Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shakira alivyogoma kuzeeka, muonekano wake gumzo

Muktasari:

  • Muonekano wake akiwa na miaka 49, watikisa dunia wanawake wengi wakionesha kutamani muonekano huo, wataalamu watahadharisha.

Dar es Salaam. Muonekano wa mwanamuziki maarufu wa Colombia, Shakira, akiwa na umri wa miaka 49 umeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wanawake duniani, huku wengi wakisema amewapa hamasa ya kujitunza na kuamini kuwa umri hauondoi mvuto wa mwanamke.

Mjadala huo umechukua kasi zaidi baada ya Shakira kutumbuiza kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026, ambapo alionekana mwenye nguvu, uwezo mkubwa wa kucheza na kujiamini mbele ya mamilioni ya watazamaji duniani.

Baada ya onyesho hilo, picha na video zake zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku wanawake wengi wakieleza kuvutiwa na namna mwanamuziki huyo anavyoendelea kuwa na mwonekano wa ujana licha ya kuwa karibu kutimiza miaka 50.

Kwa baadhi ya wanawake, Shakira si tu msanii mwenye kipaji, bali ni mfano wa mwanamke anayethibitisha kuwa kujitunza, nidhamu na maisha yenye afya vinaweza kusaidia mtu kuendelea kuonekana vizuri kadiri umri unavyoongezeka.

“Kinachonivutia kwa Shakira si sura yake pekee, bali nguvu anazoonyesha akiwa jukwaani. Ana miaka 49 lakini ana uwezo wa kucheza na kutumbuiza kwa muda mrefu bila kuonekana kuchoka. Hilo linatoa hamasa kwa wanawake wengi kujali afya zao,” amesema Latifa Mushema.

Mwingine amesema muonekano wa Shakira umemfanya atambue umuhimu wa kuwekeza katika afya badala ya kuangalia urembo wa nje pekee.

“Wakati mwingine wanawake tunasahau kujitunza kwa sababu ya majukumu ya kila siku. Kumwona mtu kama Shakira kunakukumbusha kuwa mwili nao unahitaji muda na uangalizi,” amesema Amina Mfumbate.

Baadhi ya wanawake wameeleza kuwa kinachowavutia zaidi ni kujiamini kwa mwanamuziki huyo na namna anavyokubali umri wake bila kuficha au kuogopa mabadiliko yanayoambatana na kukua.

Wamesema Shakira ameonyesha kuwa mwanamke anaweza kuendelea kuwa na mvuto katika hatua mbalimbali za maisha ikiwa ataweka mkazo katika afya ya mwili na akili.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wamesema wanawake wanapaswa kuchukua somo la kujitunza kutoka kwa watu maarufu bila kujilinganisha nao moja kwa moja, kwa kuwa kila mtu ana mazingira, vinasaba na uwezo tofauti.

Mtaalamu wa lishe, Catherine Kifugo, amesema muonekano mzuri wa mwili unatokana na mchanganyiko wa mambo mbalimbali ikiwemo lishe bora, mazoezi na mtindo wa maisha.

“Lishe ina mchango mkubwa katika afya ya mwili. Mtu anayekula mlo kamili wenye matunda, mboga za majani, protini na virutubisho muhimu ana nafasi kubwa ya kuwa na mwili wenye afya,” amesema Catherine.

Msanii Shakira wakati wakitumbuiza na Burna Boy kwenye Uwanja wa MetLife katika fainali ya Kombe la Dunia 2026.

Amesema pamoja na lishe, mazoezi ya mara kwa mara husaidia mwili kuwa imara na kuongeza uwezo wa mtu kufanya shughuli mbalimbali.

“Watu wengi huangalia matokeo ya nje bila kuona juhudi zinazofanyika nyuma yake. Muonekano wa mtu kama Shakira unahitaji nidhamu ya muda mrefu katika mazoezi, chakula na namna ya kuishi,” amesema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wanawake hawapaswi kuingia katika shinikizo la kutafuta kufanana na watu maarufu kwa kutumia njia zisizo salama.

“Lengo linapaswa kuwa kuwa na afya njema na kujisikia vizuri katika mwili wako. Kila mtu ana mwili tofauti na uzuri haupaswi kupimwa kwa kipimo kimoja,” amesema Catherine.

Kwa upande wake, mwanasaikolojia, Grace Malisa, amesema umaarufu wa watu kama Shakira unaweza kuwa na athari chanya na hasi kwa wanawake.

Amesema upande chanya ni kuwa unaweza kuwahamasisha wanawake kuanza kujali afya zao, lakini upande mwingine unaweza kusababisha baadhi kujiona hawatoshi wanaposhindwa kufikia viwango vinavyoonekana kwa watu mashuhuri.

“Ni muhimu wanawake kuelewa kuwa picha na video tunazoziona mitandaoni mara nyingi zinaonyesha sehemu nzuri zaidi za maisha ya mtu. Kila mtu ana safari yake ya kipekee,” amesema.

Amesema kujiamini na kujikubali ni sehemu muhimu ya uzuri wa mwanamke.

“Urembo wa kweli hauko kwenye sura pekee. Afya ya akili, furaha na namna mtu anavyojiona vina mchango mkubwa katika mvuto wa mtu,” amesema.

Shakira ambaye amekuwa katika tasnia ya muziki kwa zaidi ya miongo miwili, ameendelea kuwa miongoni mwa wasanii wanaovutia mashabiki duniani kutokana na uwezo wake wa kuimba, kucheza na kudumisha kiwango chake cha ubora jukwaani.

Kwa wanawake wengi, mjadala kuhusu muonekano wake akiwa na miaka 49 umefungua mazungumzo mapya kuhusu namna jamii inavyopaswa kuangalia suala la uzee, urembo na afya.

Badala ya kuona kuongezeka kwa umri kama kupoteza mvuto, wengi sasa wanaamini ni hatua inayohitaji kujitunza zaidi na kuwekeza katika afya ya mwili na akili.