoishi Rose David (40), mlemavu wa uoni hafifu, aliyojenga kabla ya kupata ulemavu wa kudumu uliomfanya ashindwe kukamilisha ujenzi huo. Picha na Hawa Mathias.

Mbali ya hayo, Rose anasema ana wajukuu wawili Stephen Sitamanga (4) na Nasia Mussa (13), ambaye ni mwanafunzi darasa la saba katika Shule ya Msingi Masaki. Baada ya masomo anasema hurejea nyumbani kuhudumia familia.

"Miaka mitatu iliyopita ndiyo ilikuwa mwisho wangu kuona mwanga wa dunia, lakini kilichoniumiza zaidi ni kuona watoto wangu wakikosa haki yao ya elimu kwa sababu siwezi tena kuwahudumia," anasema huku akitokwa na machozi.

Anasema mara nyingi familia hulala njaa kwa kukosa chakula, huku mume wake David Philipo (60) akiwa na ugonjwa wa pumu unaomzuia kufanya kazi nzito za kutafuta kipato.

"Kuna siku tunalala bila kula. Maisha yamekuwa magumu sana," anasema na kuongeza, badala ya kuwa darasani, watoto wake sasa hutafuta vibarua ili familia ipate chakula.

"Inauma sana kuona watoto waliopaswa kusoma ndio wanaotafuta fedha za kutulisha sisi wazazi. Lakini sina namna, namwachia Mungu," anasema.


Pigo baada ya upofu

Kana kwamba upofu haukutosha, Rose anasema familia ilikumbwa na msiba mwingine.

Mdogo wake wa kiume, aliyekuwa msaada mkubwa kwa familia hasa katika mahitaji ya watoto, aliuawa na watu wanaodaiwa kukodi pikipiki yake. Baada ya mauaji waliondoka nayo.

Ananyamaza kwa sekunde kadhaa kisha anasema: "Mdogo wangu alikuwa msaada mkubwa kwangu. Alikuwa akiwasaidia watoto wangu lakini aliuawa na watu waliokodi pikipiki yake. Hilo liliniumiza sana."

"Ukipata matatizo ndipo unajua watu wanaokupenda kweli. Leo watoto wangu na mume wangu ndiyo kila kitu kwangu na msaada wa karibu licha ya maumivu makali wanayopata kila wanionapo," anasema.


Makazi yatia hofu

Mbali na changamoto za afya na kipato, Rose anasema nyumba wanayoishi imeharibika kiasi cha kutishia usalama wao.

Kuta zimepasuka, huku choo kikiwa hakifai kwa matumizi ya binadamu.

Anasema kabla ya kupoteza uwezo wa kuona hakuwa akiwaza kwamba siku moja angeishi katika mazingira hayo, kwani mbali na kilimo alikuwa akifanya pia vibarua mbalimbali kujiongezea kipato.

"Nilikuwa mkulima mzuri. Nilijenga nyumba hii kwa nguvu ya kilimo. Leo siwezi hata kuitengeneza (kuikarabati). Kibaya zaidi naishi kwa kutegemea dawa za kutuliza maumivu ili kupunguza mateso ninayopata, hususan nyakati za usiku," anasema.


Ombi la msaada

Rose anasema kilichobaki kwake sasa ni matumaini.

"Naomba nipate matibabu, watoto wangu warudi shule, familia yangu ipate chakula na makazi salama. Hayo ndiyo matumaini yangu yaliyobaki," anasema na kuongeza:

"Natambua wapo Watanzania wenye mapenzi mema, Rais Samia Suluhu Hassan na hata wabunge waguswe kunisaidia, kwani watoto bila elimu mimi nitaishije safari ya uzeeni?"


Wanavyomfahamu

Alphonce Sanga, jirani wa Rose anasema anamfahamu tangu akiwa mwenye afya njema akijishughulisha na kilimo.

"Alikuwa miongoni mwa wakulima waliojituma sana. Alijenga nyumba yake kwa fedha za kilimo. Baada ya kupata upofu amebaki ndani muda mwingi na maisha yake yamebadilika kabisa," anasema.

Muonekano wa choo kinachotumiwa na familia ya Rose David (40), mlemavu wa uoni hafifu na mkazi wa Kata ya Ntokela, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya. Picha na Hawa Mathias.

Diwani wa Ntokela, Fanuel Tweve anasema Rose ni miongoni mwa wananchi wanaokabiliwa na changamoto kubwa za maisha na wanahitaji msaada wa haraka.

"Ni kweli familia hii inapitia kipindi kigumu. Tunashukuru Taasisi ya Tulia Trust imefika kujionea hali halisi na kuanza kuwapa matumaini mapya," anasema.


Mwanga wa matumaini

Baada ya kufika nyumbani kwa Rose na kujionea hali halisi ya maisha yake, Taasisi ya Tulia Trust chini ya Mkurugenzi wake, Dk Tulia Ackson imeanza mchakato wa kumsaidia yeye na familia yake.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa taasisi hiyo, Joshua Mwakanolo anasema familia hiyo inahitaji msaada wa haraka wa matibabu, chakula, kuboresha makazi na kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kurejea shuleni.

"Tulichokiona kinagusa moyo. Hii ni familia inayohitaji msaada wa wadau mbalimbali ili kurejesha matumaini yao. Sisi tumeanza hatua za kuwawezesha katika maeneo ya msingi," anasema.