Zaidi ya Sh7 bilioni kutumika kujenga chuo cha Veta Mbozi
Mwonekano wa Majengo ya chuo cha Veta kinachojengwa wilayani Mbozi.
Muktasari:
- Cheyo amesema mradi huo mpaka sasa umepokea zaidi ya Sh5.3 bilioni sawa na asilimia 68.8 ya gharama za makadirio ya mradi huo.
Mbozi. Zaidi ya Sh7 bilioni zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kinachojengwa wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe, huku mradi huo ukiwa umefikia asilimia 70 na ukitarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Julai 2, 2026, na Ofisa Udhibiti Ubora wa Elimu wa Shule za Msingi Wilaya ya Mbozi, Michael Cheyo.
Amesema mpaka sasa mradi huo umepokea zaidi ya Sh5.3 bilioni, sawa na asilimia 68.8 ya fedha zinazokadiriwa kugharimu ujenzi wake.
Alikuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir ambaye yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku moja kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
Cheo amesema zaidi ya Sh5 bilioni tayari zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa ujenzi utakamilika kwa wakati ili chuo kianze kutoa mafunzo kwa vijana kama ilivyopangwa.
"Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2026, huku chuo kikitarajiwa kudahili wanafunzi wa kwanza na kuanza rasmi mafunzo Januari 2027," amesema Cheyo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Wanu, amepongeza maendeleo ya ujenzi na kusisitiza umuhimu wa kuukamilisha kwa wakati ili vijana waanze kunufaika na mafunzo ya ufundi stadi yanayohitajika katika soko la ajira.
"Nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi huu pamoja na ubora wa majengo. Nawapongeza wananchi wa Mbozi na Mkoa wa Songwe kwa sababu chuo hiki kitakuwa fursa muhimu ya kuwajengea vijana ujuzi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi," amesema Wanu.
Amesema chuo hicho ni sehemu ya vyuo 65 vya Veta vinavyojengwa nchini kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Amesema ujenzi ulianza mwaka 2023 ukiwa na makadirio ya awali ya Sh3.31 bilioni, lakini kutokana na upanuzi wa wigo wa mradi na mahitaji ya miundombinu, gharama zimeongezeka na kufikia zaidi ya Sh7 bilioni.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo 25, ambayo ni jengo la utawala, maktaba, madarasa, bwalo na jiko, karakana saba, nyumba tano za watumishi, mabweni manne, vyoo vya nje, kibanda cha mlinzi na jengo la kupokea umeme.
Kwa upande wake, Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga amemshukuru Wanu kwa kutembelea Wilaya ya Mbozi na kumuomba kuendelea kuisemea wilaya hiyo ili ipate fursa zaidi za maendeleo, hususan katika sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi.
Ziara ya Naibu Waziri imelenga kukagua maendeleo ya miradi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na kusikiliza changamoto zinazokabili utekelezaji wa miundombinu ya elimu mkoani Songwe.